1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Marekani na Israel mashakani

Mjahida 26 Februari 2015

Hatua ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ya kukosoa juhudi za kupata makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, kumezusha hisia kali na uharibifu wa ushirikiano katika mahusiano ya Israel na Marekani.

https://p.dw.com/p/1Ei71
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Washirika hao wawili Marekani na Israel wanaendelea kutupiana maneno wakati ikiwa imesalia siku sita tu kabla ya waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kutoa hotuba yake katika bunge la Marekani wiki ijayo, akiangazia vitisho vya nyuklia kutoka Iran.

Vuta nikuvute ilianza wakati Benjamin Netanyahu alipoyatuhumu mataifa yalio na nguvu duniani kwa kutelekeza ahadi ya kuizuwiya Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

“Naiheshimu ikulu ya Marekani na rais wa Marekani Barrack Obama lakini ni jukumu langu kufanya kila niwezalo ili kuhakikisha usalama wa watu wa Israel” alisema Netanyahu kabla ya kuondoka kwenda Washington anakotarajiwa kutoa hotuba yake wiki ijayo siku ya Jumanne.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/B. Ratner

Lengo la Netanyahu ni moja tu kujaribu kuyasambaratisha mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yanayoongozwa na Marekani, hata kama hali hiyo inaweza kuhatarisha kuvunjika kwa mahusiano yake na Rais Obama. Waziri Mkuu huyo wa Israel anahofia mpango huo ambao upo katika hatua zake za mwisho za majadiliano unaweza kutoa nafasi kwa Iran kuomba kuwa na silaha za nyuklia baada ya muda wa kuizuwiya kufanya hivyo kukamilika.

John Kerry asema huenda Netanyahu akawa na maoni ambayo si sawa

Hata hivyo Waziri wa mambo ya nchi za nje wa MarekaniJohn Kerry ambaye amehusika katika mazungumzo ya kimataifa na Iran juu ya mpango wake wa nyuklia amesema Netanyahu huenda akawa amekosea.

"Sera yetu ni kwamba Iran haitopata silaha za nyuklia, Mtu yeyote anaekimbia huku na kule akisema kwamba hawapendi makubaliano, au hiki au kile, hajui makubaliano ni gani. Hakuna makubaliano yoyote kwa sasa na natoa tahadhari kwa watu kusubiri kuona majadiliano yatafikia wapi,” alisema John Kerry.

Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Getty Images/J. Sullivan

Kwa upande wake mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Susan Rice ameielezea hotuba ya Nentanyahu kama mkakati wa kuvunja mahusiano ya Marekani na Israel. Aidha rais Obama amekataa kuonana na Waziri Mkuu Netanyahu wakati wa ziara yake hiyo huku wademokrats wakiapa kutohudhuria hotuba hiyo. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Kerry pia hatokuwepo wakati wa ziara ya Netanyahu nchini humo.

Wachambuzi wanasema hii inatoa ishara kwamba Netanyahu si mgombea wanayempendelea katika uchaguzi wa Israel unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 mwezi ujao.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman