1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugavi wa maji mashakani mjini Grahamstown Afrika Kusini

Josephat Charo24 Februari 2008

Idara ya maji yakabiliwa na upungufu wa wataalam

https://p.dw.com/p/DCQT
Wahandisi wenye ujuzi wa kikazi wanahitajika kuhakikisha ugavi bora wa maji safiPicha: AP

Hali tete ya ugavi wa maji katika mji wa Grahamstown kusini mashariki mwa Afrika Kusini, ulijitokeza tena mwezi huu wakati mifereji ilipokauka kwa karibu siku mbili katika sehemu kubwa ya mji huo.

Mfumo wa ugavi wa maji katika mji wa Grahamstown umewavunja moyo wakaazi wa mji huo katika miezi 14 iliyopita katika swala la ubora wa maji na ugavi kuweza kutegemewa.

Huku mfumo wa ugavi wa maji katika mji wa Grahamstown ukiwa katika hali ya kukata tamaa, tukio la hivi majuzi halihusiani na ukosefu wa matengenezo ila kosa la binadamu.

Kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu ya manuspaa ya mji huo ambaye hakutaja jina lake litajwe, mfanyakazi mmoja wa mji huo hakufungua vali ya bomba la kuhifadhia maji la Waainek linaloihudumia sehemu kubwa ya mji wa Grahamstown.

Ukosefu huu wa umakini kazini unaonyesha vipi ukosefu wa wafanyakazi walio na ujuzi wa kikazi unaathiri ugavi wa maji mjini Grahamstown na kwa nchi nzima kwa jumla.

Afisa wa utafiti katika taasisi ya utafiti wa maji mjini Grahamstown, IWR, Lil Haigh, amesema hakuna juhudi nyingi zinazofanywa kuwaandika kazi wahandisi waliofuzu katika manuspaa ya mji huo. Amesema mji wa Grahamstown una jukumu la kuwaeleza vijana ni nafasi ngapi za ajira zilizopo katika sayansi na uhandisi.

Matatizo ya maji yaligonga vichwa vya habari mwezi Novemba mwaka wa 2006 wakati Martin Davies, mwanasayansi wa ngazi ya juu anayehusika na maswala ya kuendeleza kilimo cha miti na ufugaji wa samaki katika chuo kikuu cha Rhodes mjini Grahamstown, alipoonya juu ya sumu katika mfumo wa ugavi wa maji mjini humo. Davies anasimamia matangi makubwa ya maji yenye samaki 150,000 katika shamba la samaki la chuo kikuu cha Rhodes.

Davies aliwajulisha viongozi wa chuo kikuu hicho wakati samaki wake wadogo 35,000 walipokufa ghafla. Alisema jinsi samaki wake walivyokuwa wakiogelea kwa kufanya mizunguko na hatimaye kugeuka matumbo juu migongo chini, ilikuwa ishara ya wazi kwamba walikuwa wanakufa kutokana na sumu ya madini ya aluminiumu.

Mara moja wanafunzi wakaonywa wasiyanywe maji hayo ya chuo kikuu wala wasiyatumie kupikia huku chuo kikuu kikiagiza chupa za maji kutoka Port Elizabeth, kilomita 135 magharibi mwa nchi. Maduka makubwa yaliuza maji mengi ya chupa na vichungi vya maji viliuzwa kwa wingi.

Chuo kikuu cha Rhodes pia kiliandaa mfulululizo wa chunguzi za ubora wa maji zilizolenga kutafuta shina la tatizo hilo. Chunguzi hizi zilisimamiwa na Nikite Muller, naibu mkurugenzi wa taasisi ya IWR ambaye baada ya siku chache alitangaza kwamba maji hayo yalikuwa salama kunywa.

Meya wa mji wa Grahamstown, Phumelelo Kate, alionyesha hadharani imani yake juu ya uchunguzi wa ubora wa maji kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo alikunywa gilasi moja ya maji ya bomba yaliyokuwa na rangi ya hudhurungi.

Wakati ugavi wa maji ulipoanzishwa tena baada ya kusitishwa kwa muda mapema mwezi huu, kwa mara nyingine tena maji hayo yalikuwa na matope. Maduka makubwa yaliagiza tena maji ya chupa.

Lakini Davies anaamini mfumo wa maji wa mji wa Grahamstown una viwango hatari vya madini ya aluminiumu, akidai kwamba taasisi ya IWR haikugundua tatizo hilo wakati wa uchunguzi wake kwa sababu haikuyapima maji hayo. Yeye hunywa maji ya chupa au maji ambayo yamepitia mfumo wa kisasa wa kuchuja maji ulioujengwa nyumbani kwake.

Davies ameliambia shirika la habari la IPS kwamba mahabara huru katika mji wa Port Elizabeth na idara ya kitaifa inayohusika na maswala ya maji na misitu zimeliunga mkono dai lake kwamba kuna viwango hatari vya madini ya aluminiumu katika mfumo wa ugavi wa maji mjini Grahamstown.

Davies anasema udongo kwenye mchanga unaouzunguka mji wa Grahamstown una kiwango kikubwa cha madini ya aluminiumu ambayo huenda yameingia kwenye maji. Kiwango hicho kinasemekana ni kikubwa mno kiasi kwamba kampuni moja ya China ilitaka kwenda mjini humo kuyachimba madini hayo.

Davies pia anasema dawa inayotumiwa na manuspaa ya mji kuua mwani na kuyafanya maji kuwa safi ina madini ya aluminiumu. Mfumo huu hufaulu unapotumiwa vizuri lakini wafanyakazi wasio na ujuzi wa kikazi wanapotia viwango visivyo sawa katika maji au kama vifaa visivyofanyiwa matengenezo mazuri vinaruhusu madini haya kujikusanya, na kuweza kufikia kiwango hatari cha madini hayo katika maji.

Viwango vidogo vya madini ya aluminium katika mwili wa binadamu sio hatari kwa sababu hutoka mwilini pamoja na uchafu mwingine. Hata hivyo viwango vikubwa vya madini haya mwilini vimehusishwa na ugonjwa wa Alzheimer na aina nyingine za kichaa katika sehemu kadhaa duniani, lakini uhusiano kamili bado haujabainika wazi