1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yawatimua nchini wajumbe 4 wa kibalozi wa Russia

17 Julai 2007

Urusi inatarajiwa kutoa jibu kali kwa hatua ya jana ya Uingereza ya kuwafukuza nchini wajumbe 4 wa kibalozi wake mjini London.

https://p.dw.com/p/CB2m
David Miliband-waziri wa nje Uingereza
David Miliband-waziri wa nje UingerezaPicha: AP

Uamuizi wa jana wa Uingereza wa kuwafukuza nchini wajumbe 4 wa kibalozi wa Russia ni mkasa mwengine katika uhusiano wa misukosuko baina ya nchi hizo mbili.

Usuhuba kati ya London na Moscow umeambatana mara nyingi na visa vya ujasusi,sera za Russia na hitilafu juu ya Chechnia na kiuo cha watu wake kuwa huru.

Magazeti mashuhuri ya Russia yameieleza hatua ya Uingereza ni kutangaza “vita vya kidiplomasia”.

Russia inatazamiwa kutoa jibu haraka.

Kufukuzwa kwa wajumbe 4 wa kibalozi wa Russia mjini London, kulikotangazwa jana na waziri wa nje David Miliband ni hatua ya kwanza ya aina hiyo mnamo muda wa mwongo mmoja na kumekuja wakati wa kuzidi mvutano kati ya kambi ya magharibi na Russia.Kuchafuka huku hivi sasa kumezidi kutokana na mkasa huu mpya wa kuuliwa kwa jasusi wa zamani wa Russia aliegeuka kuikosoa Russia marehemu Alexander Litvinenko kwa kulishwa sumu mwaka jana.

Washtaki wa Uingereza waliomba

Andrei Lugovoi,jasusi wa zamani wa KGB-shirika la usalama la Urusi,apelekwe Uingereza kukabili mashtaka kwa mauaji ya Litvinenko.Russia imekataa kufanyahivyo,ikidai sheria zake haziruhusu kupelekwa mwananchi wake nchi nyengine kukabili mashtaka.

Gazeti la Uingereza la Daily Mail katika uhariri wake likauliza:Tunachagua gani sasa ?

Waziri wa nje wa Uingereza, David Milbrand jibu lake:

“Kwanza tutawaondoa nchini wajumbe 4 wa Ubalozi wa Russia mjini London.

Pili,tutachunguza upya kikomo cha ushirikiano wetu na Russia katika maswali mbali mbali na ikiwa hatua ya mwanzo tumesimamisha mazungumzo na Russia juu ya kurahisisha viza.”

Magazeti maarufu ya Russia yameueleza uamuzi wa uingereza wa kuwatimua nchini wajumbe wao 4 wa Ubalozi huko London ni sawa na kunadi vita vya kidiplomasia.gazeti la ISVESTIA linaloelemea Kremlin limejitoa na kichwa hiki cha habari:

“Waziri mkuu wa Uingereza ametangaza vita na Russia-vita vya diplomasia.”

“Hautapita muda bila kusikia jibu muwafaka kutoka Russia” liliongeza ISVESTIA.Likauliza:Uingereza kwanini inafungua safu mpya ya vita wakati haimumaliza ile ya kwanza ya kupambana na magadi wa vita vya jihadi nchini mwake ?

Mvutano wa hivi karibuni kati ya Moscow na London ulianzia 2002 alipowasili Uingereza Akhmed Zaklayev,mjumbe wa Ulaya wa rais Aslan Maskhadov, alieongoza wimbi la uhuru wa Jamhuri ya Chchenia.Akiwa ametiwa nguvuni mara tu kuwasili London baada ya Russia kutoa hati ya kimataifa ya kutiwa kwake nguvuni,Zakayev baadae aliachwa huru kwa dhamana.Mwishoe, Zakayev akapewa hifadhi ya kisiasa nchini Uingereza 2003.

Aliepalilia pia ghadhabu za Russia ni bilionea wa kirusi aishie uhamishoni Boris Berezvosky aliekuwa kigogo zamani huko Kremlin pale Russia ilipokua chini ya Boris Yeltsin.Aliposhika madaraka rais Putin,Berezvosky,hakua na turufu tena mezani.

Akituhumiwsa kunyakua fedha nyingi za seriokali,Berezovsky alikimbilia London mwaka 2000 na mara nyingi akizungumzia wazi wazi nia yake ya kurudi Russia na kumtimua Putin madarakani.

Katika mikasa yote hii 2 ,Russia ilidai watu hao 2 wapelekwe Moscow kukabili mashtaka.London haikuitikia dai hilo.

Kisa cha kuuwawa kwa Alexander Litvinenko mjini London na kunyoshewa kidole jasusi wa zamani wa Russia (KGB) kuhusika pamoja na hatua kali za Uingereza ilizotangaza jana dhidi ya Russia kunaashiria kufufuka vita baridi katika safu ya kidiplomasia na pengine sio tu kati ya London na Moscow.Ni siku chache tu zilizopita rais Putin alimtembelea rais Bush huko Marekani katika jaribio jengine la kumtuliza shetani.