1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani bado haina serikali

21 Oktoba 2013

Bunge jipya la Ujerumani linakutana 22.10.2013 kwa mara ya kwanza wakati bado serikali mpya ikiwa haijajulikana.Kansela Angela Merkel na vyama vyake aendelea kutafuta mshirika kuunda serikali.

https://p.dw.com/p/1A36k
Bunge la Ujerumani,Bundestag
Bunge la Ujerumani,BundestagPicha: picture-alliance/dpa

Katiba ya Ujerumani inasema kwamba sio zaidi ya siku 30 baada ya uchaguzi bunge jipya linabidi kukutana.Kesho Jumanne Tarehe 22 kwahivyo zinatimia siku 30 tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu. Ikiwa bunge hilo litakutana katika kikao chake cha ufunguzi itamaanisha serikali iliyokuweko madarakani imemaliza muda wake.Hata hivyo hadi sasa Kansela Angela Merkel na chama chake cha Christian Demokratic Union CDU na ndugu zao Christian Social Union CSU bado hawajapata mshirika wa kuunda nao serikali.Mazungumzo na chama cha Kijani yameshindwa wakati majadiliano na Social Demokratic SPD yanaendelea.

Merkel kuendelea na uongozi

Haina maana kwamba Ujerumani kufumba na kufumbuwa itakuwa bila ya kiongozi.Kimsingi hilo haliwezi kutokea anasema Timo Grunden mtaalamu wa masuala ya kisiasa kutoka chuo kikuu cha Giesen.Sheria ya Ujerumani iko wazi katika suala hili ambapo ikiwa serikali mpya itashindwa kupatikana basi ile iliyoko sasa itabidi kuendelea kuongoza hadi pale serikali mpya itakapopatikana.

Kansela Angela Merkel pamoja na mawaziri wake wanaruhusiwa kikatiba kuendelea kuongoza na katika kipindi hiki rais wa taifa Joachim Gauck anabeba dhima kubwa.Analazimika kuingilia kati katika mazungumzo na vyama na kutafuta serikali mpya ya muda.

Jengo la Bunge la Ujerumani Bundestag mjini Berlin
Jengo la Bunge la Ujerumani Bundestag mjini BerlinPicha: AFP/Getty Images

Ukosoaji

Hata hivyo Timo Grunden mtaalamu wa siasa anaiona hatua hiyo kama isiyokuwa ya kidemokrasia anasema rais hana mamlaka ya kidemokrasia katika bunge jipya lililochaguliwa.Na kwa maana hiyo sio tu anapoteza uhalali lakini pia kidemokrasia hana mamlaka.Hata hivyo kwa hivi sasa kila kitu kinakwenda kama mwanzoni kwasababu serikali ya muda nayo ina haki na mamlaka sawa kama serikali iliyochaguliwa.

Lakini serikali hiyo ya muda itabidi kuyaweka kando na kutoyajadili baadhi ya masuala muhimu ya kisiasa na pia baadhi ya maamuzi hayawezi kupitishwa kwasababu maamuzi hayo pengine huenda yakafikiwa kivingine hapo baadae.Mtaalamu huyo wa kisiasa anasema serikali ya mpito haiwezi kuanzisha mchakato wa kufikia maamuzi fulani kwasababu mtu hawezi kujuwa ikiwa serikali yake itakuwa na wingi katika bunge.

Kutokana na suala hilo wengi wanamkosoa Kansela Angela Merkel kwa kuendelea kutangaza msimamo aliokuwa nao katika serikali iliyopita mbele ya Umoja wa Ulaya kwamba sheria zilizopendekezwa kuhusu kiwango cha moshi unaotoka kwenye magari katika nchi hizo za Umoja wa Ulaya kwasasa hakiwezi kukubalika.Timo Grunden lakini haoni hilo kuwa ni tatizo anasema ni wajibu wake Kansela na pia ana haki kuendelea kuyasimamia maslahi ya Ujerumani katika ngazi ya Kimataifa.

Waziri wa Uchukuzi Peter Ramsauer (CSU, l),Waziri mkuu wa Jimbo la Nordrhein-Westfalen, Hannelore Kraft (SPD), na Ronald Pofalla (CDU)
Waziri wa Uchukuzi Peter Ramsauer (CSU, l),Waziri mkuu wa Jimbo la Nordrhein-Westfalen, Hannelore Kraft (SPD), na Ronald Pofalla (CDU)Picha: picture-alliance/dpa

Katika kipindi cha mpito kilichokuweko baina ya muda ulipofanyika uchaguzi mkuu na mchakato wa kutafuta serikali mpya kumekuweko daima kipindi kifupi ambapo serikali ya muda imekuwa madarakani.Mradi tu hakuna masuala muhimu yanayohitaji maamuzi basi hamna tatizo lolote.Itakumbukwa kwamba baada ya uchaguzi wa mwaka 1998 kulikuwa hakuna muda wa kupoteza,mzozo wa Kosovo ulichukuwa nafasi ya usoni huku Marekani ikiingilia kati kijeshi.Ujerumani ilikuwa ikiongozwa na serikali ya zamani chini ya Helmut Kohl wa chama cha CDU ikisubiri serikali mpya ya vyama vya SPD na Kijani iliyongozwa na Gerhard Schroeder ambayo ilikuwa bado haijaingia madarakani.

Mazungumzo rasmi ya kuunda serikali ya mseto safari hii kati ya CDU/CSU na SPD asasa yaataanza Jumatano wiki hii.

Mwandishi Seiffert Jeannette/Saumu

Mhariri AbdulRahman