1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujenzi wa makaazi watishia mazungumzo ya amani mashariki ya kati.

21 Oktoba 2010

Wapalestina waapa kutoendelea na mazungumzo ikiwa muda wa marufuku ya ujenzi hautaongezwa.

https://p.dw.com/p/PkNT
Vifaa vya ujenzi wa makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika ukingo wa magharibi.Picha: AP

Walowezi wa Kiyahudi wameanza kujenga takriban makaazi 600 tangu kukamilika kwa marufuku ya ujenzi tarehe 26 mwezi uliopita.

Hayo yanajiri wakati matumaini ya kupatikana kwa amani yakionekana kuwa finyu.

Afisa mkuu anayehusika na ujenzi wa makaazi mapya ya Walowezi wa Kiyahudi, Hagit Ofran alisema kwa makadirio yao, ujenzi wa kati ya makaazi mapya 600 na 700 umeanza katika kipindi cha mwezi mmoja na ni kasi ya mara nne ikilinganishwa na ilivyokuwa kabla ya marufuku ya ujenzi.

Mazungumzo ya amani kati ya Wapalestina na Waisraeli yanakumbwa na kitisho kikubwa cha kusambaratika kutokana na ubishi kuhusu ujenzi wa makaazi katika eneo la ardhi lililoko katika ukanda wa Gaza.

Israel imekataa kuongeza muda wa marufuku ya ujenzi na Wapalestina wamesema hawatarejelea mazungumzo ikiwa Walowezi wataendelea kujenga katika ardhi ya Wapalestina.

Bw Ofran alisema ujenzi huo unaendelezwa ili kutosheleza mahitaji ya makaazi 2000 na ni kati ya mpango wa muda mrefu wa kujenga makaazi 13,000 ambayo tayari yameidhinishwa.

Kiongozi wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas na Wanadiplomasia wa Kiarabu walikubaliana kuipa Marekani muda wa wiki kadhaa ili itafute suluhisho la kidiplomasia kuhusu mzozo huo.

Wapalestina wanailaumu vikali Israel kwa madai ya kuvuruga nafasi ya kufufua mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili. Hadi kufikia sasa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameshindwa kuongeza muda wa marufuku ya ujenzi kwa sababu chama chake kinachoegemea mrengo wa kulia hakiungi mkono azimio la kusitisha ujenzi. Kiasi ya Waisraeli laki tano wanaishi katika makaazi mia mbili katika ukanda wa Gaza likiwemo eneo la Waarabu mashariki mwa Jerusalem, maeneo yanayotizamwa na Wapalestina kama mipaka itakayokuwa ndani ya taifa waliloahidiwa.

Huku hayo yakijiri, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton amezionya Israel na Palestina kwamba hakuna njia ya miujiza ya kusitisha mkwamo katika mazungumzo ya amani lakini bidii itaweza kuleta matumaini. Bibi Clinton alikuwa akizungumza mjini Washington alipokutana na kundi la wanaharakati wa Kipalestina linalopigania kukamilika kwa mzozo wa mashariki ya kati kwa amani. Alisema mazungumzo sio rahisi lakini yana umuhimu mkubwa.

Mazungumzo ya ana kwa ana kati ya pande hizo mbili yalianza tarehe mbili Septemba na sasa kunaonekana bado kuna vikwazo vya kimsingi.

Zaidi ya hayo, utafiti uliofanywa na kituo cha Kipalestina kinachoshughulikia sera na uchunguzi na Chuo kikuu cha Kiyahudi cha Jerusalem, asilimia 30 tu ya Wapalestina ndio wana matumaini katika mazungumzo ya amani na ni asilimia sita ya Wapalestina na asilimia tano wa Waisraeli ambao wana imani kwamba kutapatikana suluhisho la kudumu.

Na bado tukikita kuhusu masuala ya mashariki ya kati, rais wa Venezuela, Hugo Chavez atakutana na mwenyeji wake, Bashar al-Assad wa Syria hii leo. Bw Chavez aliwasili nchini humo akitokea Iran alipofanya mazungumzo na rais Mahmoud Ahmadinejad. Lengo kuu la ziara yake ni kusitisha kile anakitaja kama ubepari wa mataifa ya magharibi. Chavez anatarajiwa kuondoka leo jioni kuelekea Libya.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters/DPA/Reuters

Mhariri, Josephat Charo