1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru Kenyatta ataka kesi ya ICC iakhirishwe

14 Februari 2013

Mawakili wa mgombea Kenyatta wameiomba mahakama ya icc The Hague kuahirisha kesi inayomkabili ya uhalifu dhidi ya ubinadamu wakiutuhumu upande wa uendeshaji mashataka kwa kuzuia ushahidi.

https://p.dw.com/p/17eAa
Mgombea urais Kenya Uhuru Kenyatta
Mgombea urais Kenya Uhuru KenyattaPicha: picture-alliance/dpa

Katika kikao maalum tarehe 14 Februari katika mahakama ya The hague ambacho ni cha mashauriano juu ya maandalizi ya kesi dhidi ya watuhumiwa wanne wa Kenya,mgombea urais kutoka muungano wa Jubilee Uhuru Kenyatta na aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura wanaitaka mahakamahiyo iiakhirishe kesi inayowakabili ya uhalifu dhidi ya ubinadamu iliyopangwa kuanza mwezi Aprili.

Watuhumiwa wahitaji muda kujiandaa

Watuhumiwa hao wawili wanasema wanahitaji muda wa kujiandaa kusimama kwenye kesi hiyo kutokana na kwamba upande wa mashtaka umejitokeza na ushahidi mpya.Uhuru Kenyatta kupitia  mawakili wake anasema anahitaji muda zaidi wa maandalizi katika kesi hiyo kwasababu upande wa mashataka uliamua kumbwaga shahidi muhimu na kwa maana hiyo Uhuru sasa anakabiliwa na kesi tofauti na ile  iliyotajwa mwanzo katika kikao cha kuthibitisha mashtaka yanayomkabili.

Mgombea mwenza wa Jubilee William Samoei Ruto
Mgombea mwenza wa Jubilee William Samoei RutoPicha: AP

Kwa upande mwingine wakili wa  aliyekuwa  mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura Karim Kahn amesema ni kiroja kwamba upande wa mashataka wa ICC umekuwa ukizuia kutoa ushahidi muhimu hadi dakika za mwisho jambo ambalo anadai litasababisha kesi hiyo ya mwezi Aprili kuendeshwa bila ya kuzingatia usawa.Kingine cha msingi ambacho mawakili wa Ruto na Uhuru Kenyatta walichokifikisha mbele ya kikao hicho ni kutaka kuhudhuria kesi ya Aprili kupitia njia ya Video.

Hata hivyo  jaji Sang Hyun Song amewataka  mawakili wa wanasiasa hao  kuandaa ombi rasmi kwa maandishi  linalozingatia sheria kufikia mwishoni mwa mwezi huu. Joshua Arap Sang na Francis Muthaura wakisikiliza mashauriano hayo wakiwa The Hague,Uhuru Kenyatta na William Ruto wameshiriki kikao hicho kwa njia ya Video wakiwa Nairobi.

Fatou Bensouda Mwendesha mashtaka mkuu wa icc
Fatou Bensouda Mwendesha mashtaka mkuu wa iccPicha: AFP/Getty Images

Shaka juu ya mashahidi wa ICC

Wakili wa Uhuru Kenyatta Steven Kay ameliambia jopo hilo la majaji watatu kwamba kwa jinsi ushahidi ulivyobadilika katika upande wa mashtaka wa ICC unaoongozwa na Fatou Bensouda inamlazimu kuomba kesi hiyo isogezwe mbele.Aidha sula jingine lililoibuka kutoka upande wa washtakiwa ni kudai kutambulishwa mashahidi wa upande wa icc lakini jaji amesema hilo linaweza tu kufanyika baada ya vikwazo vya kiusalama kutatuliwa na hatimae orodha ya mashahidi wa icc kutambulishwa tarehe 18 ya Februari.

Itakumbukwa kwamba aliyekuwa mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Luis Moreno Ocampo alianzisha uchunguzi wa ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya mnamo mwezi Marchi 2010 na mwaka mmoja baadae mahakama hiyo ikawahoji wakenya sita wakiwemo Ruto na Kenyatta ambao wanatuhumiwa na waendesha mashtaka wa ICC  kuwa vinara wa ghasia hizo, wakati kesi za maafisa wengine wawili wa serikali,Henry Kosgei na aliyekuwa kamishna wa polisi Hussein Ali zikatupiliwa mbali.

Mwaka 2012 mahakama ya ICC ikafikia uamuzi kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa kuwafungulia kesi juu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu wanne waliobakia Kenyatta Ruto Muthaura na Sang.Majaji wanaohusika na kikao cha leo cha mashauriano juu ya maandalizi ya kesi itakayosikilizwa mwezi Aprili,wanatarajiwa kutoa uamuzi wao baadae kuhusu ombi la kutaka kesi hiyo isogezwe mbele.

Ghasia za baada ya uchaguzi Kenya 2007
Ghasia za baada ya uchaguzi Kenya 2007Picha: AFP/Getty Images

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo.