1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

251109 Israel Siedlungsstopp

26 Novemba 2009

Israel imesitisha kwa kipindi cha miezi kumi ujenzi wa makazi ya Wayahudi katika eneo la Ukingo wa Magharibi.Hata hivyo ujenzi wa majengo ya umma bado unaendelea kama ilivyopangwa.

https://p.dw.com/p/KgkM
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: AP

Kauli hizo zimetolewa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu baada ya kikao cha baraza la mawaziri aliyewatolea wito Wapalestina kuyafufu mazungumzo ya amani.Palestina kwa upande wake imekataa kuuitikia wito huo na kudai kuwa hakuna jipya kwani ujenzi wa makazi mia tatu ulioanzishwa bado utaendelea.

Katika mkutano na waandishi wa habari ,Waziri Mkuu Benjamin Nentanyahu alifahamisha kuwa ujenzi huo utasitishwa kwa kipindi cha miezi kumi ila hauyajumuishi majenzi ya umma yaliyoko Ukingo wa Magharibi.Kiongozi huyo aliyezungumza kwa lugha ya Kiingereza ndipo apate kueleweka na jamii ya kimataifa alisisitiza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria. Wakati huohuo Waziri Mkuu Netanyahu aliwanyoshea mkono Wapalestina na akawatolea wito wa kuyafufua mazungumzo ya kusaka amani ya eneo la Mashariki ya Kati ,''Hii ni hatua muhimu tunayopia uzito.Tunataraji kuwa uamuzi huu utachangia pakubwa katika harakati za kuisaka amani ya kudumu ili tufikie makubaliano maalum kati ya Waisraeli na Wapalestina,'' akaitetea hatua hiyo

Israel / Siedlungsbau / Gilo / Ostjerusalem
Makazi ya Wayahudi yaliyoko Gilo,Jerusalem MasharikiPicha: AP

Suala la ujenzi wa makazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi ni nyeti na lina nafasi yake katika mkwamo wa mchakato mzima wa kusaka amani ya mashariki ya kati.Marekani kwa upande wake imefurahishwa na hatua hiyo ambayo haikupokelewa kwa njia tofauti na Wapalestina.Mjumbe wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati George Mitchell alisema kuwa ni hatua muhimu,''Hatua hiyo haitosababisha ujenzi wa makazi kusimamishwa kabisa ila ni hatua kubwa ambayo haijawahi kuchukuliwa na serikali yoyote ya Israel,'' ijapokuwa ina mapungufu alieleza.

Itakumbukwa kuwa awali Israel ilitangaza kuwa imeridhia ujenzi wa makazi 900 ya ziada katika eneo la Gilo la Jerusalem Mashariki tamko lililoighadhabisha jamii ya kimataifa.Kwa mujibu wa sheria za kimataifa eneo hilo halitambuliwi kuwa ni la Israel.Israel yenyewe inaamini kuwa eneo lote la Jerusalem ni ardhi yake.Hata hivyo ujenzi wa makazi alfu 3 wa majengo ya umma uliokuwa umeshaidhinishwa utaendelea.

Kwa upande wao Wapalestina hawajafurahishwa na tamko hilo kwani hakuna jipya.Waziri Mkuu wa Palestina Salam Fayyad anayeungwa mkono na Marekani kwasababu ya juhudi zake za kuuimarisha uchumi wa Ukingo wa Magharibi pamoja na kupambana na wapiganaji wanaoishambulia Israel aliupuuza wito huo wa Israel kwasababu hatma ya eneo la Jersulem Mashariki haikutajwa.

Mahmoud Abbas George Mitchell
Rais wa Mamlaka ya Palestinian Mahmoud Abbas na mjumbe wa Marekani wa Mashariki ya Kati George MitchellPicha: AP

Wakati wa kikao cha baraza la mawaziri,uamuzi huo uliungwa mkono pia na wakosoaji wanaouegemea mrengo wa shoto.Hilo huenda likamshinikiza Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas kurejea katika meza ya mazungumzo ya .Kiasi cha watu nusu milioni wanaishi katika eneo hilo la Ukingo wa Magharibi.Katika kipindi cha miaka sita tangu mpango wa kuisaka amani ya Mashariki ya Kati-Roadmap unaosema kuwa sharti ujenzi wa makazi hayo usiendelee,kiasi cha wakazi laki moja wa ziada wamelihamia eneo hilo linalozozaniwa.

Mwandishi:Wiese Hans-Jochen-ZPR/Thelma Mwadzaya

Mhariri:Aboubakary Liongo