1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi usitishwe

27 Agosti 2009

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiendelea na ziara yake barani Ulaya,leo amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje Frank-Walter Steinmeier na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/JJaF
Bundeskanzlerin Angela Merkel und der israelischen Ministerpraesident Benjamin Netanjahu am Donnerstag, 27. August 2009, auf einer gemeinsamen Pressekonferenz im Bundeskanzleramt in Berlin. Netanjahu ist zu einem zweitaegigen Besuch in der deutschen Hauptstadt. (AP Photo/Eckehard Schulz) ---German Chancellor Angela Merkel and Israeli Prime Minister Benjamin Netanyahu at a news canference at the Federal Chancellery in Berlin, Thursday, Aug. 27, 2009. Netanyahu is in Germany for a two-day visit. (AP Photo/Eckehard Schulz
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kulia) na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin.Picha: AP

Mazungumzo yao hasa yamehusika na jitahada za kufufua majadiliano ya amani kati ya Israel na Wapalestina. Kansela Merkel mara nyingine tena ameitka Israel isitishe ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi iliyoikalia na ianzishe majadiliano ya amani pamoja na Wapalestina. Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Merkel alisema ni muhimu kuanzisha upya mchakato wa amani na akaongezea:

" Tunaamini kuwa suluhisho la kuwepo mataifa mawili yaani taifa moja la Wayahudi na moja kwa ajili ya Wapalestina ni njia pekee ya kuwa na amani katika siku zijazo."

Hapo awali Kansela Merkel alitoa wito kwa kiongozi wa Israel kuwa tayari kuafikiana. Amesema kuwa tangu rais mpya wa Marekani Barack Obama kuingia madarakani,kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana suluhisho la amani. Lakini Israel imepinga kuitikia mito ya Rais wa Marekani Barack Obama kusitisha kabisa ujenzi wa makazi hayo katika ardhi iliozikalia, ili majadiliano ya amani yaweze kuanzishwa upya. Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas ameeleza waziwazi kuwa hatorejea kwenye meza ya mazungumzo mpaka Israel itakapositisha ujenzi wa makazi hayo.

Lakini lengo kuu la ziara ya Waziri Mkuu wa Israel barani Ulaya ni kuhimiza hatua kali zaidi kuchukuliwa dhidi ya Iran. Hapo awali alipopokea hati asili, za ramani ya ujenzi wa kambi ya maangamizi ya Auschwitz, yaliyotokea wakati wa Vita Vikuu vya Pili, Netanyahu alionya kuwa mradi wa nyuklia wa Iran ni kitisho sio kwa Israel na kanda hiyo tu bali ni hatari pia kwa amani duniani. Na hilo ni suala la kutiwa maanani na jumuiya ya kimataifa.

Wakati huo huo akasema kuwa amefurahi kusikia kuwa Ujerumani inachukua jukumu la kushughulikia kitisho hicho. Netanyahu ametoa wito wa kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi ili kuishinikiza kiuchumi. Amesema madola makuu yalikawia kuchukua hatua za kuwazuia Manazi kuwaua Wayahudi milioni sita wakati wa vita vikuu vya pili. Amesema nchi inayotoa wito wa kuwateketeza Wayahudi haiwezi kuachiwa bila ya hatua kuchukuliwa.

Nchi za magharibi zinaamini kuwa lengo la mradi wa nyuklia wa Iran ni kutengeneza silaha lakini Iran inashikilia kuwa mradi huo ni kwa ajili ya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa matumizi ya umma.

Netanyahu anakamilisha ziara yake mjini Berlin leo hii kwa kutembelea Wansee ambako katika Manazi katika mwaka 1942 waliandaa mpango wa kuwateketeza Wayahudi.

Mwandishi:Martin Prema/Reuters

Mhariri:Abdul-Rahman