1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Ugiriki

20 Julai 2015

Mzozo wa madeni ya Ugiriki,ziara ya waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel nchini Iran na kufunguliwa upya ofisi za balozi za Marekani na Kuba mijini Havanna na Washington ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/1G1cu
Watu wakimbilia kununua vitu vya anasa nchini UgirikiPicha: DW/O. Gill

Tuanzie lakini moja kwa moja na mzozo wa madeni ya Ugiriki na kishindo chake katika siasa za Ujerumani.Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaahisi wakati umewadia wa kutambua kuna kinachotokea nchini Ugiriki-kama bado si kiuchumi,mradi kisiasa.Nchi hiyo imekubali shingo upande na baada ya upinzani wa muda mrefu,kuachilia mbali sehemu kubwa ya mamlaka yake.Badala yake lakini inajipatia mshikamano usiokuwa na mfano.Na kwa kuwa hiyo ndio hali ya mambo,na benki nazo zinafunguliwa upya hii leo.Na kwa kuwa hivyo ndivyo mambo yalivyo,watu wasishangae kama kiu cha wawekezaji kitazidi.Angalao hatari tatu kubwa za kisiasa zimeweza kuepukwa:Nchi hiyo na wakaazi wake hawatotumbukia katika janga la vurugu.Athens haioni kama imepigwa kumbo na zaidi kuliko yote;Ulaya haijagawika kati ya wajerumani wanaofuata msimamo mkali na wafaransa,wanaofuata msimamo ambao si mkali sana.Hali ya kutisha ilijitokeza kabla ya maridhiano kufikiwa.Licha ya yote lakini bara kongwe limefanikiwa kujikwamua.

Mzozo wa Ugiriki umeshawishi kwa njia moja au nyengine siasa ya ndani nchini Ujerumani.Vyombo vya habari vimefika hadi ya kudai eti waziri wa fedha Wolfgang Schäuble anafikiria uwezekano wa kujiuzulu.Gazeti la "Rhein -Necker-Zeitung" linaandika:"Berlin imepigania masilahi ya wajerumani kama ilivyowezekana.Schäuble amekamata msimamo shupavu kwa lengo la kufikia shabaha hiyo-na serikali ya muungano nayo imejipatia shukurani za wananchi.Kwa hivyo hakuna sababu za Schäuble kujiuzulu-ila tu kama serikali sarafi hii inapanga kuendeleza peke yao domo la msimu wa kiangazi."

Ziara ya kihistoria ya Sigmar Gabriel nchini Iran

Ziara ya wazri wa uchumi wa serikali kuu nchini Iran,Sigmar Gabriel nbayo pia imemulikwa magazetini.Gazeti la "Münchner Merkur" linaandika:"Wote wanapiga foleni,tangu"Mhimili wa maovu"ulipoporomoka na Iran kujongelea uwanja wa wenye uwezo na kumezewa mate.Ziara ya Gabriel kwa hivyo inaweza kugeuka mwanzo wa enzi mpya.Uchumi wa Ujerumani unaihaitaji haraka Iran nchi ambayo ni tajiri kwa mafuta na itakayokuwa na fedha.Ishara kutoka Teheran zinatia moyo.Ujerumani ikiiacha fursa iliyojitokeza,China itafaidika -na kama ilivyoshuhudiwa wakati wa vikwazo-itaendelea kuwa nchi inayoneemeshwa zaidi na Iran."

Marekani na Cuba zajongeleana tena

Mada ya mwisho magazetini inahusu enzi mpya kati ya Marekani na Cuba ambazo leo hii zinapanga kufungua upya ofisi zao za ubalozi katika miji mikuu ya nchi hizo mbili.Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linaandika:

"Yote hayo hayamaanishi kwamba kufumba na kufumbua mageuzi na marekebisho yatafanyika.Cuba inasalia bado kuwa nchi yenye utawala wa kiimla-nchi inayohitaji kufanya mengi katika masuala ya haki za binaadam.Asiye uona ukweli huo,anajidanganya.Hata hivyo lakini mbegu zimeshasambazwa.Kama ilivyotokea wakati mmoja nchini Ujerumani,pale Willy Brandt na Egon Bahr walipojaribu,licha ya upinzani mkali kutoka vyama vya upinzani,kuleta mepya,ambayo tija yake ilipatikana miaka 20 baadae.Rais Barack Obama nae pia atapata tija kama hiyo.Kwasababu kila wakati ambapo wacuba walio wengi wataanza kuonja "maisha ya kawaida"ndipo nacho kilio cha uhuru kitakapozidi kuhanikiza.Kuanzishwa upya uhusiano wa kibalozi ndio mwanzo wa hali hiyo."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Josephat Charo