1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda kumulikwa kuhusu ukiukaji wa haki

3 Novemba 2016

Leo Novemba 3 baraza la haki za binadamu la umoja wa mataifa linaanza mchakato wa kuchunguza taarifa za haki za binadamu nchini Uganda, katika mchakato unaojulikana kama Universal Periodic Review, UPR.

https://p.dw.com/p/2S55I
Uganda Wahlen Proteste der Opposition
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Katika mapitio yake yaliyopita ya mwaka 2011Uganda ilikubali kuchukua uwanda mpana wa mapendekezo ya tume hiyo, ikijumuisha kuhakikisha inaheshimu uhuru wa ushirika na mikusanyiko ya amani, kuchunguza matumizi ya nguvu zilizopitiliza pamoja na mateso kutoka kwa maafisa wa usalama na kuahidi kuchukua hatua ikiwemo kuwafungulia mashitaka wahusika wote.

Katika mawasilisho yake ya mwaka huu, Serikali imetangaza kuwa imepiga hatua kubwa katika kukuza uelewa wa kuheshimu haki za binadamu, huku ikiorodhesha madawati ya kutetea haki za binadamu, tume pamoja na tume ndogo ambazo zimeanzishwa katika ofisi mbalimbali za serikali, pamoja na kuwa kwa kiasi kikubwa ofisi hizo zimekuwa kimya kuzungumzia masuala ya ukiukwaji wa haki ya kujieleza, kukusanyika na kujumuika.

Ghasia na unyanyasaji wa wazi uliofanywa na polisi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa mwezi Februali mwaka 2016, ulidhihirisha kuwa unyanyasaji haukuzuiwa na ongezeko la madawati na tume ambazo zinashughulikia masuala ya haki ya binadamu nchini humo.

Vyombo vya habari vilipiga picha polisi wakiwapiga waandishi wa habari pamoja na kutupa mabomu ya kutoa machozi kwa watu ambao walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya kuwasikiliza wagombea wa upinzani, baadhi ya waandishi wa habari walikamatwa na polisi kutoka katika studio wakirusha matangazo ya moja kwa moja ya matukio ya wagombea wa upinzani.

Hakuna hatua zilizochukuliwa tangu tathmini ya mwisho

Kando na hayo Serikali pia ilifunga upatikanaji wa mitandao ya kijamii kwa siku tano katika kuendelea kuzuia kukosolewa kwa mchakato wa uchaguzi, mchakato ambao wachunguzi wa ndani wanasema haukuwa huru na wa haki.

Uganda haikuchukua hatua yoyote halisi ya kuwachukulia hatua maafisa wa jeshi na polisi kwa kutumia nguvu iliyopitiliza katika kutawanya mikusanyiko, mpaka sasa hakuna mtu yeyote ambaye amepatikana na hatia ya mauaji ya  waandamanaji na watu ambao hawakuwa sehemu ya waandamanaji  yaliyofanyika Septemba 2009 na April 2011, na hakuna ushahidi kuonyesha kuwa polisi imehoji hata shuhuda mmoja wa mauaji hayo tangu tathmini ya mwisho ya tume hiyo kufanyika.

Uganda Protest der Opposition
Polisi ikitawanya waandamanaji kwa kurusha mabomu ya kutoa machoziPicha: Reuters/J. Akena

Ripoti ya Serikali kwa UPR inadai kuwa vitendo vya polisi na vile vya tume ya haki za binadamu ya Uganda vinafuatilia unyanyasaji huo lakini kuna ushahidi kidogo sana, maafisa wa ngazi za chini ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu na matokeo yake hayaonekani na kwa kiasi kidogo sana yanazuia kuendelea kwa vitendo vya unyanyasaji kwa sababu maafisa wakuu wa polisi hawajawahi kuchunguzwa kutokana na amri ambazo walitoa.

Serikali imekuwa ikipuuzia tume ya haki za binadamu nchini Uganda, katika visa viwili ambapo tume iliitaka serikali kulipa fidia kwa familia ambayo watoto wao waliuwawa na majeshi ya usalama katika maandamano, lakini pesa hizo mpaka sasa hazijatolewa.

Katika mchakato wa UPR, Uganda inaweza kujisifu kwa kutaja makosa ya uhalifu ya mwaka 2012, lakini hakuna afisa hata mmoja si wa polisi au jeshi ambao wameshitakiwa kwa mujibu wa sheria.

Mwandishi: Celina Mwakabwale

Mhariri:Iddi Ssessanga