1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuboresha hatua za usalama

27 Desemba 2016

Wanasiasa kutoka pande zote zinazounda serikali ya muungano ya Ujerumani, wametoa mwito wa serikali kuongezewa mamlaka ya kuwarejesha makwao waombaji hifadhi ambao wamekataliwa

https://p.dw.com/p/2UvTp
Deutschland Flüchtlinge kommen an der ZAA in Berlin an
Wahamiaji wakiingia mji wa Berlin nchini UjerumaniPicha: Getty Images/S. Gallup

Wanasiasa hao wametaka kurejeshwa haraka waomba hifadhi wanaoonekana kuwa kitisho kwa usalama, huku wengine wakisisitiza kuimarishwa kwa hatua za kuwafuatilia na kuwachunguza waombaji wa aina hiyo. 

Kansela Angela Merkel ambaye sera zake za milango wazi kwa wahamiaji zinakabiliwa na ukosoaji mkubwa kwa kuwa zinahatarisha hali ya usalama, ameahidi kuweka sheria mpya za uhamiaji kama itatakikana kufanya hivyo, hasa baada ya shambulizi la kigaidi kwenye soko la Krismas la Berlin lililotokea mapema wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu 12.

"Na kuhusu suala la Amri linaloibua maswali mengi ambayo si tu yanalenga tukio alilofanya, lakini pia tangu alipoingia Ujerumani mwaka jana. tunalazimika sasa kuangalia namna serikali inavyohitaji kubadilisha hatua zake. Nimemtaka waziri wa mambo a ndani Thomas de Maiziere kwa kushirikiana na vyombo vingine vya sheria na usalama kulichambua suala hili na kuwasilisha matokeo mara baada ya kukamilisha"

Mtuhumiwa wa shambulizi hilo, raia wa Tunisia Anis Amri, aliyekuwa akiomba hifadhi nchini Ujerumani, alifanikiwa kutoroka kwenye kambi ya wanaorejeshwa makwao, baada ya maombi yake kukataliwa. Aliuwawa kwenye majibizano ya risasi na polisi mjini Milan, Italia, Ijumaa iliyopita.

Deutschland Anschlag mit LKW auf Weihnachtsmarkt in Berlin
Lori lililotumiwa na Amri kwenye shambulizi la soko la Krismas la BerlinPicha: Reuters/P. Kopczynski

Washirika wa Merkel kutoka jimbo la Bavaria, Chama cha Christian Social Union, CSU, wametaka kuongezwa kwa mamlaka makubwa zaidi kwa jeshi la polisi na taasisi za kiusalama, ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa mpango wa kubadilishana taarifa kati yao. "Tunahitaji kuwa na mikakati mipya ya kuwakamata watu hatari" wanasema kwenye waraka wao walioupa jina: "Usalama kwa uhuru wetu". Suala hili litakuwa sehemu kuu ya mjadala watakapokutana mapema mwezi ujao.

Miito tofauti ya kuboresha usalama.

CSU inataka taasisi za usalama kuwa na uwezo wa kumfuatilia mtu mmoja mmoja wa kuanzia umri wa miaka 14 ili kuepusha misimamo mikali, na pia kuimarishwa kwa hatua za kuwatia kizuizini watu wanaorejeshwa makwao. Kiasi cha watu 550 wameorodheshwa na taasisi za usalama za nchini Ujerumani kama watu hatari.

Wakati wanasiasa kutoka Chama cha Kijani ambao tangu shambulizi la Berlin wakipinga mwito wa kuongezwa kwa kamera za vidio kwenye maeneo ya umma kwa kusema hilo sio jibu la matatizo ya kiusalama, kura ya maoni iliyoendesha na taasisi ya YouGov ilionesha asilimia 60 ya Wajerumani walikubaliana na mwito huo.

Kumeendelea kuwepo kwa msukumo dhidi ya Merkel wa kumtaka kufikia makubaliano na nchi za kaskazini mwa Afrika ya kuwarejesha nchini mwao waombaji hifadhi waliokataliwa, hali ambayo imesalia kuwa kizuizi cha kurejeshwa makwao ikiwa ni pamoja na Amri, ambaye alikataliwa kupokelewa na Tunisia.

Aidha, wanasiasa waandamizi nchini hapa wametaka kuimarishwa kwa ulinzi wa mipakani ili kukabiliana na kuingia kwa idadi kubwa ya wahamiaji. Msemaji wa masuala ya ndani wa serikali ya Merkel, Steffan Siebert, amekiambia kituo cha redio cha Deutschlandfunk leo hii kwamba wanatambua kitisho cha hali ya juu kwa sasa, na hawana la kufanya zaidi ya kuimarisha ulinzi wa mipakani.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, ameliambia gazeti la Bild am Sonntag kwamba anataraji kuimarisha ulinzi wa mipakani, ingawa hatua hiyo itahitaji kuridhiwa na tume tendaji ya Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Lilian Mtono/AP/RTRE.
Mhariri: Mohammed Khelef