1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yasema haitakubali shinikizo

Elizabeth Shoo2 Juni 2015

Angela Merkel, Francois Hollande na mashirika yaliyoikopesha Ugiriki, wamefanya mkutano wa dharura kujadili uwezekano wa Ugiriki kurejesha madeni yake. Serikali ya Ugiriki lakini inakataa shinikizo.

https://p.dw.com/p/1FaXc
bendera za Ugiriki na Umoja wa Ulaya
Picha: Reuters/Y. Herman

Kwa Ugiriki muda unazidi kuyoyoma. Hadi kufikia Juni 5, serikali ya nchi hiyo inapaswa kulipa deni lake la euro milioni 300 kwa Shirika la Fedha Duniani IMF.

Jumatatu usiku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa Ufaransa Francois Hollande na mkuu wa IMF Christine Lagarde walikutana mjini Berlin kutathmini kama kweli Ugiriki itaweza kulipa deni hilo. Aidha, walitafuta namna ya kuishawishi nchi hiyo irejee kwenye meza ya mazungumzo. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na mkurugenzi wa benki kuu ya Ulaya, Mario Draghi na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker.

Ugiriki lazima iendeleze mazungumzo na wakopeshaji wake na iweke bayana mipango yake ya kuleta mabadiliko ya sera za kiuchumi. Iwapo wakopeshaji wataridhika na mipango hiyo, basi wataipatia serikali ya waziri mkuu Alexis Tsipras euro bilioni 7.2 ambazo zilikuwa zimesalia kwenye mfuko uliowekwa kwa ajili ya kuufufua uchumi wa Ugiriki.

Hofu ya kutolewa kwenye ukanda wa euro

Lakini kuijumla wachumi na hata raia wa Ugiriki bado wanahofia kwamba upo uwezekano wa Ugiriki kushindwa kulipa madeni yake na hivyo kulazimika kujiondoa kwenye kundi la nchi zinazotumia sarafu ya euro. "Tuna wasiwasi mkubwa. Nadhani tukitoka kwenye ukanda unaotumia sarafu ya euro, utalii itaathirika vibaya," anasema Alexandro Vardis, raia wa Ugiriki anayemiliki mgahawa wa kitalii. "Serikali lazima ilipe deni kwa shirika la fedha duniani ili tuweze kusonga mbele na kuachana na shida hizi."

Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras
Tsipras: "Tumekabidhi orodha ya mabadiliko ya sera."Picha: Louisa Gouliamaki/AFP/Getty Images

Naibu waziri mkuu wa Ugiriki, Yannis Dragasakis ameahidi kuwatetea wananchi wake. Kupitia mtandao wa Twitter, mwanasiasa huyo ametangaza kuwa hatakubali shinikizo kutoka kwa wakopeshaji wa nchi yake. Dragasakis amesema pia kuwa raia wake hawawezi kuhimili mipango mikali zaidi ya kubana matumizi. Hata hivyo ameahidi kuwa serikali yake itafanya kila liwezekanalo ili kufikia makubaliano na Umoja wa Ulaya. Wakati huo huo, waziri mkuu Tsipras ametangaza kuwa serikali yake imeshawatumia viongozi wa Umoja wa Ulaya na IMF orodha kamili ya mabadiliko ya sera yaliyopangwa.

Merkel na wenzake hawakutoa tamko rasmi baada ya kikao chao. Lakini kwa mujibu wa ripoti ya ofisi ya kansela, wote waliohudhuria wameapa kuongeza juhudi katika kutafuta suluhu na kuwa wataendelea kujadiliana na Ugiriki.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa/reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga