1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa kujieleza na kukusanyika Rwanda wamulikwa

Admin.WagnerD28 Januari 2014

Rekodi ya Rwanda ya kuwafungulia mashitaka wanasiasa wanaomkashifu Rais wa nchi hiyo Paul Kagame inaogofya na kuwatia mzizimo wapinzani na wanaharakati wa haki za binadaamu nchini humo

https://p.dw.com/p/1AyIn
Picha: Reuters

Kagame ambaye alikuwa kiongozi wa waasi na baadaye amekuwa kiongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka 1994, amesifiwa sana kwa kufanya mageuzi yenye tija kubwa katika sekta ya uchumi wa Rwanda na pia kwa kuwa katika mstari wa mbele kutuma wanajeshi wake kulinda amani katika nchi nyingine zinazokumbwa na mizozo barani Afrika.

Lakini wapinzani wake na wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu wanamshutumu kwa kuukandamiza uhuru wa kuendeleza ajenda za kisiasa na vyombo vya habari, tuhuma ambazo serikali yake bila shaka imezikanusha.

Wanasiasa wenye maoni tofauti matatani

Mwandishi maalum wa Umoja wa Mataifa, Maina Kiai, amesema wanasiasa ambao hawakubaliani na siasa za Kagame, wanajikuta matatani kisheria mara kwa mara wakishitakiwa kwa kuhusika katika mauaji ya halaiki na kuhusishwa na makundi haramu. Wengine wanaokihama chama tawala cha Rwandan Patriotic Front, RPF, huwa wanatafutiwa sababu na kufunguliwa mashitaka ya ufisadi.

Mwanasiasa wa upinzani Rwanda Victoire Ingabire anayetumikia kifungo cha jela
Mwanasiasa wa upinzani Rwanda Victoire Ingabire anayetumikia kifungo cha jelaPicha: dapd

Marekani siku kumi zilizopita ilisema inatiwa wasiwasi na vitisho vilivyotolewa na Rais Kagame dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa baada ya mmoja wa wakosoaji wa utawala wake aliyetorokea uhamishoni kupatikana ameuawa katika chumba cha hoteli moja nchini Afrika Kusini.

Kagame na utawala wake umekanusha vikali kuhusika katika kifo cha Patrick Karegeya ambaye mwili wake ulipatakina katika hoteli moja ya kifahari mjini Johannesburg tarehe moja mwezi huu ukiwa na alama za kunyongwa.

Je uhuru wa kisiasa utaheshimika?

Kiai amesifu juhudi zilizofanywa na Rwanda katika kuimarisha miundo mbinu na kuhakikisha uthabiti wa taifa tangu mauaji ya halaiki yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu laki nane mwaka 1994, lakini amesema wanasiasa wa upinzani wanapaswa kuwa na uhuru wa kunadi sera zao na ajenda zao bila uoga.

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Reuters

Mwezi Desemba mwaka jana, mahakama ya juu ya Rwanda iliongeza kifungo cha jela cha mwanasiasa wa upinzani Victoire Ingabire kutoka miaka minane hadi 15 baada ya kujaribu kupinga hukumu yake ya awali kwa mashitaka ya kuihujumu serikali na kuyadunisha mauaji ya halaiki ya mwaka 1994.

Akizungumza na wanahabari baada ya ziara ya wiki nzima ya kutathmini hali ya uhuru wa kisiasa wa vyombo vya habari na wa raia kukusanyika Rwanda, Kiai amesema hakuna nafasi ya watu kueleza maoni yao ambayo hayaendani na misimao na mitazamo ya serikali.

Watu ambao wamejaribu kusimama na kuupinga utawala wa Kagame ambao umekuwa madarakani tangu 1994 wamenyanyaswa, kufungwa, wengine wamepotea katika mazingira ya kutatanisha na wengine wamepoteza maisha yao.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/ap

Mhariri: Josephat Charo