1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kuamua kushiriki mapambano dhidi ya IS

Admin.WagnerD2 Desemba 2015

Bunge la Uingereza hii leo linatarajia kupiga kura kuiruhusu nchi yao kujiunga na mapambano dhidi ya kundi la dola la kiisilamu la IS nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1HFkW
Russland Syrien Militärhilfe
Picha: Reuters/Ministry of Defence of the Russian Federation

Waziri mkuu wa Uingereza , David Cameron ambaye ari yake ya kuliangamiza kundi hilo la dola la kiisilamu imeongezeka zaidi hasa baada ya mashambulizi ya mjini Paris anatarajiwa kuongoza mjadala bungeni unaotarajiwa kuchukua zaidi ya saa kumi katika kuelekea upigaji kura huo.

Mawaziri nchi humo wanaimani kwamba wabunge watapiga kura ya ndiyo kuunga mkono hatua hiyo hali ambayo inaashiria kuwa ndege za kijeshi za Uingereza zitaanza mashambulizi kulilenga kundi hilo la dola la kiisilamu huko nchini Syria kabla ya kufikia mwisho wa juma hili.

Cameron amesisitiza ya kuwa hatua za kijeshi zinahitajika sasa ili kuzuia mashambulizi kama yale ya yaliyoua watu 130 mjini Paris mwezi uliopita, lakini pia akiongeza kuwa hatua hiyo itaenda sambamba na juhudi za kidiplomasia zinazoendelea sasa katika kushughulkikia mgogoro wa Syria.

" Nitajitahidi kujenga hoja na nina imani kuwa wabunge wengi kutoka katika vyama vyote wataniunga mkono " alisema waziri mkuu Cameron katika kuelekea kura hiyo:

Hata hivyo baadhi ya wataalamu wa masuala ya kisiasa na ya kivita, wanasema wabunge kadhaa na raia wa kawaida wanaonekana kuwa na mashaka. Makundi ya watu wanaopinga mambo yanayohusiana vita tayari wameandamana kuonyesha kutounga mkono hatua hiyo.

Baadhi ya wachambuzi wanauona hatua hii ya uingereza kutaka kushirika katika kampeni dhidi ya kundi hilo la dola la kiisilamu kama hatua moja wapo ya kuwaunga mkono bega kwa bega washirika wake ambao ni mataifa ya Marekani na Ufaransa.

Syrien Syrische Armee
Jeshi la SyriaPicha: Getty Images/AFP/Y. Karwashan

" Cameron kwa sasa anaona ni lazima aiunge mkono Ufaransa katika kipindi hiki inachokabiliana na tatazo la ugaidi " alisema Ben Berry ambaye ni mmoja wa washauri katika siasa za kimataifa.

Tayari Uingereza imekuwa ikishiriki katika mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la dola la kiisilamu nchini Iraq kampeni ambayo ilianza tangu mwaka jana.

Aidha inaarifiwa pia kuwa Uingereza imeombwa nawashirika wake yakiwemo mataifa ya Ufaransa na Marekani kujiunga kikamlifu katika kampeni hiyo ya mashambulizi dhidi ya kundi hilo la dola la kiisilamu.

Tayari kumekuwepo na maandamanao nchini humo kupinga hatua ya kivita dhidi ya kundi hilo la dola la kiisilamu kama anavyosema mmmoja wa watu walioshiriki katika maandamano hayo

Chama cha Labour chagawanyika kuhusiana na hatua

Hatua hii ya Cameron inakuja mnamo wakati chama kikuu cha upinzani cha Labour nchini humo kikiwapa uhuru wa kuamua wabunge wa chama hicho katika kuunga mkono au kutounga mkono uamuzi huo pasipo shinikizo lolote kutokana na msimamo wa kiongozi mkuu wa chama cha Labor Jeremy Corbyn anayeonekana kupinga hatua hiyo .

" Tunataka kuwaua watu nchini mwao kwa kutumia mabomu yetu , tafadhali pigeni kura ya kutounga mkono hatua hii ya serikali dhidi ya mashambulizi ya nchini Syria" alisema kiongozi huyo wa chama cha Labor

Hata hivyo hatua hii ya kutopata shinikizo kutoka katika chama chao inaonyesha kuwa wabunge wa chama cha Labour ambao wanataka hatua za kijeshi zichukuliwe dhidi ya kundi hilo la dola la kiisilamu watapiga kura ya ndiyo hali ambayo inaonesha kuwa waziri mkuu Cameron atapata ushindi mkubwa katika azima yake hiyo.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri :Gakuba Daniel