1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa wanahabari bado ni tatizo-CPJ

25 Aprili 2017

Kamati ya kuwalinda wanahabari CPJ imechapisha ripoti yake ya kila mwaka Jumanne, iliyopewa kichwa cha maneno, Sura mpya ya kuchuja habari''The New Face Of Censorship".

https://p.dw.com/p/2btda
China Hong Kong Media Protest
Picha: Getty Images/AFP/P. Lopez

Ripoti hiyo inaangazia jinsi vyombo vya habari vinavyoshambuliwa na serikali tofauti kote duniani. Katika kanda ya Afrika Mashariki, kumeshuhudiwa visa kadhaa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambapo wanahabari na vyombo vya habari vimenyimwa haki ya kutekeleza wajibu wao na katika baadhi ya visa, wanahabari wameishia kufariki dunia.    

Nchini Tanzania tarehe 14 ya mwezi Disemba 2016 polisi ilivamia afisi za wavuti wa Jamii Forum mjini Dar es Salaam na kumkamata mwanzilishi mwenza wa wavuti huo Maxence Melo. Wavuti huo ni maarufu sana Afrika Mashariki na hutoa nafasi kwa mijadala kuhusiana na masuala mengi yakiwemo ufisadi na utepetevu wa serikali.

CPJ inasema katika ripoti yake kwamba rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli amechukua hatua kadhaa kuvifunga mdomo vyombo vya habari tangu kuchaguliwa kwake Oktoba mwaka 2015.

Polisi walimvamia na kumtishia mwanahabari wa The Standard

Mwezi Agosti mwaka 2016 waziri wa zamani wa mawasiliano nchini Tanzania Nape Nnauye aliamrisha kufungwa kwa vituo viwili vya redio Radio Five na Magic FM, akisema kwamba vituo hivyo vilipeperusha matangazo ambayo yangewachochea wananchi na kuvuruga amani.

Tansania John Pombe Magufuli Präsident
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli anashutumiwa kwa kuvifunga mdomo vyombo vya habari nchini humoPicha: DW/S. Michael

Nchini Kenya CPJ inasema, tarehe 22 ya mwezi Machi 2017 mwanahabari wa gazeti la The Standard daily Isaiah Gwengi alitishiwa na kuvamiwa na polisi nchini humo. Kulingana na mwanahabari huyo, polisi walimzuia alipokuwa anarudi nyumbani katika kijiji cha Usenge, karibu na ziwa Victoria.

"Waliniambia watahakikisha kwamba nimefariki dunia, na kwamba siwezi kupigana nao kwa kutumia kalamu na karatasi na iwapo nataka nipigane nao basi ninunue bunduki," alisema Gwengi.

Tarehe 15 Aprili 2016 mwandishi wa gaeziti la The Nairobian alikamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa kile alichosema, polisi walimuwekea sababu tofauti za kukamatwa kwake huku mmoja akisema alikamatwa baada ya kuandika taarifa kuhusiana na mzozo wa ardhi baina ya mfanyabiashara mmoja na mtu anayehusiana naye, na afisa mwengine wa polisi akimwambia alikamatwa kwa kosa la kutumia visivyo kifaa cha mawasiliano.

Nchini Uganda mwanahabari wa NTV alikamatwa kwa kumsifu mtu aliyemkashifu rais Museveni

Huko huko Kenya, polisi walimkamata na kumzuia mwanahabari ambaye ni mwanablogu Yassin Juma tarehe 23 Januari 2017 baada ya kuchapisha picha za shambulizi la kigaidi la Al Shabaab katika kambi ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Tansania Polizei attackiert einen Journalisten in Dar es Salaam
Polisi Dar es Salaam, Tanzania wakimvamia mwanahabariPicha: Article19-East Africa

Nchini Uganda Aprili 8 mwaka 2017, watu wasiojulikana katika mitaa ya mji mkuu Kampala, walimvamia Gertrude Uwitware, mwanahabari wa masuala ya afya katika kituo cha televisheni cha kibinafsi cha NTV. Uwitware aliiambia CPJ alikamatwa kutokana na hatua yake ya kuandika taarifa katika blogu yake ya kumsifu Stella Nyanzi, msomi aliyefungwa jela kutokana na maandishi yake katika mtandao wa kijamii wa Facebook ya kumkashifu rais Yoweri Museveni na Mkewe ambaye ni waziri wa elimu.

Huko huko nchini Uganda, polisi ilimkamata mwanahabari wa kituo cha televisheni cha Kenya KTN Joy Doreen Biira ambaye ni raia wa Uganda, baada ya mwanahabari huyo kuripoti kuhusu mapambano ya polisi na walinzi wa ufalme wa Baganda.

Nchini Rwanda CPJ inasema utafiti wake unaonesha mwaka 2010 magazeti mawili Umuseso na Umuvuguzi yalifungwa nchini humo na kaimu mhariri Jean Leonard Rugambage, akauwawa kwa kupigwa risasi nje ya nyumba yake mjini Kigali. Wanahabari nchini humo walisema kwamba Rugambage aliwaambia alikuwa anajitayarisha kwenda uhamishoni baada ya kufuatiliwa na watu asiowajua na kupokea vitisho kupitia simu.

Mwandishi: Jacob Safari/CPJ

Mhariri: Yusuf Saumu