1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi yaingia fainali ya kombe la dunia

Josephat Nyiro Charo7 Julai 2010

Uholanzi ndiyo timu ya kwanza kufuzu kwa fainali ya kombe la dunia mwaka 2010 kwa kuicharaza Uruguay mabao 3:2 katika mpambano uliochezwa katika uwanja wa Green Point, mjini Capetown huko Afrika Kusini

https://p.dw.com/p/OCHU
Wadachi wakishangilia ushindi wa timu yao dhidi ya UruguayPicha: picture-alliance/dpa

Ingawa Uholanzi bado inahitaji kucheza vizuri zaidi kufikia kiwango kinachostahili sifa ilizomiminiwa, imefaulu kuingia fainali ya kwanza tangu mwaka 1978, ambapo ilishindwa na Argentina mabao 3:1 katika kipindi cha muda wa ziada.

Uholanzi sasa inasubiri mchuano kati ya Ujerumani na Uhispania leo jioni kujua ni timu gani itakayoumana nayo kwenye fainali hiyo, itakayochezwa Jumapili ijayo mjini Johannesburg.

Mkwaju mkali wa nahodha wa Uholanzi, Giovanni van Bronckhorst, dakika ya 18 ya mchezo, uliutikisa wavu wa lango la Uruguay, na mchezaji anayechezea timu ya Bayern Munich kwenye ligi ya Ujerumani, Bundesliga, Arjen Robben, na mchezaji bora wa mchuano wa jana, Wesley Sneider, kila mmoja alikomelea msumari wa moto katika jeneza la Uruguay na kuyazika katika kaburi la sahau matumaini ya Wamarekani Kusini kusonga mbele katika fainali ya kombe la dunia.

Fußball WM 2010 Niederlande Uruguay
Arjen Robben, kulia, na kocha wa Uholanzi Bert van MarwijkPicha: AP

Nahodha wa timu ya Uruguay, Diego Forlan, mara kadhaa aliwatia hofu Wadachi na alisawazisha bao la kwanza pale mlinda lango wa Uholanzi aliposhindwa kuuzuia mkwaju wake dakika ya 41 ya mchezo, muda mfupi kabla kipindi cha mapumziko. Licha ya bao la pili la Uruguay lililofungwa na Maxi Pereira katika dakika za mwisho, juhudi za Wauruguay hazikufua dafu kuwawezesha kuwapiku Wadachi na kuingia fainali.

"Ilikuwa mechi ngumu, lakini hayo yote tumeyasahau sasa tumeingia fainali. La muhimu ni kushinda mechi yetu ya mwisho, Tuko karibu sana na hakuna kitu kikubwa zaidi ya kombe la dunia," amesema Wesley Sneider, ambaye sasa ametia wavuni mabao matano kwenye michuano ya kombe la dunia huko Afrika Kusini.

Mchezaji wa Uholanzi, Rafael der Vaart amesema anajivunia ushindi wao ingawa alihofu Uruguay wangeweza kusawazisha.

"Tunajivunia mno. Nadhani mchezo wao umekuwa mgumu, lakini tumemenyana na tulikuwa na bahati kidogo. Hatimaye tumeridhika namatokeo. Sijakumbwa na hofu kiasi hiki katika maisha yangu. Tulikaribia kushindwa kwa sababu Wauruguay walikuwa na nafasi nyingi. Lakini tumepambana na tumeshinda kwa haki."

Uholanzi haijapoteza mechi yoyote katika michauano hii na haijashindwa tangu ilipotolewa nje na Urusi kwenye michauno ya kuwania kombe la Ulaya mnamo mwaka 2008. Sasa ina nafasi ya kuwa timu ya kwanza kushinda kila mechi kwenye michauno ya kombe la dunia, tangu Brazil ilipofanya hivyo mnamo mwaka 1970.

Fußball WM 2010 Niederlande Uruguay
Arjen Robben, kushoto, akifunga bao la tatu dhidi ya UruguayPicha: AP

Kocha wa Uholanzi, Bert van Marwijk, amesema Wadachi wanaweza kujivunia timu yao. "Inafurahisha kwamba tumeweza kufanya hivi. Ni miaka 32 tangu Uholanzi ilipocheza katika fainali. Tunaweza kujivunia nchi ndogo kama hii," ameongeza kusema kocha huyo.

Kocha wa Uruguay, Oscar Tabarez, kwa upande wake amevunjika moyo kwamba timu yake imeshindwa kidogo tu. "Najivunia wachezaji wangu, nakubali kushindwa na timu ambayo ilikuwa bora kuliko sisi. Tunahuzunika kwa sababu tulikuwa karibu kuingia fainali."

Ingawa imeshindwa, Uruguay inaweza kujivunia kocha Oscar Tabarez ambaye ameingoza timu hiyo kuingia semi fainali baada ya miaka 40. Ni ufanisi mkubwa kwa nchi yenye wakaazi milioni 3.4, na sasa wachezaji wanalazimika kuweka kando huzuni yao na kujiandaa kwa mtanange wa kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu Jumamosi ijayo.

Mpinzani wa Uruguay atajulikana baada ya mechi kati ya Ujerumani na Uhispania baadaye leo, mpambano ambao ni ni marudio ya fainali ya kombe la Ulaya mwaka 2008, ambapo Uhispania iliichapa Ujerumani bao 1:0 bao lililofungwa na Fernando Torres. Ujerumani inapania kulipiza kisasi.

Mwandishi:Josephat Charo/DPAE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman