1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yawakamata wapiganaji wa M23

Bruce Amani
24 Februari 2017

Uganda inawazuilia wapiganaji kadhaa kutoka kundi la waasi wa M23 waliokimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kukabiliana na wanajeshi wiki hii.

https://p.dw.com/p/2YCIi
Uganda Afrika Soldaten Sicherung Demonstration
Picha: picture-alliance/dpa/D.Kurokawa

Msemaji wa jeshi la Uganda, Richard Karemire, alisema wapiganaji 44 wa M23 wanazuiliwa katika kambi moja ya kusini magharibi mwa mji wa Kisoro.

Hata hivyo, Karemire alikanusha tuhuma zilizotolewa na serikali ya Kongo kuwa Uganda inawawezesha wapiganaji hao ili kuanzisha upya uasi wao.

Mapigano ya karibuni kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 yalianza Jumatatu hadi Jumatano katika eneo la Rutshuru, mkoa wa Kivu ya Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, karibu na Bunagana, mji ulioko kwenye mpaka na Uganda.

M23 ndilo kundi kubwa zaidi kati ya makundi mengine ya waasi ambayo kwa miaka mingi yamesababisha machafuko na umwagaji damu katika eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri wa madini.

Kundi hili liliwahi kudhibiti sehemu kubwa ya mkoa huo kabla ya kushindwa na muungano wa majeshi ya kikanda, serikali na ya Umoja wa Mataifa miaka michache iliyopita.