1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yataka Marekani iache udukuzi wa simu

22 Oktoba 2013

Ufaransa imeitaka rasmi Marekani iache kudukiza mazungumzo ya simu ya raia wa Ufaransa lakini wakati huo huo imeashiria kutaka kuutuliza mzozo juu ya suala hilo.

https://p.dw.com/p/1A401
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Laurent Fabius (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry (kulia).
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Laurent Fabius (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry (kulia).Picha: LIONEL BONAVENTURE/AFP/Getty Images

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne (22.10.2014) mjini Paris Ufaransa baada ya hapo jana Rais Barack Obama wa Marekani kumpigia simu Rais Francois Hollande katika juhudi za kutuliza mzozo huo kati ya nchi hizo mbili.

Katika mkutano wao wakati wa chai ya asubuhi na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry,waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesisitiza kupatiwa taarifa kamili kuhusu mpango tata wa upelelezi wa Marekani uliofichuliwa hivi karibuni kabisa.

Msemaji wa waziri huyo amekaririwa akisema baada ya mkutano huo kwamba Fabius amerudia tena madai yao ya kutaka kupatiwa maelezo kuhusu hatua za upelelezi ambazo hazikubaliki kati ya washirika na ambazo hazina budi kukomeshwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Laurent Fabius.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Laurent Fabius.Picha: picture-alliance/AP Photo

Licha ya kauli hiyo nzito ya wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa kuna dalili kwamba serikali ya Ufaransa inataka kuuzima mzozo huo uliosababishwa na kufichuliwa na gazeti la Le Monde kwamba Shirika la Usalama la Taifa la Marekani NSA limechunguza mawasiliano ya zaidi ya watu milioni 70 nchini Ufaransa kati ya Disemba 10 mwaka 2012 na Januari nane mwaka huu.

Alipoulizwa iwapo Ufaransa inafikiria hatua zozote za kulipiza kisasi dhidi ya Marekani kutokana na utendaji huo wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA msemaji wa serikali Najat Vallaud-Belkacem ameondowa uwezekano huo kwa kusema kwamba hafikiri kuna haja ya kuundeleza mzozo huo.

Obama azungumza na Hollande

Rais Barack Obama wa Marekani hapo jana jioni alimpigia simu Rais Francois Hollande wa Ufaransa katika juhudi za kutuliza uhusiano kati ya nchi hizo kufuatia kuibuka kwa taarifa hizo za upelelezi.

Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: picture alliance/Photoshot

Wakati wa mazungumzo hayo Rais Ollande amemwambia Rais mwenzake wa Marekani Obama kwamba vitendo hivyo vya NSA havikubaliki kufanyika kati ya marafiki na washirika.

Maafisa wa serikali ya Marekani wamekiri kwamba Wafaransa wana msingi halali kulalamika lakini wameelezea baadhi ya taarifa kuhusu mpango wa upelelezi wa NSA zilikuwa za kupotosha.

Awali Ufaransa ilimwita balozi wa Marekani nchini humo na kudai suala hilo lifikishwe katika mazungumzo ya biashara huru kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani.

Tathmini ya shughuli za ujasusi

Obama tayari ameanzisha tathmini ya kuangalia jinsi serikali ya Marekani inavyokusanya taarifa zake za ujasusi ili kushughulikia mashaka ya haki ya wananchi kuwa na faragha.

Nyaya za mawasiliano.
Nyaya za mawasiliano.Picha: Fotolia/kubais

Maafisa wa Marekani pia wamekuwa na shauku ya kusisitiza kwamba taarifa za ujasusi zinazopatika katika kuchunguza mazungumzo ya simu zinaweza kuwanufaisha washirika wote wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi.

Mipango ya upelelezi ya Marekani iliofichuliwa imebaini kwamba serikali ya nchi hiyo imekuwa ikifanya uchunguzi wa kiwango kikubwa dhidi ya serikali ya nchi za kigeni na raia wake kuanzia washindani wake China na Urusi hadi washirika wake kama vile Uingereza,Brazil,Mexico, Ujerumani na Ufaransa.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman