1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yakubaliwa mkopo na jumuia ya kimataifa

Oumilkher Hamidou3 Mei 2010

Ugiriki yapatiwa mkono wa mabilioni ya yuro kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuinusuru isifilisike

https://p.dw.com/p/ND4E
Waziri wa fedha wa Ugiriki Papakonstantinou(kushoto) na mwenyekiti wa zoni ya yuro Jean-Claude JunckerPicha: AP

Mataifa ya zoni ya Yuro yameridhia hatua za kufunga mkaja za Ugiriki na yanapanga hivi sasa kuipatia nchi hiyo msaada wa yuro bilioni 110 ili kuinusuru isifilisike.Ugiriki itapatiwa mkopo huo mnamo miaka mitatu ijayo.

Waziri mkuu wa Luxembourg Jean Claude Juncker ametangaza uamuzi huo kufuatia mkutano wa mawaziri 16 wa fedha wa zoni ya Yuro mjini Brussels.Mataifa ya zoni ya yuro yatatoa yuro bilioni 80 na yuro bilioni 30 zitatolewa na shirika la fedha la kimataifa IMF.Kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa Ujerumani itaikopesha Ugikiri yuro kati ya bilioni 22 na bilioni 23.

Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imesema kupitia mwenyekiti wake José Manuel Barroso masharti ya Ugiriki kuweza kupatiwa mkopo yametekelezwa.Lakini muhimu zaidi yalikua maoni ya mataifa wanachama.Mwenyekiti wa zoni ya Yuro Jean Claude Juncker anasema:

"Mataifa 16 ya zoni ya Yuro yamekubaliana kuunga mkono utaratibu wa kutoa msaada.Msingi wa hayo ni ripoti ya benki kuu ya Ulaya na halmashauri kuu inayozungumzia juu ya hatari ya kuvurugika hali ya ya fedha katika zoni ya Yuro."

Wolfgang Schäuble Pressekonferenz Griechenland
Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani,Wolfgang SchäublePicha: AP

Nchi za zoni ya Yuro na shirika la fedha la kimataifa wamepanga kuipatia Ugiriki katika kipindi cha miaka mitatu ijayo mkopo wa jumla ya yuro bilioni 110. Viongozi wa taifa na serikali wa nchi wanachama wa zoni ya Yuro wanapanga kukutana mjini Brussels kutia saini mopango huo.Katika baadhi ya nchi,ikiwa ni pamoja na shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,bunge lakini litatakiwa liidhinishe uamuzi huo.Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang Schäuble anasema:

"Wazungu wote-na wajerumani ni wazungu-wamejiwekea lengo la kuhifadhi utulivu wa sarafu ya yuro.Hilo ndilo jukumu letu, huo ndio wajib wetu.Kila tutakapoutekeleza ipasavyo ndivyo itakavyo leta tija kwa Ulaya na hivyo kwa wajerumani wote."

Kansela Angela Merkel anapanga kuzungumzia mpango huo pamoja na serikali yake kabla ya kuufikisha bungeni ijumaa ijayo kuidhinishwa.

Mwandioshi: Hasselbach, Christoph/ZR/Hamidou,Oummilkheir

Imepitiwa na:Mohammed Abdul-Rahman