1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yasikitishwa na hukumu ya Sudan

Halima Nyanza30 Novemba 2007

Uingereza leo imeendelea na mazungumzo na Sudan ili kumaliza adhabu aliyopewa raia wake na mahakama ya Sudan ya kifungo cha siku 15, baada ya kupatikana na hatia ya kumdhihaki mtume Muhhamad kwa kumuita sanamu la dubu.

https://p.dw.com/p/CV5i
Uislamu una nguvu kubwa nchini Sudan.Picha: AP Photo

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza David Miliband amesema amefadhaishwa na hukumu hiyo na kwamba hajaridhishwa nayo, hivyo wamekuwa wakifanya mawasiliano na Sudan kumaliza suala hilo.

Aidha awali alimtaka balozi wa Sudan nchini humo kutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na adhabu hiyo.

Viongozi mbalimbali wa kidini nchini Uingereza wameilalamikia adhabu hiyo iliyotolewa na Sudan.

Askofu wa madhehjebu ya Anglikana mjini Liverpool James Jones alikuwa na haya ya kusema baada ya kutolewa hukumu hiyo:

"Tumefedheheshwa na adhabu hiyo, lakini tumefarijika kwa vile hakuchapwa viboko hadharani, na tunaamini kwamba watu watachukua hatua, kutokana na hilo kila mtu anahofu, lakini inavunja moyo zaidi kwa vile lilikuwa ni suala la kutookuelewana."

Ni Askofu wa madhehebu ya Anglikana mjini Liverpool James Jones akizungumzia kuhusiana na hukumu aliyopewa mwalimu wa Kiingereza na mahakama ya Sudan

Naye Ibrahim Mogra wa Baraza la waislamu nchini Uingereza alikuwa na haya ya kusema

‘’Na suala ambalo ningependa kuuliza mahakama na serikali ya Khartoum. Kwa namna gani kesi hiii inasaidia uislamu? Ujumbe wa aina gani? Picha gani tunaieneza kwa dini yetu na utamaduni wetu?’’

Gillian Gibbons ambaye ni mwalimu na mama wa watoto wawili, alikutwa na hatia hiyo baada ya kuthibitishwa kuwa aliwaruhusu wanafunzi wake darasani kumuita Mtume Muhammad -SAW- sanamu la Dubu.

Alikamatwa mapema wiki hii na imeelezwa kuwa adhabu kubwa ya kesi iliyokuwa ikimkabili yeye ni kifungo cha miaka sita gerezani, viboko arubaini na kulipa fidia, Gibbons ameepuka kushtakiwa kuchochea chuki na kuonyesha dharao kwa imani za dini.

Imeelezwa kuwa baada ya kumaliza kutumikia adhabu hiyo mwalimu huyo raia wea Uingereza atarudishwa nchini kwake.