1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa mataifa waishutumu UPDF

12 Oktoba 2015

Wanajeshi wa serikali ya Uganda walioko nchini Sudan Kusini kwa ajili ya kusaidiana na majeshi ya serikali nchini humo wanatarajia kurejea nchini Uganda ifikapo mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/1Gmxj
Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.Picha: Samir Bol/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa mmoja wa maafisa wa juu wa jeshi la Uganda Jenerali Katumba Wamala wanajeshi hao wanatarajia kuondoka Sudani kusini katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba mwaka huu.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni alipeleka wanajeshi nchini Sudan kusini kwa lengo la kusaidiana na serikali ya Rais Salva Kiir katika mapambano dhidi ya waasi wanao ongozwa na aliyekuwa makamu wa Rais wa serikali ya nchi hiyo Riek Machar.

Wanajeshi hao wa Uganda wamefanya kazi kubwa ya kusaidiana na vikosi vya serikali nchini humo katika kuudhibiti mji mkuu wa Juba nchini humo.

Mwaka jana umoja wa mataifa ulililishutumu jeshi la Uganda ( UPDF ) kwa kutumia silaha zilizopigwa marufuku nchini Sudan kusini madai ambayo Uganda imeyakanusha.

Kulingana na mkataba wa kuleta amani nchini humo uliosainiwa na Kiir na Machar mwezi Augusti mwaka huu mjini Adis Ababa, wanajeshi hao wa Uganda walipaswa kuondoka nchini Sudan kusini mwishoni mwa wiki lakini tayari inainyesha haitowezekana tena kufanya hivyo.

Hatua ya kuondolewa kwa majeshi ya serikali yanayoudhibiti mji mkuu wa Juba ili kuruhusu kurejea kwa Rick Machar ni moja ya makubaliano yaliyomo katika mkataba huo.

Baada ya kuondoka kwa wanajeshi hao wa Uganda nchini humo nafasi yao itazibwa na jeshi ambalo halifungamani na upande wowote wakati wanajeshi wa Sudani kusini watapelekwa katika makambi mengine yaliyoko nje ya mji mkuu wa nchi hiyo.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri :Hamidou Oummilkheir