1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza itawapokea watoto wa msitu wa Calais

Oumilkheir Hamidou
11 Oktoba 2016

Uingereza itatekeleza ahadi ya kuwapokea watoto wote wanaoishi peke yao katika kambi ya wakimbizi ya Calais na ambao familia zao wanaishi Uingereza. Habari hizo zimetangazwa na waziri wa mambo ya ndani Amber Rudd.

https://p.dw.com/p/2R6eX
Maandamano dhidi ya kukongolewa kambi za waakimbizi za Calais
Maandamano dhidi ya kukongolewa kambi za waakimbizi za CalaisPicha: Getty Images/AFP/P. Huguen

 

Bibi Amber Rudd ameongeza kusema kwamba wamepiga hatua muhimu mbele  alipokutana na waziri mwenzake wa Ufaransa Bernard Caseneuve mjini London ambapo walizungumzia kadhia ya wahamiaji wa Calais."Serikali ya Uingereza imeahidi kuwaingiza watoto hao wanaoweza kudhurika, katika mfumo wa sheria za uhamiaji na kuhakikisha wale wote wenye familia zao nchini Uingereza wanaletwa huku kuambatana na mwongozo wa makubaliano ya Dublin" amesema bibi Amber Rudd bungeni mjini London."Tumepiga hatua muhimu mbele lakini bado kuna mengi ya kufanya"ameongeza kusema.

Kwa mujibu wa makubaliano ya Dublin,wanaoomba kinga ya ukimbizi wanabidi watume maombi yao katika nchi ya kwanza walikoingia,lakini maombi yao yanaweza kuzingatiwa katika nchi nyengine ikiwa kwa mfano jamaa zao wanakutikana katika nchi hiyo.

Watoto zaidi ya 170 watabidi kukubaliwa Uingereza

Senyenge zinalizunguka eneo la msitu wa Calais kuwazuwia wakimbizi wasiingie Uingereza
Senyenge zinalizunguka eneo la msitu wa Calais kuwazuwia wakimbizi wasiingie UingerezaPicha: DW/E. Bryant

Kabla ya mazungumzo hayo,waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Caseneuve alisema "mamia kadhaa ya watoto wanaoishi peke yao toka jumla ya watoto 800 walioko katika msitu wa Calais wana familia zao au jamaa zao Uingereza. Ripoti ya shirika la msalaba mwekundu la Uingereza iliyochapishwa mwishoni mwa wiki inazungumzia kuhusu watoto 178 wenye jamaa zao Uingereza.

Katika taarifa ya pamoja,Bernard Caseneuve na Amber Rudd wamesema wamepania kuona  juhudi za kuzikongoa kambi za Calais zinafanikiwa.Tarehe halisi ya kukongolewa kambi hizo zinazojulikana kama kambi za msitu wa Calais haijatangazwa,lakini serikali ya Ufaransa imesema inapanga kuzifyeka kambi hizo hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu. Kundi la mwanzo la wahamiaji wataanza kuondoshwa wiki ijayo.

Licha ya senyenge weaklimbizi wanaparamia
Licha ya senyenge waklimbizi wanaparamiaPicha: picture-alliance/AA/M. Yalcin

Mashirika ya misaada ya kiutu yanapinga kukongolewa "Msitu wa Calais"

Mashirika ya misaada ya kiutu yanayowasaidia wakimbizi hao wa Calais,mji wa bandari,kaskazini mwa Ufaransa,yanakopita malori yanayoelekea Uingereza yanapinga mpango wa serikali ya Ufaransa wa kuivunja kambi hiyo. Kabla ya mkutano wao katika wizara ya mambo ya ndani baadae hii leo wawakilishi wa shirika linalowahudumia watu wasiokuwa na makao,Emmaus wametoa wito wa kuakhirishwa mipango ya kuzifunga kambi hizo wakihoji masharti yote hayakutekelezwa kuhakikisha opereshini hizo zinafanyika ipasavyo. Jumla ya wahamiaji 10.000 wanaishi katika hali duni kabisa katika kambi hizo za msituni za Calais.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Khelef