1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani "iko huru kuikosowa Uturuki."

15 Mei 2016

Mwanadiplomasia mkuu wa Ujerumani ametupilia mbali madai kwamba serikali imekuwa ikiiridhia mno Uturuki kwa ajili ya kutaka kutekelezwa kwa makubaliano tata ya wahamaji kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1IoIS
Picha: picture-alliance/dpa/Turkish President Press Office/H

Katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la "Der Spiegel " yaliochapishwa Jumapili (15.05.2016) waziri wa mambo wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier amekanusha kwamba serikali ya Ujerumani imekuwa ikijaribu kuiregezea Uturuki wakati wa kujadiliana nayo masuala magumu kwa kuhofia kuvuruga makubaliano ya wahamiaji kati ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya.

Ameliambia gazeti hilo kwamba "Tuatendelea kuzungumzia matukio yanayokwenda kinyume na inavyostahiki nchini Uturuki, kuhusu vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari."

Uturuki katika miezi ya hivi karibuni imekuwa ikikabiliwa na shutuma kali kwa kuwachukulia hatua za kisheria waandishi wa habari wenye kuandika habaria za kisiasa kwa mtazamo wa kukosowa serikali na kuwazuwiya waandishi wa habari wa kigeni nchini humo.

Kama sehemu ya makubaliano yake na Umoja wa Ulaya yaliofikiwa mwezi wa Machi serikali ya Uturuki imekuwa ikiwazuwiya watu wanaowasafirisha wakimbizi na wahamiaji kwa magendo kuutumia mwambao wake kuwaingiza katika ardhi ya Umoja wa Ulaya kwenye visiwa vilioko karibu vya Ugiriki.

Mpira uko kwa Uturuki

Steinmeier amesema maslahi ya Uturuki katika makubaliano hayo yasidharauliwe ambayo yataipatia Uturuki zaidi ya euro bilinioni 3 kudhibiti wimbi la wahamiaji na wananchi wa Uturuki kusafiri bila ya viza katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.Picha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Amesema masharti ya Umoja wa Ulaya kwa Uturuki kuregezewa upatikanaji wa visa kwa wananchi wake yanatambuliwa na serikali ya nchi hiyo kwa kuwa yamejadiliwa pamoja na serikali hiyo na kuongeza kuwa "mpira sasa uko upande wa Ututuki".

Amesema "serikali ya Uturuki itabidi ijibu masuali yaliko wazi "

Mzozo wa kidiplomasia

Matamshi hayo ya Steinmeier yanakuja wakati kukiwa na mzozo kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya juu ya kigezo kinachotakiwa kutimizwa na nchi hiyo ili wananchi wa nchi hiyo wasafiri bila ya kuhitaji visa katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Bendera ya Umoja wa Ulaya (kushoto) na ya Uturuki.
Bendera ya Umoja wa Ulaya (kushoto) na ya Uturuki.Picha: Getty Images/C. McGrath

Umoja wa Ulaya unaitaka serikali ya Uturuki kuregeza sheria yake ya kupambana na ugaidi ikiwa ni mojawapo ya masharti 72 yaliokubaliwa mwezi wa Machi ili kuwawezesha raia wake wasafiri Ulaya bila ya kuhitaji visa.

Uturuki imekataa kuzifanyia marekebisho sheria zake za kupambana na ugaidi na imetishia kuyavunja makubaliano hayo iwapo Umoja wa Ulaya utaendelea kun'gan'gania sharti hilo.

Umuhimu wa Uturuki

"Aidha tupende au tusipende ,Uturuki inaendelea kuwa nchi muhimu kwa wahamiaji wanaokimbilia Ulaya. Tunahitaji kuwa na ushirikiano fulani nayo iwapo tunataka kuepuka hali kama ile tuliyoishuhudia mwaka jana ."amesema Steinmeier akikusudia wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi waliokimbilia Ulaya mwaka 2015.Ujerumani pekee iliwapokea watafuta hifadhi takriban milioni 1.1 mwaka 2015.

Wahamiaji wanaorudishwa Uturuki kutoka kisiwa cha Lesbos, Ugiriki.
Wahamiaji wanaorudishwa Uturuki kutoka kisiwa cha Lesbos, Ugiriki.Picha: picture alliance/abaca/AA

Idadi ya watu wanaojaribu kuingia Ulaya kupitia Uturuki wengi wao wakiwa wakimbizi kutoka nchi iliyokumbwa na vita ya Syria imepunguwa sana tokea makubaliano hayo yaliokosolewa mno yaanze kutekelezwa Machi 20.

Wimbi la wahamiaji wanaokimbilia Ulaya limechochea kuongezeka kwa wafuasi wa sera kali za mrengo wa kulia barani kote Ulaya. Nchini Ujerumani chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD) kilichoanzishwa hapo mwezi wa Februari mwaka 2013 kimepata uunganji mkono mkubwa kutoka kwa wale wanaokosowa sera ya Kansela Angela Merkel ya kuacha milango wazi kwa wahamiaji wanaokimbia vita nchini Syria.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dps/AFP

Mhariri : Bruce Amani