1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yawarejesha Waroma 75 nchini Romania.

20 Agosti 2010

Ufaransa imekosolewa na mashirika ya kutetea haki kwa ubaguzi wa rangi.

https://p.dw.com/p/OsGb
Waroma 371 wanatarajiwa kurejeshwa makwao kutoka Ufaransa ifikapo mwezi Septemba.Picha: AP

Zaidi ya watu 70 wa jamii ya kuhamahama wajulikanao kama Waroma wamewasili katika mji mkuu wa Romania, Bucharest baada ya Ufaransa kuanza mpango wake tete wa kuwarejesha makwao wahamiaji hao licha ya ukosoaji mkali ndani na nje ya Ufaransa.

Kulingana na duru za polisi wa mpakani nchini Romania, Ndege mbili kutoka miji ya Lyon na Paris, Ufaransa zilizowabeba Waroma 75 zilitua jana mjini Bucharest. Idadi hiyo ni ya juu zaidi ya Waroma waliofukuzwa kutoka Ufaransa tangu rais Sarkozy alipotoa amri kali dhidi ya Waroma wanaoishi nchini Ufaransa kinyume na sheria.

Jumla ya watu 371 wa jamii hiyo ya kuhamahama wanatarajiwa kurejeshwa nchini Romania kufikia katikati ya mwezi Septemba. Wengine 41 watarejeshwa nchini Bulgaria na tayari 13 kati yao waliwasili jana nchini humo.

Shrikika la habari la Mediafax lililoko nchini Romania, lilimnukulu mwakilishi wa chama cha Waroma nchini Romania akisema kwamba kurejeshwa huko kwa watu hao wa jamii ya wachache si kwa kawaida.

Mwanamke mmoja kati ya wale waliotoka mjini Lyon alisema nusu ya idadi ya Waroma waliofukuzwa kutoka Ufaransa walikuwa wakiomba pesa na wengine walikuwa wakifanya kazi ili kukidhi mahitaji yao. Alisema kwamba wengine waliotoka mjini Paris hawakuwa wakipata pesa zozote za msaada kutoka kwa serikali ya Ufaransa.

Maafisa wa serikali ya Ufaransa walisema Waroma hao walikuwa wakiondoka kwa hiari baada ya kila mtu mzima kulipwa Euro 300 na Euro 100 kwa kila mtoto.

Kwa sababu watu wa jamii hiyo ya wachache wa kutoka Romania na Bulgaria wanazingatiwa kama raia wa Umoja wa Ulaya, wanaweza kurejea wakati wowote lakini wanaweza kurejeshwa makwao ikiwa watahusika katika uhalifu ama kama watakuwa mzigo kwa jamii.

Baraza kuu la Ujerumani la Wasinti na Waroma lilitoa mwito kwa serikali ya Ufaransa iache kuwafukuza watu hao likisema kwamba wahamiaji hao wanarejeshwa katika mazingira magumu ya umaskini.

Alena - eine Roma aus Ostrovany
Waroma wengi huishi katika mazingira magumu ya umaskini.Picha: DW

Wanasiasa nchini Bulgaria wameitaja hatua hiyo kama jaribio butu la kusuluhisha tatizo la uwepo wa Waroma na wameonya kwamba suala la Waroma ni tatizo la Ulaya wala sio tu la Romania, Bulgaria au Ufaransa.

Rais wa Romania, Trian Basescu ametoa mwito wa ushirikiano na Ufaransa katika kushughulikia wahalifu wa jamii ya Waroma akitangaza kwamba maafisa zaidi wa polisi watatumwa nchini Ufaransa.

Alisema wanaelewa msimamo wa serikali ya Ufaransa na wakati huo huo, wanaunga mkono, bila pingamizi, haki ya kila raia wa Romania ya kwenda popote katika mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Wakati huo huo, waziri wa ndani wa Ufaransa, Brice Hortefeux amesema Jumuiya ya Ulaya inafaa kuongeza jitihada za kuwaunganisha Waroma na kwamba anangojea kuona Jumuiya hiyo ikionyesha uwezo wa kuwawezesha Waroma kupata elimu, ajira na makaazi.

Msemaji wa tume hiyo alisema jana kwamba kuna Euro bilioni 17.5 iliyolenga kutumiwa kati ya mwaka 2007 na 2013 ili kufadhili miradi ya kuwahusisha Waroma. Alikiri kwamba ni fedha nyingi. Uamuzi wa kuzibomoa kambi za Waroma nchini Ufaransa umekosolewa na mashirika na kutetea haki, vyama vya wafanyakazi na wanasiasa wa upinzani wakisema ni ubaguzi wa rangi. Wanasiasa nchini Ufaransa pia wameikashifu serikali kwa kulifanya suala la Waroma kama chanzo cha kukwepa na kubadilisha mada kutoka kwa kashfa zinazoendelea za kisiasa.

Mwandishi, Peter Moss /DPA

Mhariri, Josephat Charo