1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki, Eurogroup washindwa kuafikiana

12 Februari 2015

Mazungumzo kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake katika kanda inayotumia sarafu ya Euro yalimalizika Alhamisi, bila muafaka juu ya mpango wa uokozi usiyopendwa na Wagiriki wengi, na watajaribu tena siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/1EZtz
Griechenland PK Jeroen Dijsselbloem & Gianis Varoufakis 30.01.2015
Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Katika masaa saba ya mazungumzo ya dharura mjini Brussels, ambayo yaliisha baada ya saa sita za usiku, mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya Euro walishindwa hata kukubaliana juu ya tamko la pamoja kuhusu hatua zinazofuata.

Serikali mpya ya Ugiriki inayoongozwa na chama cha siasa kali za mrengo kushoto, Syriza, inataka mabadiliko katika mpango wa uokozi ambao inaulaumu kwa sehemu kubwa ya matatizo ya kiuchumi ya taifa hilo. Uchumi wa Ugiriki umenywea kwa karibu asilimua 25 katika mika michache iliyopita, na viwango vya umaskini vimepanda.

Mwenyekiti wa Eurogroup Jeroen Dijsselbloem na waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis.
Mwenyekiti wa Eurogroup Jeroen Dijsselbloem na waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis.Picha: REUTERS/Y. Herman

Matumaini ya kufikia makubaliano

Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis alieleza matumaini ya kupatikana kwa muafaka, watakapokutana tena siku ya Jumatatu.

"Kwa kuweza kuweka njia nzuri za mawasiliano na kusonga mbele, tunaelewana vizuri zaidi sasa kuliko tulivyokuwa awali, kwa hivyo nadhani hii ni hatua kubwa kwa sababu, unajua baada ya kuelewa yanafuata makubaliano," alisema Voraufakis baada ya mkutano huo.

Lakini Jeroen Dijsselbloem, mkuu wa kundi la mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya Euro - Eurogroup - alionekana kutokuwa na matumaini makubwa sana wakati akitoa tathmini yake ya mazungumzo hayo. "Tulijadili uwezekano wa kuurefusha mpango wa sasa, kwa baadhi ilikuwa wazi kwamba hii ndiyo njia inayopendelewa, lakini hatujafikia uamuzi huo bado," alisema.

"Taasisi za ukopeshaji zimeweka wazi kwamba ziko tayari kufanyakazi na serikali ya Ugiriki, lakini inahitaji maamuzi ya kisiasa kwanza kwa taasisi hizo kuanza kazi hiyo. Kwa hivyo tutahitaji muda zaidi kwa hilo," aliongeza kusema Dijsselbloem, ambaye ni waziri wa fedha wa Uholanz.

Tsipras akomaa dhidi ya mpango wa sasa

Wanadiplomasia walisema juhudi za kufikia tamko la pamoja ziligonga mwamba baada ya Varoufakis kushauriana na wenzake katika serikali. Baadhi ya maandishi katika tamko lililokataliwa na Ugiriki yalionyesha kuwa Eurogroup ilitaka kukubaliana juu kurefusha mpango wa sasa wa mkopo - jambo ambalo serikali mjini Athens haitaki kuliskia kabisaa.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras amekomalia msimamo wake. Anajua wale waliomchagua mwezi uliyopita wanasisitiza kukomeshwa kwa mpango huo wa uokozi ambao Wagiriki wengi wanaulamu kwa kuchochea hali ya umaskini inayowakabili.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeble, akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussles baada ya mazungumzo.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeble, akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussles baada ya mazungumzo.Picha: DW/B. Riegert

Tsipras, ambaye atakutana na viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kilele baadae leo, anakataa hatua zozote za kuurefusha mpango wa mkopo wa euro bilioni 240, ambao unaisha muda wake Februari 28. Anakataa kushirikiana na wawakilishi wa taasisi tatu zilizoikopesha nchi yake - yaani Umoja wa Ulaya, benki kuu ya Ulaya ECB na shirika la fedha duniani IMF, na anataka kusamehewa sehemu ya deni.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble, amesema ikiwa Ugiriki haiko tayari kuomba kurefushiwa mpango wake wa sasa wa uokozi, basi itakuwa ndiyo mwisho, akionekana kuondoa uwezekano wa msaada zaidi au kusamehewa deni.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,ape,dpae,afpe

Mhariri: Elizabeth Shoo