1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda inapanga kuanzisha Benki ya kibiashara ya kiislamu

Kalyango Siraj4 Julai 2008

Haitozi riba

https://p.dw.com/p/EWdl
Moja wa Benki za kiislamu Dubai, Umoja wa Falme za kiarabu.Benki kama hiyo karibu itafunguliwa nchini UgandaPicha: AP

Benki ya kibiashara ya kiislamu itafunguliwa nchini Uganda.

Hii ndio itakuwa mara ya kwanza kwa benki inayoendeshwa kwa msingi wa sheria za dini ya kiislamu ambazo miongoni mwa mengine haziruhusu riba.

Uganda itajiunga na mataifa mengine ya Afrika Mashariki kupata huduma za benki ya kibiashara ambayo inafuata kanuni za dini ya kiislamu.

Benki hiyo itaitwa katika lugha ya kigeni National Islamic Bank of Uganda NIBOG.

Taarifa za kufunguliwa kwa benki ya Uganda zilitolewa hivi karibuni na mwenyekiti wa benki ya kitaifa ya kibiashara na rais wa taasisi ya uwekezaji ya International Investiment House yenye makao yake makuu katika Umoja wa Falme za Kiarabu,Ahmed Dagher.

Amesema kuwa benki hiyo itaendesha biashara chini ya sheria za dini ya kiislamu ambazo hazikubali riba kwa mikopo ya benki.Aidha amesema kuwa mkazo utakuwa ulimbikizaji na wala sio viwango vya riba ambavyo kinyume na sheria za dini.

Dr Jamil Serwanga ni mhadhiri na mkuu wa kitengo sanaa na elimu ya jamii katika chuo kikuu cha kiislamu nchini Uganda.Akiwa alibobea elimu ya uchumi wa kiislamu anasema benki ya kibiashara kama hiyo ya kiislamu inaweza kufanya biashara bila ya kutegemea riba.

Mbali na benki ya kibiashara kutunza pesa za mteja kwa sababu yoyote ile lakini kuna huduma nyingine ambayo inatolewa na benki ambayo ni kutoa mkopo.Na kawaida mkopo wa benki huwa na masharti ya kuulipa.Miongoni mwa hayo ni kulipa riba fulani ya kiwango cha pesa ulizokopeshwa, na hiyo ni mojawapo wa njia bemnki zinapopata fedha.

Hata hivyo haijulikani benki hiyo itaafunguliwa lini,ila afisa wa ahabari wa benki kuu ya taifa nchini Uganda,Juma Walusimbi amesema kuwa National Islamic Commercial Bank iliwasilisha maombi yake kwa Benki kuu ya taifa ikitaka kufungua tawi lao nchini humo.

Tawi la Uganda likifunguliwa pamoja na matawi mengine mjini Khartoum nchini Sudan hii ndio itakuwa benki ya kwanza ya kiislamu nchini Uganda, mbali na kuwa kuna benki zaidi ya tano za kibiashara nchini humo.

Tangazo la kuanzishwa kwa benki ya kiislamu nchini Uganda limekuja wakati benki za kiislamu zikipanua biashara zake barani Afrika.Mwaka jana benki ya Gulf Afrika Bank ilifungua tawi lake nchini Kenya.

Hayo yanatokana na mkutano wa hivi majuzi wa mawaziri wa nje wa mataifa ya jumuia ya kiislamu ya OIC uliofanyika mjini Kampala. Na Uganda ni mwanachama.