1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuendelea kuunga mkono mkataba wa Paris

Lilian Mtono
2 Juni 2017

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema Ujerumani itaendelea kuunga mkono mkataba wa kimataifa wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi katika wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump anapoamua kuiondoa Marekani.

https://p.dw.com/p/2e234
Angela Merkel PK Klimaabkommen
Picha: Reuters/F.Bensch

Kansela Merkel amesema makubaliano hayo yalikuwa ni msingi wa mikakati ya kulinda dunia.

Merkel amewaambia waandishi wa habari kwamba hakuna anayeweza kurudi nyuma katika mikakati hiyo iliyoanza tangu mwaka 1997, enzi ya mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Kyoto na hatimaye mkataba huo wa kihistoria wa Paris wa mwaka 2015.

Ufaransa ambayo ilikuwa mwenyeji wa mkataba wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyofikiwa katika mji wa Paris mwaka 2015 imeapa leo hii kwamba itaongeza mara mbili juhudi zake za kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa pamoja na kuzihimiza nchi nyingine zilizotia saini makubaliano hayo kuunga mkono juhudi hizo. 

Waziri wa Mazingira wa Ufaransa, Nicolas Hulot, amesema hayo masaa machache baada ya Rais Donald Trump  wa Marekani kuthibitisha mipango yake ya kuliondoa taifa hilo la pili kwa uzalishaji wa hewa ukaa kutoka katika makubaliano hayo ya Paris kwa madai kwamba hayakuwa na manufaa yoyote kwa uchumi wa Marekani na yanadhoofisha uhuru wake.

USA Trump verkündet Ausstieg aus Pariser Klimaschutzabkommen
Donald Trump baada ya kutangaza kuiondoa Marekani katika mkataba wa ParisPicha: Reuters/K. Lamarque

Jana jioni, Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni, Kansela Merkel wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa waliwataka washirika wenzao kwenye makubaliano hayo kuongeza kasi katika harakati za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuahidi kufanya mengi zaidi ili kusaidia nchi zinazochipukia kiuchumi kukabiliana na hali hiyo.

Macron mwenyewe alinukuliwa alipozungumza kwenye televisheni jana usiku akilaani hatua hiyo ya Trump. Alipozungumza katika hotuba tofauti kwa lugha ya Kiingereza, aliwaalika wanasayansi wa Marekani na watafiti wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwenda Ufaransa, huku akitumia moja ya misemo ya Trump inayosema ni muda sasa wa "kuifanya dunia kuwa imara tena".

Kwa upande wake, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Japan, Fumio Kishida, ameeleza kusikitishwa na hatua hiyo ya kuondoka kwa Marekani katika mkataba huo. Kishida amewaambia waandishi wa habari leo hii kwamba Japan ilitarajia kushirikiana na Marekani katika utekelelezaji wa mkataba huo. 

Mtangulizi wa Trump, Barack Obama, naye amekosoa hatua hiyo kwa kusema Marekani inaungana na mataifa machache yaliyokataa kusiani makubaliano hayo, ambayo ni Nicaragua na Syria. Hillary Clinton, aliyekuwa mpinzani wa Trump kwenye kinyang'anyiro cha urais, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwa kuiita hatua hiyo kuwa ni kosa la kihistoria.

Hata hivyo, Urusi ambayo awali ilieleza nia ya kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa mkataba huo, muda mfupi uliopita imesema mkataba huo hautekelezeki bila ya ushiriki wa Marekani, kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi, RIA, lililomkariri msaidizi wa Ikulu ya Kremlin, Andrei Belousov. 

Mwandishi: Lilian Mtono/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef