1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yatishia kuyaondoa majeshi yake Somalia

3 Novemba 2012

Uganda imetishia kuyaondoa majeshi yake katika operesheni za kulinda amani Somalia na maeneo mengine yenye vita, baada ya Umoja wa Mataifa kuituhumu kuwasaidia waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/16cCW
Wanajeshi wa Uganda walioko Somalia
Wanajeshi wa Uganda walioko SomaliaPicha: AP

Matamshi hayo yametolewa jana na Waziri wa Usalama wa Uganda, Wilson Mukasa ambaye pia ameongeza kuwa Uganda itauelezea msimamo wake kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York. Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa ujumbe wa Uganda ambao uliongozwa na Ruhakana Rugunda, mjumbe maalum na waziri wa habari na teknolojia ya mawasiliano, haukutishia kuondoa majeshi yake kutoka kwenye kikosi cha kulinda amani wakati wa mazungumzo na maafisa wa umoja huo mjini New York wiki hii.

Ujumbe huo wa Uganda ambao ulikutana na Balozi wa India, Hardeep Singh Puri, rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu, pia haukuzungumzia kitisho cha kuondoa wanajeshi wake Somalia. Uganda ina wanajeshi 17,600 katika kikosi cha Umoja wa Afrika cha kulinda amani nchini Somalia-AMISOM, ambao wanapambana na kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na Al-Qaeda. Majeshi ya Uganda yanayosaidiwa na vikosi maalum vya Marekani pia yanaongoza operesheni za kumuwinda kiongozi wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army-LRA nchini humo, Joseph Kony ambaye yuko mafichoni katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kiongozi wa LRA, Joseph Kony
Kiongozi wa LRA, Joseph KonyPicha: AP

Katika taarifa iliyovuja kwa vyombo vya habari mwezi uliopita, kundi la wataalamu la Umoja wa Mataifa lilizituhumu Uganda na Rwanda kuliunga mkono kundi la waasi wa M-23, linaloongozwa na Bosco Ntaganda, mbabe wa vita anayetafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC. Hata hivyo, nchi hizo mbili zimekanusha vikali tuhuma hizo. Taarifa ya India ilieleza kuwa ujumbe huo ulionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti hiyo ya wataalamu na kuongeza kuwa maoni ya wataalamu binafsi sio lazima yalingane na ya Umoja wa Mataifa. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Uganda imekuwa mchangiaji muhimu sana katika kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Somalia na kwengineko.

Mukasa amesema Uganda itayaondoa majeshi yake Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ili kuzingatia zaidi usalama wake wa ndani. Anasema wamechoka kupakaziwa uongo hata baada ya kujitolea kuhakikisha marafiki na majirani zao wako salama na badala yake asante wanayoipata ni kuambiwa wanasaidia waasi. Msemaji wa jeshi la Uganda, Felix Kulayigye amesema jeshi bado halijapokea amri yoyote, lakini liko tayari kufanya hivyo iwapo litaamriwa kutekeleza suala hilo.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
Rais wa Uganda, Yoweri MuseveniPicha: AP

Akizungumza na Reuters, msemaji wa operesheni za kijeshi wa Al-Shabaab, Sheikh Abdiasis Abu Musab amesema walikuwa hawajui nia ya Uganda kuyaondoa majeshi yake na kwamba itaendelea kupigana na wanajeshi wa kulinda amani wa Afrika. Musab ameongeza kusema kuwa baada ya Uganda kuondoka Somalia, itakuwa rahisi kwao kupigana na wavamizi waliobakia.

Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wamesema haijafahamika wazi iwapo vitisho vya Uganda ni vya kweli au inajaribu tu kuwashinikiza wanajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutochukua hatua kutokana na ripoti ya wataalamu wa umoja huo. Waatalamu hao wameutaka Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo dhidi ya watu binafsi wanaowasaidia waasi wa M-23. Mchambuzi mmoja wa Somalia anayeishi London, Uingereza, Hamza Mohamed amesema kuwa Uganda inaendesha mchezo wa sanaa za kisiasa na kwamba haiwezi kuwaondoa wanajeshi wake Somalia. Mohamed anasema kuwa suala hilo litatatuliwa katika mikutano ya siri na pengine kutoweka tena hadharani taarifa za siri.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki MoonPicha: AP

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE

Mhariri: Daniel Gakuba