1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa saratani ya kizazi huwakumba zaidi wanawake katika nchi zinazoendelea

Kabogo Grace Patricla17 Novemba 2008

Kati ya wanawake 490,000 duniani kote wanaobainika kuugua saratani ya kizazi kila mwaka, asilimia 80 wanaishi katika nchi zinazoendelea. Kila mwaka wanawake 55,000 wa Jangwa la Sahara peke yake wanaugua ugonjwa huo.

https://p.dw.com/p/Fwa8
Mmoja wa wanawake waathirika wa virusi vya Ukimwi nchini Afrika Kusini, ambaye pia ni rahisi kuambukizwa virusi vya HPV vinavyosababisha saratani ya kizazi.Picha: AP

Linda Gail-Bekker mtaalamu katika Kituo cha Ukimwi cha Desmond Tutu nchini Afrika Kusini, amesema kabla ya kuwepo kwa dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa Ukimwi ARVs, wanawake wenye saratani ya kizazi walikuwa hawaonekani kwa sababu walifariki kutokana na kuugua Ukimwi. Lakini tangu kuanza kutumika kwa ARVs, hivi sasa wanawake wengi ambao wameathirika virusi vya Ukimwi, mara nyingine pia huwa wanaugua saratani ya kizazi.


Kwa mujibu wa Bibi Gail-Bekker, matatizo ya kupungua kwa kinga mwilini kwa watu wanaoishi na virusi vya HIV vinasababisha miili yao pia kupata virusi vya Human Papillomavirus(HPV). Virusi hivyo vinavyoambukizwa kwa njia ya kujamiiana, ni sababu kubwa inayochangia kuambukiza saratani ya kizazi.


Ameongeza kuwa wakati mtu anapoambukizwa virusi vya HPV, virusi hivyo baada ya muda hubadilisha seli za mlango wa uzazi na hiyo huenda ikasababisha mtu kupata saratani endapo haitatibiwa haraka.


Mtaalamu huyo amefafanua kwamba kuna tiba nyingi za virusi vya HPV, ambazo ni pamoja na kugandisha seli zisizo za kawaida pamoja na nitrojeni ya maji na kisha kuziondoa, au kuziharibu kwa kutumia mkondo wa umeme usio na maumivu.


Kwa bahati mbaya vipimo vya kuchunguza saratani ya kizazi katika maeneo mengi duniani ni pungufu, hasa katika nchi zinazoendelea. Afrika Kusini, nchi yenye idadi kubwa ya waathirika wa virusi vya Ukimwi duniani, haina cha kuepuka.


Zahanati nyingi nchini Afrika Kusini, hasa katika maeneo ya vijijini hazina vifaa vingi vya kuchunguza saratani ya kizazi kwa ufasaha na utaalamu. Mbali na tatizo hilo, uelewa mdogo pia ni kikwazo cha kukabiliana na virusi vya HPV na saratani ya kizazi. Watu wengi wana ufahamu kuhusu virusi vya Ukimwi kuliko virusi vya HPV.


Njia moja ya kuwazuia wanawake katika nchi zinazoendelea kufariki kutokana na saratani ya kizazi, ni kutolewa kwa chanjo moja kati ya mbili za kutibu ugonjwa huo, ambayo kwa sasa inasambazwa na kampuni ya madawa ya Merck na GlaxoSmithKline.


Ikihusisha dozi tatu, chanjo zote zinazuia virusi hatari vya aina mbili vya HPV vijulikanavyo kama strains 16 na 18. Ni sahihi zaidi kuwachanja wanawake na wanaume kabla hawajajamiiana, kabla maambukizi hayajaanza.


Afrika Kusini wanawake 33,000 wamefariki kutokana na kuugua saratani ya kizazi tangu mwaka 1997 na 7,000 huambukizwa ugonjwa huo kila mwaka kutokana na dawa ya chanjo ya ugonjwa huo kuuzwa kwa bei ya juu sana.


Katika vituo binafsi vya afya, dawa ya chanjo ya saratani ya kizazi inauzwa randi 2,100 ambayo ni sawa na dola 200 kwa dozi tatu ambazo zinatakiwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo. Wengi wa wananchi wa Afrika Kusini hawawezi kumuda gharama hiyo na asilimi 86 ya wananchi hao wanategemea matibabu kutoka katika vituo vya afya vya serikali.