1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki kupatiwa mkopo wa Euro bilioni 43.7

27 Novemba 2012

Mawaziri wa Fedha wa kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro leo wameidhinisha Euro bilioni 43.7 ikiwa ni katika juhudi za kuunusuru uchumi wa Ugiriki.

https://p.dw.com/p/16qLQ
Mawaziri wa Fedha wa Umoja wa Ulaya
Mawaziri wa Fedha wa Umoja wa UlayaPicha: Reuters

Makubaliano hayo baina ya mawaziri hao na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, kuhusu mpango wa kupunguza madeni ya Ugiriki, yamefikiwa mapema leo baada ya mazungumzo ya mjini Brussels yaliyodumu kwa saa 12. Mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya Euro, Jean-Claude Juncker, amesema kuwa fedha hizo zitatolewa kwa awamu nne kuanzia tarehe 13 Disemba hadi mwishoni mwa mwezi Machi mwakani.

Jean-Claude Juncker
Jean-Claude JunckerPicha: Reuters

Mpango huo ulikuwa mgumu kufikiwa

Hata hivyo Ugiriki bado inahitaji kutimiza masharti yaliyofikiwa. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Juncker amekiri kuwa huo umekuwa mpango mgumu kufikiwa na ameelezea jitihada kubwa zilizofanywa na washiriki wote. Amesema suala hilo ni ahadi ya mustakabali wa baadae kwa watu wa Ugiriki na kanda inayotumia sarafu ya Euro kwa ujumla.

Mawaziri hao wamekuwa katika wakati mgumu kufikia makubaliano na wakopeshaji wengine wa kimataifa wa Ugiriki ambao ni Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF na Benki Kuu ya Ulaya-ECB, baada ya kuahirisha uamuzi huo mara mbili katika muda wa wiki tatu zilizopita. Ugiriki imekuwa ikisubiri mkopo huo tangu mwezi Juni mwaka huu. Kamishna wa Uchumi wa Umoja wa Ulaya, Olli Rehn, amesema ni juhudi za Ugiriki katika kutekeleza hatua kali za kubana matumizi ndio zimesababisha mpango huo kufikiwa. Rehn amesema hilo lilikuwa jaribio halisi la uaminifu kwa kanda inayotumia sarafu ya Euro na kwamba wasingeweza kushindwa.

Waziri Mkuu wa Ugiriki apongeza

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras ameipongeza hatua hiyo akisema ni mwanzo mpya kwa taifa lake. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya makubaliano hayo kufikiwa, Samaras amesema kila kitu kimekwenda sawasawa na kwamba Wagiriki wote waliupigania uamuzi huo na siku mpya imewadia kwa kila Mgiriki.

Waziri Mkuu wa Ugiriki, Antonis Samaras
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Antonis SamarasPicha: reuters

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schaeuble amesema mpango huo utawasilishwa kwa wabunge wa Ujerumani ifikapo mwishoni mwa juma hili. Nchi nyingine wanachama wa kanda ya sarafu ya Euro pia zitapaswa kupata idhini ya mabunge yao kuhusu mpango huo.

Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, Christine Lagarde amesema makubaliano yaliyofikiwa yana lengo la kuiona Ugiriki inapunguza madeni yake kutoka asilimia inayokadiriwa kufikia 144 hadi asilimia 124 ifikapo mwaka 2020 na kikubwa hasa kuwa chini ya asilimia 110 ifikapo mwaka 2022. Amesema IMF inataka kuhakikisha washirika wa kanda inayotumia sarafu ya Euro wanachukua hatua madhubuti kuhakikisha madeni ya Ugiriki yanakuwa katika njia ya maendeleo endelevu na kwamba suala hilo limekuwa na mafanikio.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,AFPE
Mhariri:Hamidou Oummilkheir