1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ughali wa maisha umepanda Ujerumani

Miraji Othman18 Aprili 2008

Ughali wa maisha na mripuko wa bei za bidhaa hapa Ujerumani unaonesha unaanza kutia mizizi.

https://p.dw.com/p/DkTt
Axel Weber, Rais wa Benki Kuu ya UjerumaniPicha: AP

Ughali wa maisha katika nchi hii ilio na uchumi mkubwa kabisa barani Ulaya sasa umefikia asilimia 4.2. Kupanda huku kwa bei za jumla za bidhaa kunaashiria kwamba viwango vya riba za mikopo katika eneo la Ulaya linalotumia sarafu ya Euro vitabakia kama vilivyo katika mwaka huu wote wa sasa. Zaidi kuhusu hali hii, huyu hapa Othman Miraji...

Bei za bidhaa zinapotoka viwandani zimeongezeka sana katika mwezi uliopita wa Machi ukilinganisha tangu Disemba mwaka jana, pale nyongeza zililikuwa asilimia 4.4. Wachunguzi walioulizwa na gazeti la Financial Times walitarajia kwamba nyongeza ya bei za bidhaa zitakuwa chini kidogo, labda kwa asilimia 4.0, kima ambacho, hata hivyo, ni kikubwa zaidi kuliko kiwango cha mwezi wa Februari.

Jana , gavana mkuu wa Benki Kuu ya Ujerumani, Axel Weber, ambaye pia ni gavana katika Benki Kuu ya Ulaya, alionya kwamba kuengezeka bei za vyakula na nishati yaonesha kumezidi kuliko vile ilivokisiwa na Benki Kuu ya Ulaya kwa mwezi wa Machi. Katika hotuba alioitoa, Bwana Weber alisema katika mwezi wa Juni watayadurusu upya makisio yao, kwani vitu viwili viko wazi tangu kufanywa makadirio mnamo mwezi wa Machi. Kwanza, ni kwamba ongezeko la bei za vyakula na nishati linaonesha limetia mizizi zaidi kuliko vile ilivotarajiwa hapo kabla.

Pia bei za jumla za bidhaa hapa Ujerumani, ambazo pia zimepanda kwa asilimia 0.7 mwezi wa Machi ukilinganisha na mwezi wa Februari uliotangulia, zinatoa mfano wa hatari ya mfumko wa bei kutia mizizi. Mwanauchumi mwandamizi wa benki ya Amerika hapa Ujerumani, Holger Schmeiding, alisema jambo hilo linaonesha mbinyo ulioko ambao unasababisha ughali wa maisha kupanda katika eneo lote la nchi 15 zinazotumia sarafu ya Euro, ambako bei za bidhaa zilifikia kiwango kikubwa kabisa cha asilimia 3.6 mwezi wa Machi. Magavana wa Benki Kuu ya Ulaya wamebakisha viwango vya riba za mikopo kuwa asilimia 4.0 tangu mwezi Juni mwaka jana, wakihofia juu ya kupanda ughali wa maisha kwa wakaazi milioni 320 katika eneo hilo la Euro.

Nishati na vyakula bado ni bidhaa zilizobakia zinasababisha ughali wa maisha kupanda, huku bei za mafuta zikipanda kwa asilimia 20 mnamo mwaka uliopita, na mafuta ya kutia ujoto majumbani yakipanda bei kwa asilimi 60. Bei ya umeme impenda kwa asilimia 12.4. Na ukienda madukani kununua vyakula, utalipa sasa asilimia 26.9 zaidi kuliko mwaka uliopita, nakusudia ukinunua mchele na nafaka zilizosagwa; asilimia 42.7 zaidi kwa mafuta ya kupikia na asilimia 23 zaidi kwa bidhaa zinazotokana na maziwa.

Lakini Benki Kuu ya Ulaya imesema ughali wa bidhaa utabakia ukiengezeka kwa asilimia 2.0 kwa miezi ijayo. Lengo la benki hiyo ni kwamba ughali wa maisha ubakie chini ya asilimia 2.0.

Wanauchumi wanasema ughali huo wa bidhaa utabebwa na wateja.

Jana, taasisi sita za utafiti wa kiuchumi hapa Ujerumani zilikisia kwamba ughali wa maisha hapa Ujerumani kwa mwaka huu utafikia asilimia 2.6 kabla ya kutulia na kuwa asilimia 1.8 mwakani.

Lakini kuna habari nzuri, kwa upande mwengine. Ilitangazwa jana kwamba kwa mara ya kwanza tangu mwanzo wa miaka ya tisini, huenda ukosefu wa nafasi za kazi mwakani ukashuka chini kidogo, na kwamba chini ya ya watu milioni tatu watakuwa hawana kazi . Pia ilitajwa kwamba uchumi mwaka huu utapanda kwa asilimia 1.8 na mwakani kwa asilimia 1.4.

Wanauchumi wanashikilia kwamba licha ya misukosuko ya sasa katika taasisi za kifedha za kimataifa, bei ya juu ya nishati na vyakula, uchumi wa Ujerumani bado ni imara na utaweza kuhimili musukosuko hiyo; pia wateja hapa nchini hawatasita kuwacha mifuko yao wazi na kutumia zaidi. Lakini bado mategemeo ya uchumi wa Ujerumani yatakuwa zaidi katika kuuza bidhaa zake katika nchi za nje.