1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa aina mpya na Urusi

Maja Dreyer16 Mei 2007

Suala moja linalozingatiwa leo hii ni ziara za mawaziri wa nje wa Ujerumani na Marekani, Bw. Steinmeier na Bi Rice, nchini Urusi. Matokeo ya mazungumzo yao ni yapi?

https://p.dw.com/p/CHSw

Kwanza ni gazeti la “Neue Osnabrücker”:

“Shinikizo limepunguzwa. Ziara za mawaziri wa nje wa Ujerumani na Marekani, kwa upande mmoja, zilisaidia mkutano kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya ufanikiwe na, kwa upande mwingine, mvutano kati ya Marekani na Urusi juu ya mitambo ya kufyetua makombora na vile vile juu ya hali ya haki za binadamu umetulizwa kwa kiasi. Lakini pengo kati ya Urusi na nchi za Magharibi bado lipo.”

Mahusiano na Urusi yamebadilika, linaandika gazeti la “Berliner Zeitung” katika uchambuzi wake. Sera hizo mpya ni matokeo ya kuangalia nyuma sera za miaka ishirini iliyopita, na gazeti hilo linaendelea:

“Katika kuthamini gharama na mapato ya muda huu, Urusi imeona kwamba baada ya enzi ya Jelzin ya kukubaliana, na enzi ya Putin ya ushirikiano na upande wa Magharibi katika vita dhidi ya ugaidi, basi majukumu ni mengi lakini faida ni ndogo. Kwa hivyo, kuna sababu za kutosha kuachana na majukumu hayo ikiwa Urusi itanufaika. Wakati umewadia sasa. Urusi ina nguvu tena, na kisiasa ina uwezo wa kutekeleza maslahi yake. Sasa inabidi kuendelea na mazungumzo na Urusi. Lakini wakati huo huo, nchi za Ulaya zinapaswa kufikiria juu ya mkakati mpya wa uhusiano mpya na Urusi.”

Na suala la pili ambalo linagonga vichwa vya habari humu nchini leo hii, ni makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo marefu kati ya vyama tawala vya Ujerumani kuhusu sera za familia. Baada ya miaka mitano, wazazi watakuwa na haki ya kupewa nafasi katika shule za chekechea kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitatu. Pale vyama havikuweza kukubaliana ni juu kima cha chini cha mshahara hapa Ujerumani. Kinachojadiliwa leo ni mustakabali wa muungano huo wa kisiasa kati ya vyama vya Christian Democrats, CDU, na Social Democrats, SPD. Gazeti la Kölnische Rundschau linafahamu shida ya kuafikiana katika serikali hii:

“Bila shaka, kuna sababu za kulalamika juu ya mivutano mingi katika serikali hii ya mseto. Ukosoaji fulani si sawa. Lakini wengi wanasahau kwamba ni vigumu sana kwa vyama hivi viwilil ambavyo sera zao ni tofauti sana, kugundua hoja zinazokubaliwa na wote. Kwa hivyo kuna sababu ya kusifu maafikiano yaliyoapatikana kuhusu suala muhimu sana la kijamii.”

Ni gazeti la “Kölnische Rundschau”. Mhariri wa “Stuttgarter Zeitung” lakini ana wasiwasi juu ya mustakabali wa muungano huo wa kisiasa. Ameandika:

“Serikali hii itaendelea vipi? Kuhusu suala la kima cha chini cha mshahara kuna tofauti kubwa ya kiitikadi. Ikiwa chama cha Christian Democrats hakitakubali hoja za Social Democrats, basi hili litakuwa suala muhimu katika kampeni ijayo ya uchaguzi. Inaonekana kama mkakati wa kisiasa ni muhimu kuliko maisha ya mamia ya Wajerumani ambao wana shida kubwa kutekeleza matakwa yao ya kila siku kwa sababu mishahara yao ni midogo mno – licha ya kwamba wanafanya kazi siku nzima. Hadi sasa, bado nusu ya kipindi cha utawala hakijafikiwa, na tayari sasa vyama hivi viwili vikubwa vimeshindwa kugundua nia ya pamoja.”