1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yampongeza Karzai

Kabogo Grace Patricia19 Novemba 2009

Pongezi hizo zimetolewa leo baada ya Rais Karzai kuapishwa

https://p.dw.com/p/KbDR
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan akikagua gwaride la jeshi baada ya kuapishwa.Picha: picture-alliance/ dpa

Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown amempongeza Rais Hamid Karzai wa Afghanistan kwa kuapishwa kwake kwa awamu ya pili ya miaka mitano madarakani, lakini amemtaka kiongozi huyo sasa atekeleze wajibu wake ipasavyo kwa maslahi ya Wa-Afghani wote.

Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, amesema Bwana Brown aliisifia hotuba iliyotolewa leo asubuhi na Rais Karzai baada ya kuapishwa akisema inatoa matumaini kwa wananchi wa Afghanistan, ambapo imesisitiza juu ya suala la kukabiliana na rushwa, huku akiwakaribisha wapinzani wake wakuu katika serikali atakayoiunda ya umoja wa kitaifa. Kwa mujibu wa msemaji huyo, Bwana Brown alisisitiza kuwa kuna matarajio makubwa katika kipindi hiki cha pili cha uongozi wa Rais Karzai katika sura ya jumuiya ya kimataifa na kwamba watafanya kazi kwa kushirikiana na Rais Karzai kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa wananchi wa Afghanistan.

Pongezi toka kwa viongozi wengine

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza, David Miliband amesema hotuba ya Rais Karzai inaonyesha jinsi kiongozi huyo alivyoelewa matakwa yaliyotolewa kwake. Naye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton alisema anatumai Rais Karzai ataimarisha maisha ya Wa-Afghani. ''Kwa sasa kuna uwezekano kwa Rais Karzai na serikali yake kufanya mapatano mapya na watu wa Afghanistan na kuonyesha wazi kwamba watawajibika ipasavyo na kutoa matokeo kamili, aliongeza Bibi Clinton.'' Mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya nchini Afghanistan na Pakistan, Ettore Sequi amesema hotuba ya Rais Karzai inaangazia pia vipaumbele katika njia iliyo sawa na hivyo kutoa muda kwa kiongozi huyo kuangaliwa katika utendaji wake wa kazi.

Kauli za wapinzani wa Karzai

Wakati hayo yakijiri, mpinzani wa Rais Karzai, Abdullah Abdullah ambaye amekaribishwa katika serikali mpya itakayoundwa na Karzai, ameliambia shirika la habari-Reuters kuwa hana mipango ya kukubali kujiunga na serikali hiyo mpya. Bwana Abdullah amesema yote yaliyozungumzwa leo asubuhi na Rais Karzai kuhusu kufanya mageuzi, kukabiliana na rushwa na kufanya mapatano na kurejesha usalama nchini humo ni yale yale yaliyokuwa yakizungumzwa miaka minane iliyopita na kwamba hali ya nchi hiyo imezidi kuwa mbaya. Nalo kundi la wanamgambo la Taliban limesema kitendo cha rais Karzai kuapishwa, hakina maana yoyote na hawatakubali wito wake wa kujiunga na serikali ya umoja wa kitaifa. Msemaji wa Taliban, Zabiullah Mujahid amesema siku ya leo siyo ya kihistoria na kwamba serikali ya Afghanistan haijafanya chochote kutokana na majeshi ya kigeni kuendelea kuweko nchini humo hadi sasa.

Wakati huo huo, wanajeshi wawili wa Marekani wameuawa katika shambulio la bomu la kutegwa kwenye gari kaskazini mwa Afghanistan katika muda ambao Rais Karzai alikuwa akiapishwa. Msemaji wa jeshi linaloongozwa na Jumuiya ya Kujihami-NATO, Luteni Nico Melendez, amesema gari hilo liliripuka nje ya eneo la kijeshi katika wilaya ya Shah Joy iliyopo katika jimbo la Zabul.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE/APE)

Mhariri:Abdul-Rahman