1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi nayo yatikisika

Admin.WagnerD2 Mei 2012

Uholanzi ambayo ni moja ya mataifa machache yaliyobakia yanye uchumi imara katika kanda inayotumia sarafu ya euro, inakabiliwa na kipindi kigumu cha mtikisiko wa kiuchumi na kisiasa. Nini mustakbali wa taifa hilo?

https://p.dw.com/p/14oDk
Mark Rutte alipowasili Bungeni kujadili kujiuzulu kwa serikali yake.
Mark Rutte alipowasili Bungeni kujadili kujiuzulu kwa serikali yake.Picha: REUTERS

Hii ni baada ya kuanguka kwa serikali ya nchi hiyo mwezi Aprili, kulikosababishwa na mvutano juu ya kupunguza matumizi. Nchi hiyo sasa inalaazimika kuingia katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Septemba 12 mwaka huu.

Wakati fulani, siasa za Uholanzi zilikuwa imara na zinazotabirika, lakini sasa hali imekuwa tofauti, ikiashiria tofauti za vyama katika masuala kuanzia uhamiaji na ustawi wa jamii, mapato ya serikali na gharama za kuokoa chumi za mataifa yanayokabiliwa na mizigo ya madeni katika kanda ya euro.

Hakuna chama kinachojitosheleza
Kura za maoni zinaonyesha hakuna chama chenye uwezo wa kushinda wingi wa kura kama uchaguzi ungefanyika leo hii. Kutokana na mgawanyiko uliopo kisiasa, vitahitajika vyama vitatu au vinne kushirikiana ili kuunda serikali ya mseto.

Serikali iliyoongozwa na chama cha Christian Democrat cha Waziri Mkuu Mark Rutte ilijiuzulu Aprili 23 baada ya mshirika wake, Chama cha Uhuru kukataa mapendekezo ya kupunguza bajeti kwa euro bilioni 14 kwa mwaka 2013 zinazohitajika kufikia kikomo cha nakisi ya asilimia 3 ya bajeti kilichowekwa na Umoja wa Ulaya.

Waziri wa Fedha wa Uholanzi, Jan Kees de Jager.
Waziri wa Fedha wa Uholanzi, Jan Kees de Jager.Picha: picture-alliance/dpa

Siku chache baadaye, Waziri wa Fedha, Jan Kees de Jager aliunda ushirika wa vyama vitatu vya upinzani kwa ajili ya kupitisha marekebisho ya bajeti ya serikali. Vyama hivyo, ambavyo kwa pamoja vina wingi wa wabunge, vinaweza kupitisha baadhi ya vipengele vya kupunguza bajeti kabla ya uchaguzi wa tarehe 12 Septemba.

Kama mwanchama muhimu wa kanda ya euro na mkosoaji wa mataifa ya Ugiriki na Ureno kwa kushindwa kutii kanuni za matumizi, Uholanzi nayo imejikuta katika shinikizo la kuweka mahesabu yake sawa.

Kwa sasa inaweza kupumua
Kwa kurekebisha bajeti yake, nchi hii imeepusha mgogoro uliotishia ustawi wake na sasa inaweza kupunguza nakisi yake ambayo ilitabiriwa kufikia asilimia 4.6 ya pato la jumla kwa mwaka 2013 kufikia kiwango cha chini ya asilimia 3. Haifahamiki bado ni marekebisho mangapi ya bajeti yatatekelezwa kabla ya uchaguzi kufanyika, au nini itakuwa hatma ya hatua ambazo zitakuwa bado hazijatekelezwa baada ya serikali mpya kuingia madarakani.

Marekebisho ya sasa yanahusisha kuongezwa kwa kodi ya thamani, kodi zaidi katika mafuta yanayochimbwa ardhini, mvinyo na sigara, kupunguza bajeti ya afya, kusimamisha malipo kwa wafanyakazi wa umma kwa miaka miwili na kuzidisha mara mbili kodi mpya inayotozwa kwa mabenki.

Mark Rutte akiondoka kutoka makaazi ya malkia wa Uholanzi baada ya kujiuzulu kwa serikali yake.
Mark Rutte akiondoka kutoka makaazi ya malkia wa Uholanzi baada ya kujiuzulu kwa serikali yake.Picha: AP

Makubaliano hayo bado yanahitaji kukokotolewa na ofisi ya uchambuzi wa sera za uchumi kuhakikisha kuwa itaweza kupunguza nakisi hadi chini ya asilimia 3 kwa mwaka. Vyama vya wafanyakazi na vyama vikuu vya upinzani tayari vimepinga mpango huo vikionya kuwa utaathiri ukuaji wa uchumi na kwamba utakataliwa baada ya kufanyika kwa uchaguzi.

Mpaka sasa, kama chama cha mrengo wa kushoto cha wasoshalisti ambacho kina umaarufu sawa na kile cha waliberali kwa mujibu wa kura za maoni, au kile cha wafanyakazi vingeunda serikali, baadhi ya vipengele vya bajeti ya mwaka 2013 tayari vingeshafutwa, na hivyo kuleta wasiwasi juu ya uwezekano wa Umoja wa Ulaya kufikia malengo yake.

Kazi bado kubwa
Ofisi ya uchambuzi wa sera za kiuchumi imeshaonya kuwa Uholanzi itakabiliwa na nakisi kubwa baada ya mwaka 2020 isipofanya mageuzi makubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza umri wa kustaafu, kulegeza masharti ya soko la ajira na kupunguza ruzuku za nyumba na misamaha ya kodi, ambavyo baadhi yake vinapingwa na upinzani.

Mpango wa bajeti wa mwaka 2013 unazungumzia baadhi ya mageuzi hayo ikiwa ni pamoja na kupunguza misamaha ya kodi kwa wamiliki wapya wa nyumba, kuongeza umri wa kustaafu kufikia miaka 66 mwaka 2019 na miaka 67 kufikia mwaka 2024, kuongeza malipo ya huduma za afya kwa walaji na kupunguza viwango wanavyolipwa wafanyakazi baada ya kupunguzwa kazi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman