1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki kuomba kitita cha kwanza cha msaada wa fedha

11 Mei 2010

Serikali ya Ujerumani yaidhinisha mchango wake

https://p.dw.com/p/NLAM
Kanzela Merkel na waziri wake wa nje Guido Westerwelle.Picha: AP

Wakati Baraza la mawaziri la Ujerumani, leo limeidhinisha sehemu yake ya mchango wa Mfuko wa dala bilioni 750 utakotumika kutoa dhamana kuziokoa nchi za sarafu ya Euro zitazakumbwa na msukosuko, serikali ya Ugiriki, inatoa leo ombi lake la kukabidhiwa kitita cha kwanza kutoka mfuko huo .Masoko ya fedha barani Asia na Ulaya, yameanguka hii leo na sarafu ya Euro pia imeshuka thamani kutoka kipimo chake cha jana .Hii inatokana na wasi wasi uliopo kuwa licha ya kuinua-mgongo hicho,Ugiriki na nchi nyengine zilizongwa na madeni , hazitaweza kutekeleza hatua zilizopitisha za kubana matumizi.

Serikali ya Ugiriki, itauomba leo Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), kiinua-mgongo cha kwanza cha kiasi cha Euro Bilioni 20 sawa n a Dala bilioni 26 kutoka kima ilichoahidiwa cha bilioni 110 kuisaidia kulipa madeni yake mwezi huu.Hii ni kwa muujibu wa wizara ya fedha mjini Athens,Ugiriki ilivyoarifu.

Ombi hilo limetolewa siku 1 tu baada ya serikali ya Ugiriki ilipoamrisha mageuzi makubwa katika mfumo wa pensheni wa nchi hiyo ambao imeonya kwamba, unakaribia kuporomoka kabisa. Hatahivyo, vyama vya wafanyikazi vimeapa kwamba vitaupinga mpango huo wa serikali ambao utateremsha malipo ya uzeeni kwa wastani kwa kima cha 7% hadi ifikapo 2030.

Baraza la mawaziri la Ujerumani, limeidhinisha kutoa mchango wake katika mfuko wa kuziokoa nchi zanachama wa Euro zitakazojikuta matatani. Ujerumani , itachangia Euro bilioni 123 sawa na dala Bilioni 157.Kuna onyo kwamba, mchango wa Ujerumani, yamkini ukapanda na kufikia Euro Bilioni 150.

Baada ya kupanda kwa nguvu thamani ya sarafu ya Euro hapo jana kutokana na kupitishwa mfuko wa pamoja wa kima cha Euro bilioni 750 kuziokoa nchi zanachama zinazoweza kujikuta matatani, masoko ya hisa yalirudi leo kudorora mwanzoni mwa shughuli zake.

Masoko ya hisa ya London,Frankfurt na Paris, yote yalijikuta chini kwa kima cha 1.5%.Huko barani Asia, masoko ya hisa ya Tokyo,Syndney na Hong Kong yote yalimaliza shughuli zao leo kwa kuanguka thamani ya kima cha 1.1%.Sarafu ya Euro ambayo muda mfupi jana ilipanda hadi dala 1.30 ilipoteza nguvu mbele ya sarafu kuu na leo alaasiri, ilifikia dala 1.2718 mjini Tokyo.

Serikali kuu zilielezea matumaini kuwa kitita kilicho idhinisha cha Euro bilioni 750 kati ya Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kingekuwa ngao ya kujikinga na mzozo mpya wa madeni usitikse uchumi wa dunia.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Robert Gibbs, amearifu kwamba, rais Barack Obama wa Marekani na timu yake ya mabingwa wa uchumi waliridhika na hatua iliochukuliwa na Umoja wa ulaya.

Lakini, masoko ya fedha na wachambuzi yanatia shaka shaka kuwa hiyo ilikua dawa mujarabu huku kila mmoja akisubiri iwapo Ugiriki, itachukua kweli hatua ilioahidi kupunguza madeni yake ya kima cha 13.6% ya pato la Taifa na Ureno na Spain, kutangaza hatua zao za kubana matumizi.

Mwandishi:Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman