1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhalifu uko juu DRC

Admin.WagnerD30 Novemba 2010

Ripoti ya Umoja wa Mataifa yaonesha kuwa mitandao ya wahalifu inavuruga juhudi za kuleta amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

https://p.dw.com/p/QLpp
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: AP Photo

Kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inayotathmini jinsi hali ilivyo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, bado kuna ukosefu wa usalama mashariki mwa taifa hilo, licha ya kukamilika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1998 na 2000 vilivyosababisha kiasi ya raia milioni 1 na laki tatu kukimbia makaazi yao. Bado kuna upinzani mkali kuhusu udhibiti wa raslimali na hatimaye inavuruga mikakati ya kuleta amani.

Jopo la wataalam watano waliopewa jukumu na Umoja wa Mataifa la kufanya uchunguzi nchini humo, limesema kuna ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika jeshi la kitaifa la FARDC.

Maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi hilo wanang'ang'ania udhibiti wa maeneo ya migodi bila kujali usalama wa raia.

Ripoti hiyo, ikirejelea visa 300 vya ubakaji katika wilaya ya Walikale kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka huu, imelilaumu genge lililoundwa ndani ya jeshi la kitaifa kwa kutekeleza visa hivyo vya ubaradhuli.

Jopo hilo la Umoja wa mataifa limehitimisha kuwa waasi wa Mai Mai Sheka wapo katika mtandao wa uhalifu ndani ya jeshi la kitaifa la FARDC na wamekuwa wakilenga udhibiti wa maeneo ya migodi.

Ripoti hiyo imeandikwa kutokana na taarifa kutoka kwa Umoja wa Mataifa, makundi mashinani, ushahidi wa moja kwa moja wa wanachama wa jopo hilo na imetajwa kama ya kweli.

Msemaji wa jeshi la Jamhuri hiyo ilioko Afrika ya kati, hakujibu alipojaribu kupigiwa simu. Hata hivyo, afisa mmoja wa ngazi ya juu jeshini, Sylvain Ekenge, ameipuuza ripoti hiyo akidai wataalam waliohusika walizingatia tuhuma tu za mitaani na kuwa mahakama ya kijeshi inafuatilia mienendo ya maafisa fulani.

Baraza la usalama la Umoja wa Matiafa limeunga mkono baadhi ya mapendekezo ya ripoti hiyo, ukiwemo uchunguzi wa ukiukaji wa jeshini na kuwepo kwa masharti mapya yatakayotumiwa katika sekta ya uchimbaji madini.

Baraza hilo limeongeza muda wa vikwazo kwa mwaka mwingine mmoja. Vikwazo hivyo nia pamoja na kupiga marufuku uuzaji wa silaha kwa makundi ya waasi, marufuku ya usafiri, kuzuia mali ya washukiwa na sasa kuweko mtaalam atakayejiunga na jopo hilo kushughulikia masuala ya mali asili.

Balozi wa Marekani katika Umoja huo, Susan Rice, amesema kati ya masharti yanayohitajika ni kuhakikisha wanunuzi wa madini wanadhihirisha yanakotolewa madini hayo ili kusitisha visa vya biashara ya magendo ambayo kwa miaka mingi vimevuruga jitihada za amani.

Ripoti hiyo pia inasema kwamba wanajeshi hao wamekuwa wakifaidika kutokana na uuzaji wa dhahabu ya kima cha Dola milioni 160 kila mwaka, uuzaji wa pembe za ndovu na hata mbao, yanachangia uharibifu mkubwa wa misitu na wamekuwa pia wakiwasajili watoto jeshini.

Mwaka wa 2008, waasi kutoka Rwanda ambao wanapiga kambi mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, walijaribu kuuza mikebe sita ya kile walichodai yalikuwa madini ya Uranium yaliyokuwa yamefichwa chini ya ardhi tangu enzi za ukoloni wa Ubelgiji.

Mwandishi: Peter Moss /Reuters/AFP

Mhariri: Othman Miraji