1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa China na Bara la Afrika

P.Martin - (RTRE)10 Februari 2009

Rais wa China Hu Jintao anafanya ziara ya siku 8 nchini Saudi Arabia, Mali,Senegal,Tanzania na Mauritius.Hiyo ni ziara yake ya kwanza ya kigeni mwaka huu wa 2009.

https://p.dw.com/p/Gr3d
Chinese President Hu Jintao speaks during a group interview with journalists in Beijing Friday, Aug. 1, 2008. (AP Photo/Rafael Wober)
Rais wa China Hu Jintao.Picha: AP

Ni matumaini ya China kuwa ziara yake barani Afrika itaonyesha kwamba ushurikiano wake na bara hilo hauhusiki tu na maslahi ya kujipatia mafuta,madini na mikataba.Mbali na Saudi Arabia iliyo na utajiri mkubwa wa mafuta,ziara ya Rais Hu Jintao kuanzia tarehe 10 hadi 17 mwezi wa Februari,inampeleka katika nchi nne za Kiafrika ambazo hazina utajiri mkubwa wa mafuta au raslimali nyingine.Kwa hivyo uhusiano wa China na Afrika hauzingatii raslimali tu na hasa wakati wa ziara hii.Hayo amesema Naibu Waziri wa mambo ya Nje wa China Zhai Jun alipozungumza na waandishi wa habari mjini Beijing.Akaongezea kuwa China ina urafiki wa dhati na ushirikiano mzuri na nchi zote nne zitakazotembelewa barani Afrika.

Uhusiano wa China na Afrika unaozidi kuimarika umesababisha wasiwasi miongoni mwa wafadhili wa magharibi wakihofia kuwa Beijing inadharau ukiukaji wa haki za binadamu ili kuweza kuendelea na biashara yake hasa nchini Sudan.China,imetumia mabilioni ya dola barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni kutafuta raslimali kwa ajili ya uchumi wake unaoinukia.Vile vile sasa ni mfadhili mkubwa wa misaada inayotolewa kwa nchi masikini kabisa barani Afrika.China inasema,msaada wake hauna masharti na biashara inayofanywa na nchi za Kiafrika husaidia kuendeleza uchumi wa nchi hizo.

Kwenye mkutano wa kilele wa nchi za Kiafrika ulioitishwa na China katika mwaka 2006 mjini Beijing,China na Bara la Afrika zilitia saini mapatano 16 yenye thamani ya dola bilioni 1.9.Baada ya mikataba hiyo kutiwa saini kati ya makampuni 12 ya Kichina na serikali na makampuni ya Kiafrika 11,Rais Hu aliahidi kutoa mikopo yenye thamani ya dola bilioni 5 na vile vile kuongeza maradufu msaada wake ifikapo mwaka 2009.Katika mwaka 2008 biashara iliyofanywa kati ya China na nchi za Kiafrika,ilifikia dola bilioni 106.Kulinganishwa na mwaka 2007 huo ni muongezeko wa asilimia 45.

Ziara hii ya Hu barani Afrika ilitanguliwa na ziara ya Waziri wa Biashara wa China Chen Deming nchini Kenya,Zambia na Angola mwezi uliopita.Naibu Waziri Zhai amesema,Rais Hu atatangaza msaada mpya kwa nchi za Kiafrika,lakini alikataa kueleza zaidi.Vile vile hakutaka kusema mikataba gani ya mafuta itatiwa saini pamoja na Saudi Arabia.Ushirikiano katika sekta hiyo ni sehemu muhimu ya uhusiano wa nchi hizo mbili.