1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa habari bado ni ndoto Syria

3 Mei 2011

Wakati Syria ilipoondosha hali ya hatari iliyodumu miaka 50 pamoja na marufuku ya mawasiliano kupitia mitandao hivi karibuni, ilitarajiwa kuwa mwanzo wa mageuzi. Lakini hiyo ilikuwa ndoto tu, maana ukandamizaji ungalipo.

https://p.dw.com/p/117l0
Magazeti nchini Syria
Magazeti nchini SyriaPicha: Mona Naggar

Vitendo vya ukandamizaji na mateso vimezidi tangu wimbi la kudai mageuzi katika nchi za Kiarabu kufika nchini Syria na serikali ya chama cha Baath kuingiwa na wasiwasi.

Idadi ya watu wanaojitokeza barabarani kuipinga serikali inaongezeka. Viongozi wa nchi hiyo wanaikabili hali hiyo kwa kutumia mabavu, kuwatia ndani wapinzani wake na kuweka vikwazo dhidi ya vyombo vya habari.

Skeyes ni kituo kinachotetea uhuru wa vyombo vya habari na utamaduni kipo mjini Beirut na ambacho kila mwezi hutoa orodha ya vitendo vinavyokiuka uhuru wa vyombo vya habari nchini Syria.

Saad Kiwan, anayefanya kazi katika kituo hicho, anasema nchini Syria wanashuhudia hali iliyo ngumu sana kwa waandishi wa habari, ingawa hiyo ni hali iliyokuwepo hata kabla ya matukio ya hivi sasa.

Mwandamanaji wa Syria akiipiga picha ya Rais wa nchi hiyo, Bashar al-Assad, kwa kiatu
Mwandamanaji wa Syria akiipiga picha ya Rais wa nchi hiyo, Bashar al-Assad, kwa kiatuPicha: AP

"Vyombo vya habari haviwezi kufanya kazi yake. Wakati wa utafiti wetu, wafanyakazi wanapaswa kufanya kazi kwa siri, wakati wanapokusanya habari kuhusu watu waliokamatwa au kuhusu kesi za waandishi wa habari au wanaharakati wa haki za binadamu." Anasema Kiwan.

Katika ripoti iliyopita, kituo hicho kiliarifu kuhusu Wassim Hassan na Khalid al-Mubarak waliokamatwa. Vijana hao wawili ni waandishi wa blog na wamewekwa jela tangu katikati ya mwezi Aprili mwaka huu.

Mwengine ni Mahmoud Issa, ambaye alikamatwa na vikosi vya usalama, baada ya mwanaharakati huyo wa haki za binadamu kuhojiwa na Al-Jazeera. Saad Kiwan anakisia kuwa idadi ya waandishi wa habari, wanablogi na waandishi vitabu waliozuiliwa nchini humo ni takriban 300.

Hata vituo vya televisheni vya Al-Arabiya na Al-Jazeera vimeonywa kuhusiana na ripoti za maandamano nchini Syria.

Mkuu wa tawi la kituo cha Skeyes katika mji mkuu wa Syria, Damascus, Mazen Darwish, anasema kuwa mada zinazoruhusiwa kuripotiwa katika vyombo vya habari hutegemea hali ya kisiasa ndani ya nchi na katika kanda hiyo.

Wakati huu wa machafuko, vyombo vya habari vya taifa na binafsi vinaamriwa kuachilia mbali ripoti zote za ukosoaji, likiwemo suala la ufisadi.

Kila mwaka, Syria inashika nafasi za mwisho katika orodha ya kimataifa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, inayotolewa na Shirika la Waandishi wa Habari wasio na Mipaka.

Mwandishi: Mona Naggar/ZPR
Tafsiri: Prema Martin
Mhariri: Josephat Charo