1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yagubikwa na moto

24 Agosti 2009

Nchini Ugiriki wazima moto wanaendelea na harakati za kupambana na moto uliosambaa kwenye msitu ulio karibu na mji mkuu wa Athens.Moto huo umekuwa ukiwaka kwa muda wa siku nne sasa.

https://p.dw.com/p/JHDW
Moshi uliotanda UgirikiPicha: AP

Kulingana na Wizara ya Afya ya Ugiriki kiasi cha watu watano wanaendelea na matibabu baada ya kupata majeraha ya moto na wengine kadhaa wameripotiwa kuwa na matatizo ya kuvuta pumzi.Ugiriki iliathiriwa na moto kama huo mwaka 2007 ambapo watu 65 walifariki.

Helikopta nne,malori 187 ya kuzima moto pamoja na kiasi cha wazima moto 430 waote wanashirikiana kupambana na moto huo.Wanajeshi 300 nao pia wamejiunga na operesheni hiyo.

Tayari ndege za Italia na Ufaransa nazo zimewasili Ugiriki ili kuiimarisha operesheni hiyo ya kuuzima moto huo uliosambaa hadi Athens mjini.Kwa mujibu wa Ordanis Louizos,meya wa mji wa Nea Makri ulioathirika zaidi na moto huo operesheni hiyo ilianza tangu mapema asubuhi na wanataraji moto huo utazimwa katika kipindi cha siku moja.

Maelfu walazimika kukimbia

Hapo jana moto huo ulipungua katika mitaa iliyoko karibu na mji wa Athens wakati ambapo uongozi wa Ugiriki uliwatolea wito maelfu ya wakazi wa eneo hilo kuyaondoka makazi yao.Miale ya moto iliripotiwa kuishambulia misitu ila pepo kali nazo zilikuwa zinauchochea.

Ministerpräsident Kostas Karamanlis
Waziri Mkuu wa Ugiriki Costas KaramanlisPicha: Botschaft Griechenland

Hata hivyo wengi ya wakazi wa eneo lililo karibu na Athens walitumia mabomba ya maji na vitata kuuzuwia moto kuzifikia nyumba zao.Operesheni za kuuzima moto huo ni changamoto kubwa kwa serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu wa Ugiriki Costas Karamanlis inayozongwa na matatizo ya kisiasa baada ya upinzani kutisha kuwa huenda wakaitisha uchaguzi wa mapema pale rais mpya atakapochaguliwa ifikapo mwezi wa Machi.Ikumbukwe kuwa watu 65 walipoteza maisha yao mwaka 2007 pale moto ulipoivamia Ugiriki katika kipindi cha siku 10.

Serikali imezembea

Kulingana na upande wa vyama vya upinzani juhudi hizo za kupambana na moto zingeweza kusimamiwa kwa njia bora zaidi tofauti na hali ilivyo kwa sasa.Chama cha Kikomunisti kwa upande wake kimeitolea wito serikali kukodisha ndege zaidi zitakazotumiwa katika operesheni hiyo kwasababu Ugiriki ina uhaba wa nyenzo hizo maalum.

Juzi Jumamosi serikali ilitangaza hali ya hatari katika eneo la Attica lililoko mashariki mwa nchi ambako eneo lililo na ukubwa wa kiasi cha ekari alfu 37 la misitu,mashamba na miti ya figili liliteketea.Kwa sasa Ugiriki imepata usaidizi wa mataifa mawili wandani wa Umoja wa Ulaya baada ya idara ya utabiri wa hali ya hewa kutangaza kuwa pepo kali bado zinatarajiwa hadi wakati wa jioni.Helikopta nne,malori 187 ya kuzima moto pamoja na kiasi cha wazima moto 430 waote wanashirikiana kupambana na moto huo.Wanajeshi 300 nao pia wamejiunga na operesheni hiyo.Moto huo ulianza siku ya Ijumaa iliyopita katika kijiji cha Grammatiko kilicho umbali wa kilomita 40 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Athens.Baada ya moto huo kusambaa wakazi walilazimika kuondoka kwenye hospitali moja ya watoto,nyumba moja ya wazee pamoja na nyumba ya watawa.Ugiriki imekuwa ikitatizwa na moto hususan wakati wa kipindi cha joto barani Ulaya kwasababu ya viwango vya juu vya joto,pepo kali na ukavu kwa jumla.Mwezi uliopita maeneo mengi ya Ulaya ya kusini ya misitu pamoja na nyumba yaliteketea kwasababu ya hilo.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya DPAE/RTRE/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman