1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

121011 Hunger und Sicherheit

21 Oktoba 2011

Katika nchi nyingi pametokea vurugu zilizosababishwa na kupanda kwa bei ya vyakula au uhaba wa chakula. Tatizo hilo linaweza kukua kadri idadi ya watu waishio duniani inavyoongezeka.

https://p.dw.com/p/12rvg
Watu wengi duniani wanakabiliwa na kitisho cha janga la njaaPicha: picture alliance/dpa

Robert Malthus alikuwa mchungaji na mwanauchumi kutoka Uingereza aliyeishi katika karne ya 18. Baada ya kuona ghasia zikizuka katika miji ya London na Paris kutokana na uhaba wa chakula, Malthus alitoa nadharia inayosema kwamba rasilimali zilizopo duniani zinatosha kulisha idadi fulani tu ya watu. Idadi hiyo inapoongezeka, njaa, majanga na vita hutokea ili kupunguza idadi ya watu hadi kufikia kiwango kinachotakiwa.

Wakati huu idadi ya watu ulimwenguni imefikia billioni saba na inatarajiwa kufikia billioni tisa ifikapo mwaka 2050. Mbinu za kisasa za upandaji wa mazao pamoja na mifumo ya kibiashara inayoiunganisha dunia nzima inatoa ishara potofu kwamba idadi ya watu inaweza kuongezeka tu, bila kuleta madhara yoyote. Ukweli ni kwamba kila mtu wa saba duniani anakabiliwa na kitisho cha janga la njaa. Janga hilo pamoja na athari zake zinatishia usalama wa watu binafsi na hata wa mataifa kwa ujumla.

Wolfgang Heinrich, mtaalamu wa masuala ya kilimo wa shirika la misaada ya maendeleo la Kanisa la Kiinjili Ujerumani anaeleza:

"Kwa kawaida njaa hutokea katika maeneo ya vijijini. Mara nyingi serikali zinafanikiwa kukidhi mahitaji ya watu wanaoishi mijini kwa mfano kwa kupunguza bei na kutoa ruzuku kwa ngano inayonunuliwa kutoka nje.  Pia, serikali nyingi hujaribu kuwanyamazisha kwa nguvu watu wanaozusha ghasia katika maeneo ya vijijini. "

Proteste in Tunesien
Watunisia wakiandamana kupinga kupanda wa bei ya vyakulaPicha: dapd

Wakati wa mgogoro wa chakula uliotokea mwaka 2008 jambo hilo lilitokea tena. Maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya vyakula yalizuka katika nchi za Afrika na za Karibik. Baadhi ya serikali zilianza kuyumba na wakati mwengine serikali hizo hizo zilijikuta katika migongano na makundi mengine ya kisiasa  katika nchi zao. Joachim von Braun ni mkuu wa taasisi ya utafiti wa masuala ya maendeleo iliyopo mjini Bonn, Ujerumani.

"Uchunguzi tuliofanya unaonyesha kwamba katika kipindi cha mgogoro wa chakula wa mwaka 2008 palikuwa na vurugu na maandamano zaidi ya mara 50. Wakati mwingine utawala ulipinduliwa. Hili lilikuwa jambo jipya. Vurugu hizo zilizuwa wasiwasi mkubwa kwa wanasiaisa duniani kote," anaeleza von Braun. "Tangu wakati huo suala hili linajadiliwa hata na Umoja wa Mataifa na nchi za G20. Mpaka sasa bado bei za vyakula ziko juu sana na vurugu zinaendelea lakini si kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa mwaka 2008."

Ni vigumu kuonyesha kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya uhaba wa rasilimali na migogoro. Inaweza kusema kwamba upungufu wa rasilimali katika nchi na maeneo ambayo hayana amani ya kutosha unaweza kuwa chanzo cha vurugu. Lakini mara nyingi njaa au uhaba wa chakula ni chanzo kimoja tu kati ya vingi. Kutokuwepo kwa  mgawanyo wa haki pamoja na utawala mbaya pia vinachangia kuzua tatizo hilo ambalo si la kijamii tu, bali pia la kiusalama. Mara nyingi maandamano ya kupinga bei kubwa za vyakula hugeuka na kuwa maandamano dhidi ya serikali tawala.

Nchini Kenya ukodishwaji na uuzaji wa mashamba makubwa kwa wawekezaji kutoka nje unawatia watu wengi uchungu. Wakati mwingine watu hao hutumiwa na makundi ya magaidi wa kiislamu. Wolfgang Henrich anaeleza kuwa shughuli za makundi hayo katika nchi za pembe ya Afrika zimeongezeka katika miaka michache iliyopita.

Piraten auf dem Deck der gekapertern Luxusjacht Le Ponant vor Somalia
Meli iliyotekwa na maharamia wakisomaliPicha: picture-alliance/dpa

"Kaskazini mwa Kenya yapo makundi yanayohusika na migogoro ya nchini Somalia. Wapo wasomali wanaoishi Kenya. Jinsi jumuiya ya kimataifa ilivyokuwa ikiushughulikia mgogoro wa Somalia katika miaka 20 iliyopita, imesababisha wapiganaji wa kisomali wanaoishi katika nchi mbali mbali nao kuamua kuunda mtandao wa kimataifa tangu mwaka 2006, hasa kuwa na mafungamanao na ushirikiano na makundi ya Al-Qaeda na Wataliban," anaeleza Heinrich.

Mara nyingi watu walioathirika na janga la njaa hawako tayari kupigana kwa kutumia silaha. Wako radhi kukimbia makazi yao wakiwa wanatafuta chakula. Matatizo ya mgawanyo wa chakula barani Afrika yanatokea mara nyingi katika kupokea wakimbizi. Wakati mwingine watu wanaoshindwa kuzilisha familia zao hutafuta njia mbadala ya kupata riziki. Uharamia katika nchi za pembe ya Afrika ulisababishwa na uvuvi uliopita kiasi uliokuwa ukifanywa karibu na pwani ya Somalia. Hivi sasa maharamia wameamua kujinufaisha na meli zinazovua katika pwani hiyo.

Wataalamu wanatabiri kwamba hapatakuwa na vita vya kupigania chakula katika siku za usoni, licha ya kwamba kuna dalili nyingi zinazoashiria hilo. Hata hivyo, mtafiti wa masuala ya maendeleo anaeleza kwamba wasiwasi juu ya uhaba wa chakula utasababisha kuongezeka kwa athari za kiusalama na za kisiasa ulimwenguni kote.

"Ninatarajia kwamba migogoro inayosababishwa na uhamiaji pamoja na migogoro kuhusu umiliki wa ardhi itaongezeka na kuyumbisha serikali mbali mbali,"

Mwandishi: Scheschkewitz, Daniel/Shoo, Elizabeth

Mhariri: Josephat Charo

ENDE