1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa usiojuilikana waendelea kusambaa Uganda

Caro Robi13 Januari 2012

Maafisa wa afya wa Uganda na wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wamesema wanashirikiana kudhibiti ugonjwa usiojulikana ambao umewaathiri karibu watu 3,000, hasa watoto, nchini Uganda.

https://p.dw.com/p/13izx
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: AP

Maafisa hao wa afya wamesema bado hawajaweza kubaini chanzo cha ugonjwa huo ambao vyombo vya habari nchin humo vimeripoti kuwa umewauwa zaidi ya watu 100 nchini Uganda tangu kuanza na sasa unasambaa kwa haraka. Wilaya tano kaskazini mwa nchi hiyo zimeripioti visa vya ugonjwa huo wa ajabu ambao wataalamu wa afya wameshindwa kuungamua kufikia sasa.

Msemaji wa wizara ya afya nchini humo Rukia Nakamatte amesema serikali inatoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kijamii na kutoa dawa za kupunguza maumivu huku ikiandaa mpango kabambe utakaohusisha utafiti,matibabu na hatua za kuzuia ikiwemo kutoa virutubishi.

Wanasayansi wanasema huenda ugonjwa huo wa kutikisa kichwa unasababishwa na ukosefu wa virutubisho katika lishe za waathiriwa. Dalili zake ni mgonjwa kutikisa kichwa mfululizo,udhaifu,kutoweza kufanya lolote,matatizo ya ubongo na kifafa kikali.

Kundi moja la watafiti wa serikali lilitumwa katika eneo hilo la kaskazini mwa Uganda wiki iliyopita lakini halikuafikia lolote la kutatua kitendawili hicho.

Huku utafiti ukiendelea, mipango inawekwa ya kuwafunza wafanyakazi wa kijamii watakaokwenda vijini kuwaelimisha watu kuhusu umuhimu wa lishe bora.

Watoto nchini Uganda.
Watoto nchini Uganda.Picha: DW

Wizara ya afya pia inatarajiwa kusambaza mahospitalini dawa ijulikanyao Carbimazole inayotoa afueni kwa wagonjwa hao ambao wengi ni watoto wa kati ya umri wa miaka 5 na miaka 18.

Kulingana na Dakatri Lawrence Ojom ambaye ni mkurugenzi wa Hospitali moja kaskazini mwa wilaya ya Kitgum eneo ambalo limeathirika zaidi na ugonjwa huo, ni kwamba hospitali katika eneo hilo hazina uwezo wa kuwahifadhi wagonjwa hao kwani idadi ya walioathirika ni kubwa na kwasababu bado ufumbuzi wa tiba haujapatikana, haitawezekana kwa hospitali kuwaweka katika vyumba vya kulaza wagonjwa idadi kubwa namna hiyo.

Mwakilishi wa shirika la afya duniani WHO nchini Uganda Solomon Fisseha amesema shirika lake linatafuta fedha za kusaidia tatizo hilo na kama fedha hizo zitapatikana zitatumika kutoa lishe bora.

Fisseha amesema ugonjwa huo mara ya kwanza uligundulika nchini Tnazania katika miaka ya 60. Inaaminika kuwa ugonjwa huo ni aina nyingine ya ugonjwa wa kifafa uliokomaa ambao unaweza kuzuilika kwa kupata lishe bore.

Mwandishi: Caro Robi/DPA
Mhariri: Othman Miraji