1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi, Italia zagawana mhula wa Baraza la Usalama

Admin.WagnerD29 Juni 2016

Uholanzi na Italia zimependekeza kugawana mhula wa miaka miwili katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kufuatia kushindwa kupatikana mshindi kati yao baada ya kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/1JFSY
Uholanzi na Italia zimejikuta sambamba baada ya mizunguko itano ya kura.
Uholanzi na Italia zimejikuta sambamba baada ya mizunguko itano ya kura.Picha: Getty Images/AFP/K. Betancur

Kura hiyo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ilipigwa kuwachagua wanachama wapya watano wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la umoja huo. Ethiopia iliyowania kiti kwa ajili ya bara la Afrika, na Bolivia iliyowakilisha Amerika Kusini na Caribeani zilipita kwa kura nyingi, kwa kuwa hazikuwa na mpinzani. Hali kadhalika, Sweden na Kazakhstan zilipita bila taabu yoyote.

Upinzani mkali ulijitokeza katika kutafuta mwanachama wa tano atakayejiunga na baraza hilo la usalama kwa miaka miwili ijayo kuanzia mwaka kesho, pale Italia na Uholanzi zilipopata kura 95 kila moja, huku zikihitajika angalau 127 kushinda kiti katika Baraza la Usalama.

Baada ya mikondo mitano ya upigaji kura ambayo haikumbainisha mshindi kati ya nchi hizo mbili, baraza lilikwenda kwenye mapumziko, na baadaye mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Uholanzi na Italia, wakatangaza kupata muafaka.

Mshikamano wa kiulaya

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uholanzi, Bert Koenders alisema, ''Mimi na mwenzangu wa Italia, tungependa kuwasilisha pendekezo, ambalo limeungwa mkono na nchi za Ulaya Magharibi na makundi mengine, kwamba tungependa kuugawana mhula''.

''Maana yake ni kwamba'', ameendelea kusema Koenders, ''Italia itakuwa mwanachama wa baraza kwa kipindi cha mwaka 2017 hadi 2018, nayo Uhalanzi itakuwa katika baraza kuanzia mwaka 2018 hadi 2019''.

Uamuzi huo wa Uholanzi na Italia umechukuliwa na wanadiplomasia, kama ishara madhubuti ya uungwana na ushirikiano miongoni mwa mataifa ya Ulaya.

Kiti Katika Baraza la Usalama ni kitu cha kifahari kwa nchi nyingi
Kiti Katika Baraza la Usalama ni kitu cha kifahari kwa nchi nyingiPicha: picture alliance/AA

Siyo mara ya kwanza kutokea utaratibu huu wa nchi mbili kugawana mhula katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ilikwishatokea mara tano mnamo miaka ya 1950 na 1960, ambapo kwa mfano Czechoslovakia ilikikalia kiti cha baraza hilo mwaka 1964, na baadaye ikakikabidhi kwa Malaysia mwaka 1965.

Fahari kuwa na kiti katika baraza

Kushinda kiti katika Baraza la Usalama ni fahari kwa nchí nyingi, kwani inazipa sauti kubwa katika kufanya maamuzi ya kimataifa kuhusu amani na usalama, kwa mizozo kuanzia Syria hadi Sudan Kusini, au kukabiliana na vitisho kama vile majaribio ya silaha za nyuklia ya Korea Kaskazini, na mashambulizi ya makundi ya kigaidi kama lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Ni baraza hilo hilo ambali pia linaidhinisha na kusimamia Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani katika sehemu mbali mbali za dunia.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linao wanachama watano wa kudumu ambao pia wanayo kura ya turufu, ambao ni Marekani, Urusi, China, Uingereza na Ufaransa. Baraza hilo pia linao wanachama 10 wasio wa kudumu, ambao wanakuwa na mhula mmoja wa miaka miwili. Kila mwaka wanachaguliwa wanachama wapya watano.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/dpae

Mhariri:Yusuf Saumu