1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhondo wa AFCON wazidi kunukianukia kule Guinea ya Ikweta na Gabon

9 Januari 2012

Wachezaji nyota wa bara Afrika wanaocheza soka yao ya kulipwa katika vilabu mbalimbali vya ulaya wameanza kurejea makwao tayari kwa fainali za kombe la mataifa barani Afrika.

https://p.dw.com/p/13gbU
Mchezaji wa timu ya taifa ya Ghana Dede Ayew
Mchezaji wa timu ya taifa ya Ghana Dede Ayew (kushoto)Picha: AP

Fainali za mwaka huu zinaandaliwa nchini Guinea ya Ikweta na Gabon kuanzia tarehe 21 mwezi huu hadi 14 mwezi ujao wa Februari na zitayahusisha mataifa 16. Tayari wachezaji kadhaa wa ligi kama vile ya uingereza, ufaransa, uhispania, na hata Italia wamejiunga na kambi za mazoezi za timu zao ili kuyanoa makali. Wengine mwishoni mwa wiki walishiriki mechi za mwisho katika vilabu vyao kabla ya kufunga safari.

Shirikisho la soka barani Afrika CAF limekubali kuahirisha mchuano wa kwanza wa kufuzu kwa dimba la mataifa ya barani Afrika la mwaka 2013 kwa sababu timu ya Lesotho haikuweza kusafiri hadi Sao Tome na Principe kwa wakati ufaao ili kushiriki mchuano wa jana jumapili wa mkondo wa kwanza. Shirikisho la CAF lilisema mchuano huo umeahirishwa hadi jumapili ijayo tarehe 15 baada ya Lesotho kukosa safari za ndege hadi taifa hilo la kisiwa kando ya pwani ya Afrika magharibi. Mkondo wa pili utasalia jinsi ulivyopangwa tarehe 22 mwezi huu wa januari. Kuanza kwa mechi za kufuzu kwa kinyang'anyiro cha mwaka ujao tayari kulikuwa kumetatizika kutokana na kujiondoa kwa Swaziland kabla ya mkondo wake wa kwanza dhidi ya Ushelisheli. Shirikisho la soka la Swaziland lilisema halingeweza kushiriki dimba hilo.

Huku bado ikiendelea kuteketea kutokana na matukio makuu yanayomhusisha mchezaji Luis Suarez na John Terry, soka ya uingereza inakabiliwa na kesi nyingine ya ubaguzi wa rangi baada ya mchezaji mweusi kudunishwa na mashabiki wakati wa mchuano wa kombe la FA. Hapo jana klabu ya Liverpool ilimwomba msamaha mchezaji beki wa timu ya Oldham Tom Adeyemi ambaye anadaiwa kutukanwa wakati wa mchuano wa jumamosi lakini ikajitenga na mshukiwa aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo. Katika taarifa yake, Liverpool imesisitiza kuwa vitendo vya mtu yeyote mmoja haviwawakilishi mashabiki wake.

Tukio hilo lilijiri baada ya mshambulizi wa Liverpool Luis Suarez kuanza kutumikia adhabu ya kupigwa marufuku ya mechi nane kwa kumbagua kwa misingi ya rangi beki wa Manchester United Patrice Evra. Na siyo nchini Uingereza tu kunakoshuhudiwa matukio ya ubaguzi wa rangi viwanjani….katika mchuano wa jana ambao uliishia sare ya bao moja baina ya Espanyol na Barcelona, baadhi ya mashabiki wa Espanyol waliziiga sauti za nyani kila wakati mchezaji wa Barcelona Dani Alves alipougusa mpira.

Baada ya kulipiza kisasi dhidi ya mahasimu wao wa mji wa Manchester hapo jana katika mchuano wa duru ya awamu ya tatu ya kombe la FA kwa kuifunga Manchester City mabao matatu kwa mawili, Manchester United imepangiwa kuchuana na Liverpool katika duru ya nne ya kombe hilo. Mchuano huo utakuwa na hisia tofauti kutokana na kesi ya ubaguzi wa rangi unaomhusisha Luis Suarez wa Liverpool ambaye yuko nje kwa mechi nane kama adhabu ya kumbagua Patrice Evra wa Man United.

Mashabiki wa Liverpool ambayo itaikaribisha Man United katika mchuano wa duru ya nne ya kombe la FA
Mashabiki wa Liverpool ambayo itaikaribisha Man United katika mchuano wa duru ya nne ya FAPicha: Pressefoto ULMER

Mchuano mwingine ambao huenda ukafufua madai ya kibaguzi ni kati ya QPR dhidi ya Chelsea ikiwa QPR itafuzu mchuano wa marudio dhidi ya MK Dons. Nahodha wa Chelsea John Terry anakabiliwa na shtaka la uhalifu baada ya kumtolea matamshi ya kibaguzi mlinzi wa QPR Anton Ferdinand. Terry atafikishwa mahakamani tarehe mosi mwezi ujao.

Tukiangalia soka ya hapa Ujerumani ni kuwa Rais mteule wa shirikisho la soka nchini Ujerumani DFB Wolfgang Niersbach anashinikiza juhudi za upatanishi baina ya kocha wa timu ya taifa Joachim Loew na nahodha wa zamani Michael Ballack. Uamuzi wa Loew wa kumtema Ballack kufuatia mechi za kombe la dunia mwaka 2010 ambazo nahodha huyo kwa wakati huo alikosa michuano hiyo kwa sababu ya jeraha ndio umekuwa kiini cha machungu hayo. Niersbach ambaye anatarajiwa kuchukua mahapa pa Theo Zwanziger kama rais wa shirikisho la soka la Ujerumani amesema kuwa shirikisho la DFB lina nia ya kutatua mzozo huo. Mshambulizi wa zamani wa Ujerumani Rudi Voeller ambaye sasa ni mkurugenzi wa spoti katika klabu anayochezea Ballack Bayer Leverkusen ameunga mkono juhudi za upatanishi zinazofanywa na Niersbach.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Josephat Charo