1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yataka kuzungumza na al Qaeda kuwaokoa raia wake

Josephat Nyiro Charo27 Septemba 2010

Makamanda wa jeshi na wataalamu wa kupambana na ugaidi kutoka nchi za aneo la Sahel walikutana jana kusini mwa Algeria kujadiliana njia za kukabiliana na kitisho cha wanamgambo wenye mafungamano na al Qaeda

https://p.dw.com/p/PNVQ
Rais wa Ufaransa, Nicolas SarkozyPicha: AP

Ufaransa inaendeleza juhudi zake za kutaka kuzungumza na watekaji nyara wa kundi lenye mafungamano na kundi la kigaidi la al aqaeda linalowazuilia mateka watano wa rehani raia wa Ufaransa na wengine wawili ya kigeni katika milima iliyoko kaskazini mwa Mali.

Mpambe mmoja wa rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy amesema wako tayari kuzungumza na watekaji nyara wa kundi la al Qaeda katika eneo la maghreb, AQIM. Akizungumza hapo jana (26.09.2010) afisa huyo alisema wana kila sababu ya kushukuru kwamba mateka hao bado wangali hai na wamepelekwa katika eneo kame la milima la Timetrine, kaskazini mwa Mali karibu na mpaka na Algeria.

Kwa mujibu wa duru zilizo karibu na mazungumzo na wanamgambo, mateka hao wameonekana wakiwa hai. "Nimewaona mateka. Wote ni wazima na hata wanaweza kusimama, " amesema afisa mmoja wa Mali ambaye hakutaka jina lake litajwe. Afisa huyo aidha amesema busara ya kiwango cha juu inahitajika katika kuwaokoa mateka hao na kwamba wametoa taarifa hiyo ili kuzihakikishia familia za mateka hao wa rehani, lakini akataka wasiulizwe maswali bila kutoa maelezo zaidi.

Wengi wa mateka hao wanaifanyia kazi kampuni kubwa ya nishati ya nyuklia, Avera, inayomilikiwa na serikali ya Ufaransa au kampuni ya uhandisi ya Satom. Kampuni hizo zimewaondoa wafanyakazi wake wanaofanya shughuli za kuchimba madini ya uranium nchini Niger. Ufaransa imewaonya raia wake wasisafiri kwenda nchi za Afrika Magharibi na Afrika Kaskazini zilizoko katika eneo la Sahel, eneo kubwa la jangwa ambako katika miaka ya hivi karibuni kundi la al Qaeda limeongeza harakati zake.

Waziri mkuu wa Ufaransa, Francois Fillion, hapo kesho atakutana na viongozi wa vyama mbalimbali katika bunge la nchi hiyo kujadili vitisho vya usalama ndani na nje ya nchi.

Mkutano kuhusu ugaidi Sahel

Wakati huo huo, makamanda wakuu wa kijeshi na wataalamu wa kupambana na ugaidi kutoka nchi za eneo la Sahel walikutana jana (26.09.2010) kusini mwa Algeria katika juhudi za kutafuta njia za kukabiliana na kitisho cha wanamgambo wa al Qaeda kinachozidi kuongezeka. Mkutano huo uliofanyika katika mji wa jangwani wa Tamanrasset ulilenga kuratibu jitihada za kanda nzima ya Sahel za kupambana na ugaidi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mnadhimu wa jeshi la Algeria, Ahmed Gaid Sakah, alisema mkutano huo ulijikita zaidi katika masuala ya ugaidi na uhalifu wa kupangwa. Sakah alisema mkutano pia ulilenga kuweka malengo ya wazi katika mkakati wa kupambana na al Qaeda na kutoa fursa ya kubadilishana habari muhimu. Amezitaka nchi za eneo la Sahel ziheshimu ahadi zao na zichukue hatua dhidi ya ugaidi katika eneo hilo.

Akizungumza baada ya mkutano huo kumalizika, afisa mmoja wa Mali alisema makamanda wa jeshi wamekubaliana kufanya luteka za pamoja za kijeshi.

Mkutano huo wa mjini Tamanrasset, ulifanyika takriban wiki moja tangu Wafaransa watano na raia wengine wawili wa kigeni kutekwa nyara kaskazini mwa Niger, na uliwaleta pamoja wajumbe kutoka Algeria, Mali, Mauritania na Niger.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman