1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhaba wa maji waitatiza dunia

Louise Osborne22 Machi 2016

Siku ya Maji Duniani inaadhimishwa tangu mwaka wa 1993 kutokana na azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mwaka huu wataalamu wanaonya kwamba uhaba wa maji unaongezeka katika maeneo mengi.

https://p.dw.com/p/1IHRP
Maji Ghana (c) DW/M. Suuk
Picha: DW/M. Suuk

Uhaba wa maji ni tatizo kubwa duniani kote. Kwa mujibu wa mhariri mkuu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa Richard Connor tatizo hilo linazidi kuwa kubwa. Ameiambia DW kwamba maji yanaendelea kupungua wakati ambapo idadi ya watu inaongezeka na shughuli za kiuchumu zinazidi kupanuka duniani kote.

Mhariri huyo amesema kutokana na ongezeko la watu na ustawi wa uchumi mahitaji ya maji yamekuwa yanaongezeka lakini ugavi wake unapungua.

Asilmia 70 ya maji safi yanayotokana na vyanzo asilimia yanatumika kwa ajili ya shughuli za kilimo kama vile kumwagilia mashamba ya ngano na mpunga. Uzalishaji wa nishati unatokana na matumizi ya asilimia 15 ya maji, na asilimia 5 inatumika majumbani.

Kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa idadi ya watu duniani, ugavi wa maji utazidi kutatizika. Kwa mujibu wa utabiri, idadi wa watu duniani itafikia bilioni 9.3 mnamo mwaka wa 2050, yaani asilimia 33 zaidi ya idadi ya mwaka wa 2014.

Maji yatakiwa kuhifadhiwa

Heka heka za kutafuta maji nchini Ghana (c) DW/M. Suuk
Heka heka za kutafuta maji nchini GhanaPicha: DW/M. Suuk

Maeneo ya Asia ya kati, Mashariki ya Kati, Marekani na China yamepungukiwa maji. Hata hivyo mhariri wa ripoti ya Umoja wa Mataifa Richard Connor ameeleza kuwa nchi zinazoeindelea zimo katika hali nzuri kutokana na kuwa nazo akiba za maji na kutokana na mazingira yanayochangia katika upatikanaji wa maji.

Wakati huo huo, usimamiaji mbaya wa maji unasababisha uhaba wa raslimali hiyo. Richard Connor amesema wakati mwingine maji yapo lakini hayatumiki vizuri. Katika nchi zinazioendelea watu bilioni 1.8 wanatumia maji machafu.

Connor ameeleza kuwa hata katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ambako yako maji mengi, hali za kiuchumi zinasababisha uhaba wa maji kwa baadhi ya watu. Katika nchi kama Ethiopia, uhaba wa maji unasababisha matatizo makubwa katika upatikanaji wa chakula.

Njia bora za kuhifadhia maji zinahitajika. Usimamizi mzuri utasaidia kuepusha uhaba wa maji. Umwagiliaji maji mashambani unapaswa kuzingatia mbinu za kisasa. Wataalamu wanasema njia hizo zitapunguza uhaba wa chakula kwa nusu hadi ufikapo mwaka wa 2050.

Mwandishi: Abdul Mtullya/ Osborne Louise

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman