1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuendelea kuisaidia Tanzania

Christopher Buke22 Novemba 2006

Ni katika sekta ya afya kupambana na ukoma, kifua kikuu.

https://p.dw.com/p/CHm6

Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la Kijerumani linalojihusisha na mapambano dhidi ya magonjwa ya kifua kikuu na ukoma GLRA imetoa msaada wa magari 5 na piki piki 34 kwa serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya na ustawi wa Jamii.

Akizungumza wakati wa Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bwana Wolfgang Ringe aliahidi kuwa wananchi wa nchi yake wataendelea kutoa misaada ya namna hiyo ili kuzisaidia nchi kama vile Tanzania ili kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Akielezea hali ya magonjwa ya kifua kikuu na ukoma nchini Tanzania, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wa Tanzania Profesa David Mwakysa alisema licha ya kuwa serikali yake imekuwa ikiendeleza mapambano dhidi ya magonjwa haya lakini akaonya kasi ya kifua kikuu inapanda.

Alisema kuwa hali ilionekana kuleta matumaini mwaka 1980 baada ya nchi kuonekana kuanza kuudhibiti ugonjwa huo ambapo walirekodiwa wagonjwa 11,000 tu.

Anasema kutokana na kuongezeka kasi ya maambukizo ya virusi vya hiv na ukimwi idadi ya watu walioambukizwa kifua kikuu imepanda hadi watu 65,000 mwaka 2005.

Anasema wataalamu wa afya Tanzania wanaangalia maambukizo haya kwa tahadhari na hivyo akaishukuru serikali ya ujerumani kuwa msaada huo wa magari na piki piki umekuja kwa wakati mwafaka.

Balozi Ringe kwa upande wake anasema ugonjwa wa kifua kikuu ungali ukichukuliwa kama kitisho kwa walimwengu hata na mataifa makubwa kama vile nchi yake Ujerumani.

“Hata katika mataifa makubwa kama vile Ujerumani uzoefu hasa baada ya vita, unaonyesha jinsi kifua kikuu ulivyo ugonjwa wa kufisha, na ndio sababu watu katika ujerumani wataendelea kutoa fedha kwa GLRA kwa ajiri ya kusaidia nchi kama vile Tanzania kwa mapambano yake dhidid ya TB na ukoma”.

Lakini wakati hali inazidi kutisha upande wa maambukizo ya kifua kikuu, Waziri Mwakyusa anasema hali inatia matuamini sana upande wa ukoma.

Anasema Tanzania inazidi kuutokomeza ugonjwa huo lwamo lengo la dunia lilikuwa ni kutokomeza ugonjwa huu alau asalie mtu mmoja tu kati ya kila watu 10,000.

Waziri anasema kwa lengo hili Tanzania imesogea pazuri sana maana hivi sasa nchini ni mtu 1.1 katika kila watu 10,000.

Akizidi kutoa shukurani za Tanzania kwa wananchi wa Ujerumani ambao ndio hutoa michango kwenye taasisi ya GLRA Waziri Mwakyusa aliwaambia waandishi wa habari kuwa sio kuwa ujerumani imekuwa ikitoa misaada ya magari na piki-piki tu bali vipuri na gharama za kuendesha magari na piki-piki hozo.

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka kutoa shukrani hizi kwa njia ya maandishi shukrani kwa watu wenu, wa Ujerumani na hasa GLRA kwa kuendelea kutoa msaada hasa katika muda kama huu ambapo tupo katika hitaji kubwa” aliongezea waziri Mwakyusa.

Haikujulikana mara moja gharama za ununuzi wa magari hayo ambayo ni aina ya Land-cruise hard board na Piki-piki aina ya Honda sport lakini land Cruser ya aina hiyo hapa Tanzania ni shilingi milioni 32 kila moja wakati piki-piki moja ya aina hiyo huuzwa shilingi milioni 4.5

Balozi Ringe alikumbusha kuwa ujerumani hutoa misaada ya magari 5 kila baada ya miaka 5 kusaidia sekta hiyo wakati piki-piki hubadilishwa kila baada ya miaka 3 na kuongeza kuwa nchi yake kupitia GLRA imekuwa ikifanya hivyo kwa miaka 45.

Magari hayo matano yaliyotolewa November 20, 20006 jijini Dar es salaam yanapelekwa kwenye mikoa ya Manyara, Mwanza, Ruvuma na moja Zanzibar.

Kwa zile piki piki 34 zitatumwa kwenye sehemu wilaya mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar.

Mwisho.