1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani imeunyoosha mkono wa msaada

14 Septemba 2011

Ujerumani imetoa msaada wa dola milioni 300 kuwasaidia wahanga wa baa la njaa na ukame katika pembe ya Afrika

https://p.dw.com/p/12Yth
Athari kubwa zimedhihirika za baa la njaa katika pembe ya AfrikaPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Ujerumani imewapongeza viongozi wa mataifa ya Mashariki na Pembe ya Afrika kwa kutia saini azimio lenye lengo la kukomesha athari za ukame wa mara kwa mara katika eneo hilo.

Kenia Dürre in Ostafrika Flüchtlingslager in Dadaab Kind
Picha: dapd

Balozi wa Ujerumani nchini Kenya, Bi Margit Helwig-Boette amesema hayo kwenye mkutano na waadishi na habari katika makazi yake mjini Nairobi.

Balozi huyo wa Ujerumani amesema mkakati ulioafikiwa kwenye mkutano wa viongozi uliofanyika juma lililopita mjini Nairobi unaambatana na mwelekeo uliotolewa na Ujerumani wakati wa ziara yake waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo Dirk Niebel mwezi uliopita nchini Kenya ambapo alitangaza msaada wa Euro Milioni 118 kufadhili miradhi ya kukabiliana na athari za ukame.

Balozi Margit amesema Ujerumani ikiwa mstari wa mbele katika ushirikiano wa kimaendeleo na Kenya imesaidia wahanga wa baa la njaa na ukame na wakati huu imetenge Dola milioni 300. Huu ni msaada wa muda mfupi lakini lengo letu ni kutafuta suluhisho la kudumu kwa tatizo la Ukame.

Sehemu ya msaada huo imepangiwa mipango ya dharura kwa wakimbizi kutoka Somalia na nchi zinazowapokea huku sehemu nyingine ikilenga miradi ya uzalishaji chakula kwa ushirikiano na Shirika la IGAD kwa lengo la kuzuia mizozo.

Geberkonferenz der Afrikanischen Union zur Hungersnot in Ostafrika
Katibu mkuu wa IGAD, Mahbub Mualem, kushoto, na rais wa mpito Somalia Sheik Sharif Sheik AhmedPicha: dapd

Akipongeza hatua hiyo Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya Abbas Gullet amesema nchi kama Kenya haingetegemea misaada endapo kungekuwa na sera mwafaka za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Huku hayo yakijiri Rais wa Ujerumani Christian Wulff ametuma risala za rambirambi kwa watu wa Kenya kufuatia mkasa wa moto uliosababisha vifo vya watu wapatao 100 na wengine 120 kujeruhiwa katika mtaa wa mabanda wa Sinai mjini Nairobi.

Serikali ya ujerumani imeahidi kutoa msaada kwa hospitali kuu ya Kenyatta ambako wahanga 76 wa mkasa huo wamelazwa wakiwa na mejeraha mabaya ya moto.

Mkasa huo ulitokea siku ya Jumatatu wakati wakaazi wa mtaa huo walipokuwa wakichota mafuta ya petrol yaliyokuwa yakivuja kutoka kwa bomba la mafuta linalomilikiwa na Kampuni ya Kenya Pipeline.

Kufuatia mkasa huo, Serikali ya Kenya imetangaza siku mbili za kuomboleza kuanzia leo hadi kesho.

Mwandishi: Alfred Kiti DW Nairobi.
Mhariri:Josephat Charo