1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuchukua hatua dhidi ya ujasusi wa Marekani

2 Julai 2013

Wakati hasira zikipanda barani Ulaya juu ya taarifa zilizovuja kwamba Marekani imekuwa ikiyatega mawasiliano ya maafisa wa Umoja wa Ulaya, Ujerumani inasema jambo hilo likithitibishwa, basi halitakubalika.

https://p.dw.com/p/19033
GettyImages 170293810 NEW YORK, NY - JUNE 10: A supporter holds a sign at a small rally in support of National Security Administration (NSA) whistleblower Edward Snowden in Manhattan's Union Square on June 10, 2013 in New York City. About 15 supporters attended the rally a day after Snowden's identity was revealed in the leak of the existence of NSA data mining operations. (Photo by Mario Tama/Getty Images)
Bildergalerie WhistleblowerPicha: Getty Images

Kwa mujibu wa msemaji wa Kansela Angela Merkel, Steffen Siebert, serikali ya Ujerumani inalichukulia jambo hili kwa hadhari na umuhimu wa hali ya juu, kabla ya kuchukua hatua zozote dhidi yake, bali likithibitika litakuwa na matokeo mabaya kwa mahusiano ya kijadi kati ya Marekani na Ulaya.

“Kimsingi ripoti si lazima ziwe ukweli, lazima kwanza zichunguzwe, lakini lau zikithibitika kwamba balozi za Umoja wa Ulaya au nchi binafsi zimekuwa zikipelelezwa, lazima tusema wazi kwamba angalia rafiki yetu Marekani, hili halikubaliki na haliwezekani. Hatuko tena kwenye enzi za vita baridi.”

Akiwa jijini Dar es Salaam, Tanzania, hapo jana Rais Barack Obama wa Marekani, alionekana kutetea kile kilichovujishwa na mfanyakazi wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani, Edward Snowden, na kuchapishwa na jarida la Der Spiegel la hapa Ujerumani, kwamba Marekani imekuwa ikiwapeleleza maafisa wa kibalozi wa Umoja wa Ulaya, kwa kuyatega mawasiliano yao ya mitandao na simu.

Obama azungumzia kashfa

Rais Obama alisema kwa namna moja ama nyengine hiyo ndiyo maana ya kuwa na taasisi ya ujasusi kwa nchi yoyote ulimwenguni.

Rais Barack Obma wa Marekani.
Rais Barack Obma wa Marekani.Picha: DW/L. Schadomsky

“Ninadhani tunapaswa kukisia kwamba kila shirika la ujasusi, sio letu tu, bali kila shirika la ujasusi la Ulaya, la Asia na popote palipo na shirika kama hilo, kuna kitu kimoja wanaokifanya wote: watakuwa wanajaribu kuuelewa ulimwengu vyema zaidi na kile kinachoendelea kwenye miji mikuu duniani kupitia vyanzo ambavyo havipatikani kwenye gazeti la New York Times au televisheni ya NBC News. Wanatafuta taarifa za ziada ya kile kipatikanacho kweupe. Kama si hivyo, kusingelikuwa na haja ya kuwa na mashirika ya kijasusi.” Alisema Obama.

Hata hivyo, akijibu masuali ya waandishi wa habari juu ya taarifa hizo zilizoyakasirisha mataifa ya Ulaya, Obama alisema kwamba ameshaliagiza shirika la ujasusi na timu yake kufuatilia suala zima lilivyo na kama kuna majibu ya kutoa kwa washirika wao wa Ulaya, basi watafanya hivyo mara moja.

Taarifa zinasema kwamba Kansela Angela Merkel atazungumza na mwenzake wa Ufaransa, Francois Hollande, kwa kile ambacho Steffen Siebert amekiita kuchukua muelekeo wa pamoja kwenye suala hili tete.

Katika toleo lake la hapo Jumamosi, jarida la Der Spiegel lilisema hakuna ofisi yoyote ya Umoja wa Ulaya inayoweza kuepuka kuchunguzwa na Shirika la Ujasusi la Marekani, zikiwemo zile za Brussels na Washington.

Kwa mujibu wa jarida hilo, hata Kansela Merkel mwenyewe alikuwa akichunguzwa, kama ilivyo kwa mamilioni ya raia wa kawaida wa Ujerumani.

Kiujumla, Shirika hilo la Kijasusi la Marekani, linasemekana kukusanya taarifa nusu bilioni kwa mwezi kutoka Ujerumani pekee.

Mwandishi: Bettina Marx/DW Berlin
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Oummilkheir Hamidou