1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa ni imara

9 Julai 2012

Miaka 50 ya uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa,uchaguzi nchini Libya na jinsi ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa fedha barani Ulaya ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

https://p.dw.com/p/15U0T
Kansela Merkel na rais Hollande katika sherehe za Reims,kuadhimisha miaka 50 ya uhusiano kati ya Ujerumani na UfaransaPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini na uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa ambao umekamilisaha miaka 50 tangu uliopoanzishwa mnamo mwaka 1962.Gazeti la "Allgemeine Zeitung" linaandika:Maarifa kwamba Ulaya inafaidika zaidi Ujerumani na Ufaransa zinapoungana kuliko zinapotengana,yalipewa umuhimu mkubwa zaidi kuliko kumbu kumbu za maafa yaliyoshuhudiwa kwa mara ya mwisho,wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.Charles de Gaule na Konrad Adenauer waliamua kuifuata kwa dhati njia hiyo kwa namna ambayo uhusiano waliouanzisha mpaka leo ni madhubuti.Hata kama kila masika ina mvua zake.Francois Hollande pia,kama alivyokuwa mlezi wake wa kisiasa Francois Mitterand,hahofii kuichukulia Ujerumani kama mshirika wa kibiashara kwa masilahi ya ndani.Mshirika wa kibiashara ambae ikilazimika anaweza hata kugeuzwa habusi wa kiuchumi.Lakini sisa kama hiyo haitakuwa na faida kwa mustakbal wa Ulaya ambao tokea hapo ni tete.

Gazeti la "Dresdner Neueste Nachrichten" linatathmini jinsi viongozi wa nchi hizi mbili walivyokuwa katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 kule kule ambako makubaliano ya urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa yalitiwa saini mwaka 1962.Gazeti linaendelea kuandika:Hawakuwa na bashasha sana, Francois Hollande na Angela Merkel walipofika jana katika kijiji cha Champagne huko Reims.Hata hivyo viongozi hao hawakuwa na kazi ya kuondowa hisia za uadui kama ilivyokuwa wakati wa enzi za Charles de Gaule na Konrad Adenauer.Uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa ni imara.Hata hivyo Merkel na Hollande bado hawajafikia ile daraja ya uhusiano uliokuwepo kati ya kansela Angela Merkel na kiongozi wa zamani wa kasri ya Elysee-Nicolas Sarkozy.Lakini viongozi wote hawa wawili ni werevu wa kutosha kuweza kutambua kwamba mhimili wa Ujerumani na Ufaransa ni muhimu kwa Ulaya yenye nguvu na utulivu wa sarafu ya Euro.

SNB Schweizer Nationalbank
EuroPicha: picture-alliance/dpa

Utulivu wa sarafu ya Euro ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na gazeti la "Saabrücker Zeitung" linaloandika:Mnamo miaka inayokuja,hali itazidi kuwa ngumu barani ulaya,katika kusaka ufumbuzi wa matatizo ya fedha. Ndio maana panahitajika kiongozi mwenye ujuzi kuongoza kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro. Wolfgang Schäuble ndie anaefaa kukabidhiwa wadhifa huo. Lakini baadhi ya wanachama wa Umoja wa Ulaya, wakitanguliwa na Ufaransa, wanataka kulipiza kisasi dhidi ya madaraka na uamuzi wa upande mmoja wa kansela Angela Merkel. Ndio maana mhula wa wadhifa huo utagawanywa mara mbili. Si ufumbuzi wa maana na hautakuwa na faida kwa ulaya.

Na hatimae gazeti la "Der Neue Tag" limechambua uchaguzi nchini Libya na kuendelea kuandika:Yawezekana kwamba Libya ina njia ndefu ya kufuata hadi kuifikia demokrasia. Yawezekana lakini pia kwamba na sisi pia tunafuata njia sio kabisa: Wajerumani ambao ni wavivu wa kupiga kura,wanabidi watanabahi wanapoona jinsi walibya wanavyosherehekea,jinsi haki ya kupiga kura ilivyo tunu.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef