1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda kuitisha tena mazungumzo ya Burundi

19 Desemba 2015

Uganda imesema itaitisha tena mazungumzo ya upatanishi ya Burundi, kufuatia machafuko yaliyoipeleka nchi hiyo ndogo kwenye kingo za vita na kuulazimu Umoja wa Afrika kujitayarisha kutuma kikosi cha kuwalinda raia.

https://p.dw.com/p/1HQU3
Burundi Armee findet Waffen in der Hauptstadt Bujumbura
Picha: Reuters/J. P. Aime Harerimana

Serikali ya Burundi na pia kundi kubwa zaidi la upinzani wamekaribisha hatua ya kuanzisha tena mazungumzo hayo. Siku ya Ijumaa, (18.12.2015) Umoja wa Afrika ulisema unajiandaa kutuma kikosi cha wanajeshi 5,000 nchini Burundi kuwalinda raia, ukitumia nguvu kwa mara ya kwanza kutuma wanajeshi katika nchi mwanachama dhidi ya matakwa ya nchi hiyo.

Hali ya wasiwasi umekuwa ikiongezeka nchini Burundi hasa tangu watu wenye silaha walipovamia kambi za kijeshi katika mji mkuu Bujumbura wiki iliyopita, na kuzusha hofu katika kanda hiyo ambako kumbukumbu za mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda zingalipo.

Burundi ilitumbukia katika mgogoro mwezi Aprili baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza mipango ya kuwania muhula wa tatu madarakani. Umoja wa Mataifa unasema watu wasiopungua 400 wameuawa tangu mwezi Aprili, wakati uamuzi huo wa Nkurunziza ulipozusha maandamano na baadae jaribio la mapinduzi lililoshindwa.

Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al-Hussain amekuwa akionya juu ya hatari inayoikabili Burundi.
Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al-Hussain amekuwa akionya juu ya hatari inayoikabili Burundi.Picha: picture-alliance/dpa/M. Trezzini

Serikali yasema iko tayari

Waziri wa ulinzi wa Uganda Chrispus Kiyonga, aliuambia mkutano wa wandishi wa habari mjini Kampala siku ya Jumamosi, kwamba hali ya usalama nchini Burundi imekuwa ikidorora kila kukicha. "Tunadhani sasa ni wakati muafaka na muhimu kuanzisha tena majadiliano," alisema Kiyonga.

Kiyonga alisema karibu makundi 14 yanayowakilisha matabaka mbalimbali ya jamii ya Burundi, kikiwemo chama tawala, vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia yatahudhuria mazungumzo hayo.

Msemaji wa serikali ya Burundi Philippe Nzobonariba alisema serikali imekuwa tayari wakati wote kufanya mazungumzo na ilikuwa inasubiri mwaliko. "Ni mazungumzo ya Warundi na ni Warundi tu watakaoamua nini cha kujadiliana," aliliambia shirika la habari la Reuters.

Nzobonariba hata hivyo aliondoa uwezekano wa kuzungumza na yeyote ambaye serikali inamchukulia kuwa mhusika katika jaribio la mapinduzi lililofeli. "Linaweza kuwa tukio la kutuwezesha kuwakamata kwa sababu wanatafutwa na vyombo vya sheria vya Burundi," alisema.

Mazungumzo kuanza Desemba 28

Pancrace Cimpaye, msemaji wa muungano mkubwa zaidi wa upinzani nchini Burundi unaojulikana kama CNARED, alikaribisha hatua ya Uganda kuitisha upya mazungumzo ya amani, inagwa alisema mungano wake ulikuwa bado haujapatiwa mwaliko.

"Kwetu mazungumzo ni kati ya pande mbili kwenye mgogoro, na pande hizo mbili zinazozozana ni Nkurunziza na serikali yake kwa upande mmoja, na CNARED kwa upande mwingine," aliliambia shirika la Reuters.

Vurugu za karibuni mjini Bujumbura zilisababisha vifo vya watu Karibu 90.
Vurugu za karibuni mjini Bujumbura zilisababisha vifo vya watu Karibu 90.Picha: Reuters/J.P. Aime Harerimana

Mazungumzo hayo yataanza tena nchini Uganda Desemba 28, na baadae yatahamishiwa mjini Arusha nchini Tanzania, yaliko makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo Burundi ni mwanachama wake.

Mwezi Julai jumuiya ya Afrika Mashariki ilimeteua Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni kuwa mpatanishi wa mgogoro huo na mikutano ya awali ilifanyika katika mji mkuu wa Burundi katika mwezi huo.

Hali yazidi kuwa mbaya

Katika mapigano mabaya zaidi tangu jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwezi Mei, waasi walizishambulia kambi za kijeshi katika mji mkuu wa Burundi; Bujumbura wiki iliyopita, ambapo karibu watu 90 waliuawa.

Mashirika ya kuteteta haki za binaadamu yameripoti kuwepo na makabiliano mabaya kati ya waandamanaji na vikosi vya serikali, mashambulizi ya silaha na kuwekwa vizuwizini wakosoaji wa serikali. Lakini serikali imepuuza ripoti za ukiukaji wa haki za binaadamu.

Mamia ya maelfu ya Warundi wameikimbia nchi hiyo kunusuru maisha yao tangu ulipoibuka mgogoro huo mbaya zaidi kuikumba Burundi tangu ilipotoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa na mwelekeo wa kikabila mwaka 2005.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.

Mhariri. Caro Robi